1 Petero 3

1 Petero 3

Wake wawatii waume wao!

1Vivyo hivyo nanyi wake sharti mwatii waume wenu! Maana kama wako wasiolitii Neno, watatekwa kwa mwenendo wa wake zao pasipo kuambiwa maneno,[#Ef. 5:22.]

2wakiona kwa macho yao, mnavyoendelea king'avu kwa kuwaogopa.

3Nayo marembo yao yasiwe ya miili, kama misuko ya nywele na mapambo ya dhahabu na mavazi ya nguo nzuri![#Yes. 3:18-24; 1 Tim. 2:9.]

4Ila uzuri wao uwe wa mioyoni unaojificha mle ndani pasipo kuangamia, maana ni wa mtu mwenye roho ya upole na ya utulivu, naye Mungu huuona kuwa mali kweli.

5Kwani hata kale wanawake watakatifu waliomngojea Mungu walijipamba hivyo wakiwatii waume wao,

6kama Sara alivyomtii Aburahamu akimwita bwana. Nanyi wanawake, mnakuwa watoto wake mkitenda mema pasipo kuogopa vituko vyo vyote.[#1 Mose 18:12.]

Waume wawape wake zao macheo!

7Vilevile nanyi waume, mwendeleane na wake zenu na kuwatambua kuwa viumbe vinyonge kuliko ninyi! Tena waheshimuni! Maana nao watagawiwa urithi wao wa uzimani pamoja nanyi; fanyeni hivyo, msizuiliwe kuomba![#Ef. 5:25.]

8*Kisha nyote mioyo yenu sharti iwe mmoja, mpate kuvumiliana na kupendana kama ndugu walio wenye uororo na unyenyekevu!

9Msimlipe mtu uovu kwa uovu, wala matukano kwa matukano! Ila wafanyao hivyo mwaombee mema! Kwani hayo ndiyo, mliyoitiwa, mwirithi mbaraka.[#1 Tes. 5:15.]

10Maana

atakayependa kuwa uzimani naye atakaye kuona siku njema

aulindie ulimi wake, usiseme mabaya,

nayo midomo yake, isiseme madanganyifu!

11Yaliyo mabaya ayaepuke, afanye mema,

atafute penye utengemano, apakimbilie!

12Maana macho ya Bwana huwatazama walio waongofu,

masikio yake huyasikia maombo yao.

Lakini uso wa Bwana huwapingia wafanyao mabaya.

Kristo alivyokwenda kuzimuni.

13Yuko nani atakayewaponza ninyi, mkijikaza kufanya mema?

14Lakini ijapo mteswe kwa ajili ya wongofu mtakuwa wenye shangwe. Lakini msiyaogope maogopesho yao, wala msiyahangaikie![#1 Petr. 2:20; Yes. 8:12; Mat. 5:10.]

15Ila mtakaseni Bwana Kristo mioyoni mwenu!* Tena po pote mwe tayari kumjibu kila mtu anayewauliza kwa ajili ya kingojeo chenu kilichomo mwenu! Lakini wajibuni kwa upole na kuwaogopa![#Yes. 8:13.]

16Mioyo yenu sharti ijulike kuwa miema! Hivyo wenye kuwasengenya kwamba: M waovu, wataingiwa na soni kwa ajili ya mwenendo wenu, ukiwa mzuri kwa nguvu ya Kristo.

17Kwani kuteswa kwa ajili ya kutenda mema, Mungu akivitaka, ni vizuri kuliko kuteswa kwa ajili ya kutenda maovu.[#1 Petr. 2:20; 3:14.]

18Kwani naye Kristo alikufa mara moja kwa ajili ya makosa yetu; yeye aliyekuwa mwongofu alikufa kwa ajili yetu tulio wapotovu, atupeleke kwake Mungu. Aliuawa kimwili, lakini alirudishwa uzimani Kiroho.[#1 Petr. 2:21-24; Ef. 2:18.]

19Hapo aliwaendea wazimu nao mle, waliomo kifungoni, akawapigia mbiu[#1 Petr. 4:6.]

20wale waliokataa kutii kale, Mungu alipowangoja na kuwavumilia siku zile za Noa, kile chombo kikubwa kilipotengenezwa; lakini miongoni mwao wakaokoka wachache, watu wanane tu katika kondo ile ya maji.[#1 Mose 7:7,17.]

21Maji hayo ni mfano wa maji ya ubatizo yanayowaokoa sasa hata ninyi; kweli hayaondoi machafu ya miili, ila ya mioyo, ipate kuwa miema na kupatana naye Mungu kwa nguvu ya ufufuko wake Yesu Kristo.[#Ef. 5:26; Ebr. 10:22.]

22Yeye yuko kuumeni kwa Mungu, maana amekwenda mbinguni, atiiwe nao malaika na wenye nguvu na wenye uwezo.[#Ef. 1:20-21.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania