1 Wafalme 22

1 Wafalme 22

Shauri la Ahabu na Yosafati la kuwapelekea Washami vita.

(2-35: 2 Mambo 18:2-34.)

1Wakakaa miaka mitatu, Washami na Waisiraeli wasipopigana.[#1 Fal. 22:41.]

2Ikawa katika mwaka wa tatu, akashuka Yosafati, mfalme wa Wayuda, kuja kwake mfalme wa Waisiraeli.[#Yos. 21:38.]

3Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipowaambia watumishi wake: Je? Mwajua, ya kuwa Ramoti wa Gileadi ni wa kwetu? Nasi tunajikalia tu tukiacha kuuchukua mkononi mwa mfalme wa Washami?

4Alipomwuliza Yosafati: Utakwenda pamoja na mimi Ramoti wa Gileadi kupiga vita? Yosafati akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, nao farasi wangu ni kama farasi wako.[#2 Fal. 3:7; 2 Mambo 19:2.]

5Kisha Yosafati akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Uliza leo hivi, Bwana atakavyosema!

6Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipowakusanya wafumbuaji, watu 400, akawauliza: Niende Ramoti wa Gileadi kupiga vita, au niache? Wakasema: Panda tu! Bwana atautia mkononi mwa mfalme.

7Yosafati akauliza: Huku hakuna tena mfumbuaji wa Bwana, tumwulize naye?[#2 Fal. 3:11.]

8Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: Yuko bado mtu mmoja wa kumwuliza neno la Bwana, lakini mimi ninamchukia, kwani hanifumbulii mema, ila mabaya tu, ndiye Mikaya, mwana wa Imula. Yosafati akasema: Mfalme asiseme hivyo!

9Ndipo, mfalme alipomwita mtumishi mmoja wa nyumbani, akamwambia: Piga mbio kumwita Mikaya, mwana wa Imula!

10Mfalme wa Waisiraeli na Yosafati, mfalme wa Wayuda, walikuwa wamekaa kila mmoja katika kiti chake cha kifalme na kuvaa mavazi, wakawa wakikaa hapo pa kupuria ngano penya lango la kuuingilia mji wa Samaria, nao wafumbuaji wote wakawa wakifumbua mbele yao.

11Ndipo, Sedekia, mwana wa Kenaana, alipojifanyizia pembe za chuma, akasema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa pembe kama hizi utawakumba Washami, mpaka uwamalize.

12Nao wafumbuaji wote wakafumbua hivyo kwamba: Upandie Ramoti wa Gileadi! Utafanikiwa, naye Bwana atautia mkononi mwake mfalme!

13Yule mjumbe aliyekwenda kumwita Mikaya akamwambia kwamba: Tazama, maneno ya wafumbuaji ni kinywa kimoja tu cha kufumbua mema yatakayomjia mfalme. Basi, neno lako nalo na liwe kama neno la mmoja wao hao, useme mema yatakayokuwa.

14Mikaya akasema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, nitasema hayo tu, Bwana atakayoniambia.

Mfumbuaji Mikaya anamkataza mfalme kwenda vitani.

15Alipofika kwake mfalme, mfalme akamwuliza: Mikaya, twende Ramoti wa Gileadi kupiga vita, au tuache? Akamwambia: Upandie tu! Utafanikiwa, naye Bwana atautia mkononi mwake mfalme.

16Mfalme akamwambia: Nimekuapisha mara nyingi, usiniambie mengine katika Jina la Bwana, isipokuwa iliyo ya kweli.

17Ndipo, aliposema: Nimewaona Waisiraeli, nao walikuwa wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Bwana akasema: Hawa hawana bwana, na warudi na kutengemana kila mtu nyumbani kwake.

18Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: Sikukuambia: Hanifumbulii yatakayokuwa mema, ila yatakayokuwa mabaya tu?[#1 Fal. 22:8.]

19Mikaya akasema: Lakini lisikie neno la Bwana! Nimemwona Bwana, akikaa katika kiti chake kitukufu, navyo vikosi vyote vya mbinguni vilisimama mbele yake, kuumeni na kushotoni kwake.[#Ufu. 5:11.]

20Bwana akauliza: Yuko nani atakayemponza Ahabu, aje kuupandia Ramoti wa Gileadi, aangushwe huko? Wakajibu, mmoja akisema hivi, mmoja hivi.

21Kisha akatokea roho, akasimama mbele ya Bwana, akasema: Mimi nitamponza. Bwana akamwuliza: Kwa nini?[#Yes. 19:14.]

22Akasema: Nitatoka kuwa roho ya uwongo vinywani mwa wafumbuaji wake wote. Bwana akasema: Utamponza kweli, utaweza hivyo, toka kufanya hivyo![#Yoh. 8:44; Ufu. 16:14.]

23Sasa tazama! Bwana ametia roho ya uwongo vinywani mwa hawa wafumbuaji wako wote, maana yeye Bwana amekwisha kukutakia mabaya.

24Ndipo, Sedekia, mwana wa Kenaana, alipomkaribia Mikaya, akampiga makofi na kumwuliza: Roho ya Mungu imeshika njia gani, inipite mimi, ije kusema na wewe?

25Mikaya akasema: Jiangalie! Utaviona siku hiyo, utakapoingia chumba kwa chumba, upate kujificha.

