The chat will start when you send the first message.
1Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma watumishi wake kwa Salomo, kwani alisikia, ya kuwa wamempaka mafuta, awe mfalme mahali pa baba yake, kwani Hiramu alikuwa akimpenda Dawidi siku zote.[#2 Sam. 5:11.]
2Salomo akatuma kwa Hiramu kumwambia:
3Wewe unajua, ya kuwa baba yangu Dawidi hakuweza kulijengea Jina la Bwana Mungu wake nyumba kwa ajili ya vita, adui zake walivyomletea toka pande zote, hata Bwana akawaweka chini ya nyayo za miguu yake.
4Sasa Bwana Mungu wangu amenipa kutulia pande zote, hakuna mpingani wala jambo baya.
5Kwa hiyo nimesema, nilijengee Jina la Bwana Mungu wangu nyumba, kama Bwana alivyomwambia baba yangu Dawidi kwamba: Mwanao, nitakayempa kukaa mahali pako katika kiti chako cha kifalme, ndiye atakayelijengea Jina langu nyumba.[#2 Sam. 7:13.]
6Sasa agiza, watu wanikatie miangati huko Libanoni! Watu wangu na wachanganyike na watu wako, nao mshahara wote wa watu wako nitakupa, kama utakavyosema, kwani mwenyewe unajua, ya kuwa kwetu hakuna ajuaye kuchonga miti kama watu wa Sidoni.
7Ikawa, Hiramu alipoyasikia haya maneno ya Salomo akafurahi sana, akasema: Bwana na atukuzwe leo hivi, kwani amempa Dawidi mwana mwenye werevu wa kweli wa kuwatawala wale watu wengi.[#1 Fal. 10:9.]
8Ndipo, Hiramu alipotuma kwa Salomo kumwambia: Nimeyasikia maneno yako, uliyotuma kuniambia. Mimi nitayafanya yote, uyatakayo, nikupatie miti ya miangati na miti ya mivinje.
9Watu wangu wataitelemsha toka Libanoni hata baharini; kisha mle baharini nitaifunga, ielee; ndivyo, nitakavyoifikisha mahali pale, utakaponiambia; hapo nitaifungua tena, wewe upate kuichukua. Nawe na uyafanye, niyatakayo, ukiwapa watu wa kwangu vyakula.
10Kisha Hiramu akampa Salomo miti ya miangati na miti ya mivinje, yote kama alivyoitaka.
11Naye Salomo akampa Hiramu kori 20000, ndio frasila 200000 za ngano kuwa posho za watu wa kwake na kori 20, ndio frasila 200 za mafuta mazuri mno; hivi ndivyo, Salomo alivyompa Hiramu mwaka kwa mwaka.
12Bwana akampa Salomo werevu wa kweli, kama alivyomwambia. Kwao Hiramu na Salomo yakawako matengemano, wakafanya agano hao wawili.[#1 Fal. 3:12; 4:29.]
13Kisha mfalme Salomo akawatoza Waisiraeli wote watu wa kazi za nguvu, nao hao watu wa kazi za nguvu wakawa watu 30000.
14Akatuma kila mwezi watu 10000 kwenda Libanoni, wapokeane hivyo: mwezi mmoja wakae Libanoni, kisha nyumbani kwao miezi miwili. Naye Adoniramu alikuwa mkuu wao hao watu wa kazi za nguvu.[#1 Fal. 4:6.]
15Salomo akawa nao wachukuzi wa mizigo 70000, tena wachonga mawe 80000 milimani.
16Tena Salomo akawa na wasimamizi 3300 waliowekwa naye kuwa wakuu wa wafanya kazi na kuwasimamia, wakifanya kazi.
17Mfalme akaagiza, wavunje mawe yaliyo makubwa na mazuri mno ya kuchonga ya kuwekea misingi ya nyumba.
18Waashi wa Salomo na waashi wa Hiramu na Wagebali wakayachonga. Ndivyo, walivyotengeneza miti na mawe, wapate kuijenga hiyo nyumba.[#Yos. 13:5; Ez. 27:9.]