The chat will start when you send the first message.
1Salomo alipomaliza kuijenga Nyumba ya Bwana na nyumba ya mfalme na kuyafanya yote, Salomo aliyotaka kuyafanya kwa kupendezwa nayo,
2ndipo, Bwana alipomtokea Salomo mara ya pili, kama alivyomtokea kule Gibeoni.[#1 Fal. 3:5.]
3Bwana akamwambia: Nimeyasikia maombo yako na malalamiko yako, uliyonilalamikia; nimeitakasa Nyumba hii, uliyoijenga, nilikalishe Jina langu humu kale na kale, nayo macho yangu pamoja na moyo wangu yatakuwa humu siku zote.[#1 Fal. 8:29.]
4Wewe nawe ukiendelea kuwa machoni pangu, kama baba yako Dawidi alivyoendelea kwa moyo ulionyoka wote, uyafanye yote, niliyokuagiza, ukiyaangalia maongozi yangu na maamuzi yangu,
5ndipo, nitakapokisimamisha kiti cha kifalme cha ufalme wako wa kuwatawala Waisiraeli, kisimame kale na kale, kama nilivyomwambia baba yako Dawidi kwamba: Kwako hakutakoseka mtu atakayekaa katika kiti cha kifalme cha Waisiraeli.[#2 Sam. 7:12.]
6Lakini mtakaporudi nyuma ninyi au wana wenu, msinifuate, msiyaangalie maagizo yangu na maongozi yangu, niliyoyatoa machoni penu, mkaja kutumikia miungu mingine na kuiangukia,
7ndipo, nitakapowang'oa Waisiraeli katika nchi hii, niliyowapa, nayo Nyumba hii, niliyoitakasa, iwe Kao la Jina langu, nitaiacha, macho yangu yasiione tena, nao Waisiraeli watakuwa fumbo na simango kwa makabila yote.[#5 Mose 4:26; 8:19-20; Mat. 23:38.]
8Nayo Nyumba hii iliyokuwa imetukuka kabisa, basi, kila atakayeipita ataistukia na kuizomea, waulize: Kwa sababu gani Bwana ameifanyizia hivi nchi hii na Nyumba hii?
9Ndipo, watakapojibu: Kwa kuwa walimwacha Bwana Mungu wao aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine wakaiangukia na kuitumikia; hii ndiyo sababu, Bwana akiwaletea haya mabaya yote.
10Ile miaka ishirini, ambayo Salomo alizijenga zile nyumba mbili, Nyumba ya Bwana na nyumba ya mfalme, ilipokwisha kupita,[#1 Fal. 6:38; 7:1.]
11ndipo, mfalme Salomo alipompa Hiramu, mfalme wa Tiro, miji ishirini katika nchi ya Galili, kwa kuwa alimpatia mfalme Salomo miti ya miangati na miti ya mivinje na dhahabu, yote pia, kama alivyoitaka.
12Hiramu alipotoka Tiro kuitazama hiyo miji, Salomo aliyompa, haikumpendeza,
13akasema: Ni miji gani hii, uliyonipa, ndugu yangu? Wakaiita nchi ya Kabuli hata siku hii ya leo.
14Naye Hiramu alikuwa amempelekea mfalme vipande 120 vya dhahabu, ndio frasila 360.
15Kazi za watu, mfalme Salomo aliowatoa kufanya kazi za nguvu, ni hizi: waliijenga Nyumba ya Bwana na nyumba yake na Milo na boma la kuuzunguka Yerusalemu, tena Hasori na Megido na Gezeri.
16Kwani Farao, mfalme wa Misri, alikuwa amepanda, akauteka Gezeri, akauteketeza kwa moto, nao Wakanaani waliokaa humo, akawaua, kisha akampa mwanawe aliyekuwa mkewe Salomo, uwe tunzo lake.[#Yos. 16:10; 1 Fal. 3:1.]
17Lakini Salomo akajenga Gezeri tena, hata Beti-Horoni wa chini,
18na Balati na Tamari ulioko nyikani katika nchi ile;
19hata miji yote yenye vilimbiko, Salomo aliyokuwa nayo, nayo miji ya magari na miji ya farasi na majengo yote, Salomo aliyotaka kuyajenga kwa mapenzi yake mle Yerusalemu nake huko Libanoni na katika nchi yo yote ya ufalme wake.[#1 Fal. 10:26.]
20Watu, aliowatumia, ndio wote waliosalia wa Waamori na wa Wahiti na wa Waperizi na wa Wahiwi na wa Wayebusi wasiokuwa wa wana wa Isiraeli;
21wana wao wale waliosalia na kuachwa na wenzao katika nchi hii, kwa kuwa wana wa Isiraeli hawakuweza kuwamaliza na kuwaua kwa kuwatia mwiko wa kuwapo, basi, hawa Salomo akawatoa, akawafanyisha kazi za nguvu za kitumwa hata siku hii ya leo.[#Yos. 16:10.]
22Lakini wana wa Isiraeli Salomo hakuwataka kuwa watumwa, kwani hawa walikuwa wapiga vita na watumishi wake na wakuu wake na wakuu wa thelathini na wakuu wa magari yake na wapanda farasi wake.
23Nao wakuu wa mfalme Salomo waliowekwa kusimamia kazi walikuwa 550; ndio waliowatawala watu waliofanya kazi.
24Binti Farao alipokwisha kutoka katika mji wa Dawidi na kuingia katika nyumba yake, aliyomjengea, ndipo, alipolijenga lile boma lililoitwa Milo.
25Salomo akatoa kila mwaka mara tatu ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani hapo pa kutambikia, alipomjengea Bwana; kila mara, alipozitoa, akavukiza penye meza iliyoko mbele ya Bwana. Alifanya hivyo alipokwisha kuimaliza hiyo Nyumba.[#2 Mambo 8:13.]
26Kisha mfalme Salomo akatengeneza nazo merikebu za mizigo kule Esioni-Geberi karibu ya Eloti huko pwani kwenye Bahari Nyekundu iliyoko katika nchi ya Edomu.
27Hiramu akatuma watumishi wake wa kutumia merikebuni walio mafundi wa kazi za merikebuni, walioijua nayo bahari, wafanye kazi pamoja na watumishi wa Salomo.[#1 Fal. 10:11.]
28Wakaenda Ofiri, wakachukua huko vipande vya dhahabu 420, ndio frasila 1260, wakampelekea mfalme Salomo.[#1 Mose 10:29.]