26Mfalme wa Waisiraeli akasema: Mchukue Mikaya, mrudishe kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoasi, mwana wa mfalme,

27useme: Hivi ndivyo, mfalme anavyosema: Mwekeni huyu kifungoni, mmpe chakula cha mahangaiko na maji ya mahangaiko, hata nitakapofika salama.

28Mikaya akasema: Kama utarudi salama, Bwana hakusema kinywani mwangu. Kisha akasema: Lisikieni hili, ninyi makabila yote!

Kufa kwake Ahabu.

29Kisha mfalme wa Waisiraeli na Yosafati, mfalme wa Wayuda, wakaupandia Ramoti wa Gileadi.

30Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: Nitavaa nguo nyingine, niingie penye mapigano, lakini wewe zivae nguo zako! Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipovaa nguo nyingine, kisha akafika penye mapigano.

31Naye mfalme wa Ushami alikuwa amewaagiza wakuu wake wa magari 32 kwamba: Msipigane na mtu ye yote, mdogo kwa mkubwa, ila mpigane na mfalme wa Waisiraeli peke yake tu!

32Ikawa, wakuu wa magari walipomwona Yosafati wakamwazia yeye kuwa mfalme wa Waisiraeli, wakamgeukia kupigana naye; ndipo, Yosafati alipopiga yowe.

33Ikawa, wakuu wa magari walipoona, ya kuwa siye mfalme wa Waisiraeli, wakarudi na kuacha kumfuata.

34Kulikuwa na mtu, akauvuta upindi wake kwa kubahatisha tu, akampiga mfalme wa Waisiraeli hapo, vyuma vya kisibau chake vilipounganishwa. Ndipo, alipomwambia mwendeshaji wake wa gari: Ligeuze kwa mkono wako, unitoe hapa, wanapopigana, kwani nimeumia.[#2 Mambo 35:23.]

35Mapigano yakazidi siku hiyo; kwa hiyo mfalme alikuwa amesimama garini ng'ambo ya huku ya Washami, akafa jioni; nayo damu ya kidonda chake ilikuwa imemwagika ndani ya gari.

36Jua lilipokuchwa, mbiu ikapigwa makambini kwamba: kila mtu na arudi mjini kwake! Kila mtu na arudi katika nchi yake!

37Mfalme alipokwisha kufa, akapelekwa Samaria; ndiko, walikomzika mfalme wa Samaria.

38Walipolisafisha lile gari kwa maji penye ziwa la Samaria, mbwa wakailamba damu yake nao wanawake wagoni wakaoga papo hapo, kama Bwana alivyosema.[#1 Fal. 21:19; 2 Fal. 9:25.]

39Mambo mengine ya Ahabu nayo yote, aliyoyafanya, na habari za ile nyumba ya pembe za tembo, aliyoijenga, nazo za miji yote, aliyoijenga, hazikuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?

40Ahabu alipokwisha kulala na baba zake, mwanawe Ahazia akawa mfalme mahali pake.[#1 Fal. 22:52.]

Ufalme wa Wayuda: Mfalme Yosafati.

(41-51: 2 Mambo 20:31-21:1.)

41Yosafati, mwana wa Asa, akapata kuwa mfalme wa Wayuda katika mwaka wa 4 wa Ahabu, mfalme wa Waisiraeli.[#1 Fal. 15:24.]

42Yosafati alikuwa mwenye miaka 35 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 25; jina la mama yake ni Azuba, binti Silihi.

43Akaendelea kuzishika njia zote za baba yake Asa, hakuziacha kabisa, akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana.

44Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, watu wakaendelea bado kutoa huko ng'ombe za tambiko na kuvukiza kule vilimani.[#1 Fal. 15:14; 2 Fal. 12:3.]

45Yosafati akakaa na kupatana na mfalme wa Waisiraeli.

46Mambo mengine ya Yosafati na matendo yake yenye nguvu, aliyoyafanya alipopiga vita, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda?[#2 Mambo 17—20.]

47Nao wagoni wa patakatifu waliosalia katika siku za baba yake Asa akawatowesha kabisa katika hiyo nchi.[#1 Fal. 15:12.]

48Kule Edomu siku zile hakuwako mfalme mwenyewe ni mtawala nchi tu aliyeshika ufalme.

49Yosafati akajitengenezea merikebu za Tarsisi kwenda Ofiri kuchukua dhahabu, lakini hazikufika, kwani hizo merikebu za Tarsisi zilivunjika Esioni-Geberi.[#1 Fal. 9:28.]

50Siku zile Ahazia, mwana wa Ahabu, alimwambia Yosafati: Watumishi wangu, na waende pamoja na watumishi wako merikebuni. Lakini Yosafati akakataa.

51Yosafati akaja kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa baba yake Dawidi, naye mwanawe Yoramu akawa mfalme mahali pake.[#2 Fal. 8:16.]

Ufalme wa Waisiraeli: Mfalme Ahazia:

52Ahazia, mwana wa Ahabu, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli kule Samaria katika mwaka wa 17 wa Yosafati, mfalme wa Wayuda, akawa mfalme wa Waisiraeli miaka 2.[#1 Fal. 22:40.]

53Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, akaendelea kuishika njia ya baba yake na njia ya mama yake na njia ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Waisiraeli.[#1 Fal. 12:30.]

54Akamtumikia Baali na kumtambikia, akamchafukisha Bwana Mungu wa Isiraeli kwa kuyafanya yote, baba yake aliyoyafanya.[#1 Fal. 16:31-33.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania