1 Wafalme 8

1 Wafalme 8

Mweuo wa Nyumba ya Mungu.

(1-11: 2 Mambo 5.)

1Kisha Salomo akawakusanya wazee wa Waisiraeli nao wote waliokuwa vichwa vya mashina na wakuu wa milango ya wana wa Isiraeli mle Yerusalemu kwake yeye mfalme Salomo kwenda kulitoa Sanduku la Agano la Bwana katika mji wa Dawidi ulioitwa Sioni.

2Ndipo, watu wote wa Isiraeli walipokusanyika kwa mfalme Salomo kufanya sikukuu katika mwezi wa Etanimu, ndio mwezi wa saba.

3Wazee wote wa Isiraeli walipokwisha fika, watambikaji wakalichukua hilo Sanduku.

4Wakalipeleka Sanduku la Bwana pamoja na Hema la Mkutano na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa Hemani; hivi watambikaji na Walawi wakavipandisha.

5Naye mfalme Salomo pamoja na mkutano wote wa Waisiraeli wote waliokusanyika kwake kuwa naye mbele ya hilo Sanduku wakatoa mbuzi na kondoo na ng'ombe kuwa ng'ombe za tambiko, nao hawakuhesabika, wala hawakuwangika kwa kuwa wengi mno.[#2 Sam. 6:13.]

6Watambikaji wakaliingiza Sanduku la Agano la Bwana mahali pake katika chumba cha ndani kiitwacho Patakatifu Penyewe, wakaliweka chini ya mabawa ya Makerubi.

7Kwani yale Makerubi yalikuwa yameyakunjua mabawa juu ya mahali pale, Sanduku lilipowekwa; ndivyo, Makerubi yalivyolifunika juu hilo Sanduku nayo mipiko yake.

8Kwa urefu wa mipiko pembe zao hii mipiko zikaonekana mle Patakatifu kuelekea mle chumbani mwa ndani, lakini nje hazikuonekana; nayo imo humo hata siku hii ya leo.[#2 Mose 25:13-15; 2 Mambo 5:9.]

9Mle Sandukuni hamkuwamo na kitu, ni zile mbao mbili za mawe tu, Mose alizoziweka humo huko Horebu, Bwana alipofanya Agano na wana wa Isiraeli, walipotoka katika nchi ya Misri.[#Ebr. 9:4.]

10Ikawa, watambikaji walipotoka Patakatifu, ndipo, wingu lilipoijaza Nyumba ya Bwana.

11Nao watambikaji hawakuweza kusimama humo na kuzifanya kazi za utumishi wao kwa ajili ya hilo wingu, kwani utukufu wa Bwana uliijaza Nyumba ya Bwana.[#2 Mose 40:34-35.]

Kuomba kwake Salomo.

(12-53: 2 Mambo 6:1-40.)

12Ndipo, Salomo aliposema: Bwana alisema, ya kuwa hukaa mawinguni mwenye weusi.[#2 Mose 20:21; 5 Mose 4:11.]

13Nami nimekujengea Nyumba, iwe Kao lako la kukaa humu kale na kale.

14Kisha mfalme akaugeuza uso wake, akaubariki mkutano wote wa Waisiraeli, nao wote wa mkutano wa Waisiraeli walikuwa wamesimama.

15Akasema: Atukuzwe Bwana Mungu wa Isiraeli! Aliyomwambia baba yangu Dawidi kwa kinywa chake, ameyatimiza kwa mkono wake, ya kwamba:

16Tangu siku ile, nilipoutoa ukoo wangu wa Waisiraeli huko Misri, sikuchagua mji katika mashina yote ya Isiraeli, ndimo wanijengee Nyumba, Jina langu likae humo. Lakini nilimchagua Dawidi wa kuutawala ukoo wangu wa Waisiraeli.

17Baba yangu Dawidi akawaza moyoni kulijengea Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli nyumba.[#2 Sam. 7.]

18Lakini Bwana akamwambia baba yangu Dawidi: Ukiwaza moyoni mwako kulijengea Jina langu nyumba, umefanya vema kuyawaza hayo moyoni mwako.

19Lakini wewe hutaijenga hiyo nyumba, ila mwanao atakeyetoka viunoni mwako ndiye atakayelijengea Jina langu nyumba.

20Bwana akalitimiza hilo neno, alilolisema, nami nikaondokea mahali pa baba yangu Dawidi, nikakaa katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli, kama Bwana alivyosema, nikalijengea Jina la Bwana Mungu wa Isiraeli Nyumba hii.

21Nikapata humu mahali pa kuliwekea Sanduku, Agano la Bwana lilimo, alilolifanya na baba zetu alipowatoa katika nchi ya Misri.

22Kisha Salomo akaja kusimama mbele ya meza ya kumtambikia Bwana machoni pao mkutano wote wa Waisiraeli, akaikunjua mikono yake na kuielekeza mbinguni,

23akasema: Bwana Mungu wa Isiraeli, hakuna Mungu afananaye na wewe, wala mbinguni juu wala katika nchi huku chini. Unawashikia watumishi wako agano lako na upole wako, wakiendelea mbele yako kwa mioyo yao yote.

24Umemshikia mtumishi wako, baba yangu Dawidi, uliyomwambia; uliyoyasema kwa kinywa chako, umeyatimiza kwa mkono wako, kama inavyoonekana siku hii ya leo.

25Na sasa Bwana Mungu wa Isiraeli, mshikie mtumishi wako, baba yangu Dawidi, uliyomwambia kwamba: Kwako hakutakoseka mtu atakayekaa machoni pangu katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli, wanao wakiziangalia tu njia zao, waendelee kuwa machoni pangu, kama wewe ulivyoendelea kuwa machoni pangu.

26Sasa Mungu wa Isiraeli, hilo neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, baba yangu Dawidi, na lishupazwe!

27Inakuwaje? Mungu anakaa kweli huku nchini? Tazama! Mbingu nazo mbingu zilizoko juu ya mbingu hazikuenei, sembuse Nyumba hii, niliyoijenga![#Yes. 66:1; Tume. 7:49; 17:24.]

28Yageukie maombo ya mtumishi wako na malalamiko yake, Bwana Mungu wangu, uvisikilize vilio na maombo, mtumishi wako anayokuomba usoni pako leo hivi!

29Uwe macho kuiangalia Nyumba hii usiku na mchana, ipate kuwa mahali pale, ulipopasema: Mahali hapa ndipo, Jina langu litakapokuwa! Kwa hiyo yasikie maombo, mtumishi wako atakayokuomba mahali hapa![#Zak. 12:4; 2 Mose 20:24; 5 Mose 12:5,11.]

30Yasikie nayo malalamiko ya mtumishi wako nayo yao walio ukoo wako wa Waisiraeli, watakayokuomba mahali hapa! Wewe wasikie huko juu mbinguni, unakokaa! Tena utakapowasikia uwaondolee makosa!

31Mtu akikosana na mwenziwe, akachukuliwa, aape, basi, wakimwapisha hivyo, naye akija kuapia mbele ya meza ya kutambikia katika Nyumba hii,

32wewe umsikie huko mbinguni, ulitengeneze jambo hilo na kuwaamua watumishi wako, ukimlipisha yule aliyekosa na kumtwika kichwani pake matendo yake, tena yule asiyekosa ukimtokeza kuwa pasipo kosa, ukimpa yaliyo haki yake.

33Itakuwa, walio ukoo wako wa Waisiraeli wakimbizwe na adui, kwa kuwa wamekukosea; kisha watakapokurudia na kuliungama Jina lako, wakuombe na kukulalamikia humu Nyumbani,

34wewe na uwasikie huko mbinguni, uwaondolee walio ukoo wako wa Waisiraeli makosa yao! Kisha warudishe katika nchi hii, uliyowapa baba zao!

35Itakuwa, mbingu zizibane, mvua isinye, kwa kuwa wamekukosea; kisha watakapoombea mahali hapa na kuliungama Jina lako na kuyaacha makosa yao, kwa kuwa umewatea,[#1 Fal. 17:1.]

36wewe na uwasikie huko mbinguni, uwaondolee makosa yao walio watumishi wako nayo yao walio ukoo wako wa Waisiraeli! Kisha wafundishe njia iliyo njema, waishike, upate kuinyeshea nchi yako mvua tena, kwa kuwa umeipa walio ukoo wako, iwe fungu lao.

37Itakuwa, njaa iingie katika nchi hii au magonjwa mabaya, itakuwa, jua kali linyaushe mashamba yote, itakuwa, nzige na funutu wamalize vilaji vyote, itakuwa, adui zao wawasonge watu kwao malangoni mwao, itakuwa, mapigo menginemengine na magonjwa yo yote yawapate,

38basi, lisikie kila ombo na kila lalamiko litakalokutokea, kama ni la mtu mmoja awaye yote, au lao wote walio ukoo wako wa Waisiraeli, kwa kuwa kila mtu anayajua mapigo ya moyo wake. Hapo watakapokuja kuikunjua mikono yau humu Nyumbani,

39wewe na uwasikie huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa, uwaondolee makosa ukifanya yapasayo na kumrudishia kila mtu, kama njia zake zilivyo, kwa hivyo, unavyoujua moyo wake! Kwani wewe peke yako unaijua mioyo ya wana wa watu wote,[#Sh. 7:10; 139:1.]

40kusudi wakuogope siku zote, watakazokuwapo katika nchi hii, uliyowapa baba zetu.

41Tena itakuwa, hata mgeni asiye wa ukoo wako wa Waisiraeli aje huku na kutoka katika nchi ya mbali kwa ajili ya Jina lako,[#4 Mose 15:14-16.]

42kwani watapata habari za Jina lako lililo kuu na za kiganja chako kilicho na nguvu na za mkono wako uliokunjuka; basi, hapo atakapokuja, aombee humu Nyumbani,

43wewe na umsikie huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa, uyafanye yote, yule mgeni atakayokuomba na kukulilia, makabila yote ya nchi yalijue Jina lako, wakuogope kama wao walio ukoo wako wa Waisiraeli, tena wajue, ya kuwa Nyumba hii, niliyoijenga, imeitwa kwa Jina lako.

44Itakuwa, walio ukoo wako wakitoka kupigana na adui zao na kuishika njia, utakayowatuma, wakuombe, Bwana, njiani na kuuelekea mji huu, uliouchagua, hata Nyumba hii, niliyolijengea Jina lako,

45basi, hapo na uyasikie huko mbinguni maombo yao na malalamiko yao, uwatengenezee shauri lao.

46Tena itakuwa, wakukosee, kwani hakuna mtu asiyekosa, nawe utawakasirikia, uwatie mikononi mwao adui, wawateke na kuwahamisha wakiwapeleka katika nchi ya kwao ya mbali au ya karibu;[#Rom. 3:23.]

47lakini hapo, watakapojirudia wenyewe mioyoni mwao katika nchi hiyo, walikohamishiwa, basi, hapo watakapokulalamikia tena katika nchi ya uhamisho wao na kusema: Tumekosa, tumekora manza, tumefanya maovu,[#Dan. 9:5.]

48watakapokurudia hivyo kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote katika nchi ya adui zao, walikowahamisha nako, watakapokuomba na kuielekea nchi yao, uliyowapa baba zao, nao mji, uliouchagua, nayo Nyumba hii, niliyolijengea Jina lako,

49basi, wewe huko mbinguni kuliko na Kao lako la kukaa na uyasikie maombo yao na malalamiko yao, uwatengenezee shauri lao

50na kuwaondolea walio ukoo wako makosa yao, waliyokukosea, hata mapotovu yao yote, waliyokutendea, kisha uwapatie huruma machoni pao waliowahamisha, wawahurumie!

51Kwani ndio watu wa ukoo wako na fungu lako, uliowatoa huko Misri katika tanuru ya kuyeyushia vyuma.

52Uwe macho, upate kuyasikiliza malalamiko ya mtumishi wako na malalamiko yao walio ukoo wako wa Waisiraeli, uwasikie kila, watakapokulilia!

53Kwani wewe mwenyewe umewatenga na kuwatoa katika makabila yote ya nchini, wawe fungu lako wewe, kama ulivyosema kinywani mwa mtumishi wako Mose, ulipowatoa baba zetu huko Misri, wewe Bwana Mungu.

54Salomo alipokwisha kumwomba Bwana maombo haya yote na kumlalamikia hivyo, akainuka hapo mbele ya meza ya kumtambikia Bwana, alipokuwa amepiga magoti, mikono yake ikiwa imekunjuliwa na kuelekea mbinguni.

55Akasimama, akaubariki mkutano wote wa Waisiraeli na kupaza sauti sana akisema:[#2 Sam. 6:18.]

56Bwana na atukuzwe, kwa kuwa amewapatia walio ukoo wake wa Waisiraeli kutulia! Yote yakawa, kama alivyosema. Katika maneno yake yote mazuri, aliyoyasema kinywani mwa mtumishi wake Mose, hakutupotelea hata moja.[#Yos. 21:45.]

57Bwana Mungu wetu awe nasi, kama alivyokuwa na baba zetu, asituache, wala asitutupe,

58apate kuielekeza mioyo yetu na kwake, tuendelee katika njia zake zote na kuyaangalia maagizo yake na maongozi yake na maamuzi yake, aliyowaagiza baba zetu.

59Hayo maneno yangu ya kumlalamikia Bwana na yamkalie Bwana Mungu wetu karibu mchana na usiku, amtengenezee mtumishi wake mashauri yake nao walio ukoo wake wa Waisiraeli mashauri yao, kama itakavyowapasa siku kwa siku,

60kusudi makabila yote ya nchi yapate kujua, ya kuwa Bwana ndiye Mungu, hakuna mwingine tena.

61Nayo mioyo yenu yote mizima iwe upande wa Bwana Mungu wetu, mwendelee kuyafuata maongozi yake na kuyaangalia maagizo yake kama siku hii ya leo!

(62-66: 2 Mambo 7:4-10.)

62Kisha mfalme nao Waisiraeli wote pamoja naye wakamtolea Bwana ng'ombe za tambiko.

63Salomo akatoa ng'ombe 22000 na mbuzi na kondoo 120000 kuwa ng'ombe za tambiko za kumshukuru Bwana. Ndivyo, mfalme na wana wa Isiraeli wote walivyoieua Nyumba ya Bwana.

64Siku hiyo mfalme alikitakasa kipande cha kati cha ua uliokuwa mbele ya Nyumba ya Bwana, kwani ndiko, alikotolea ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na vilaji vya tambiko na mafuta ya ng'ombe za tambiko za shukrani, kwani ile meza ya shaba ya kutambikia iliyokuwako kule mbele ya Bwana ilikuwa ndogo, haikueneza kabisa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na vilaji vya tambiko na mafuta ya ng'ombe za tambiko za shukrani.

65Ndivyo, Salomo alivyofanya sikukuu wakati huo, yeye pamoja nao Waisiraeli wote, wakawa mkutano mkubwa wa watu waliotoka Hamati mpaka kwenye mto wa Misri; wakafanya sikukuu mbele ya Bwana siku saba, na tena siku saba, pamoja zilikuwa siku kumi na nne.

66Siku ya nane akawapa watu ruhusa, wakaagana na mfalme na kumbariki, wakaenda mahemani kwao wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote, Bwana alimfanyizia mtumishi wake Dawidi nao walio ukoo wake wa Waisiraeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania