The chat will start when you send the first message.
1Nahasi wa Waamoni akapanda, akapiga makambi huko Yabesi katika nchi ya Gileadi. Ndipo, watu wote wa Yabesi walipomwambia Nahasi: Fanya agano nasi, tukutumikie![#1 Sam. 31:11.]
2Mwamoni Nahasi akawaambia: Basi, nitapatana nanyi hivyo: nitawachoma ninyi kila mtu jicho lake la kuume, niwatweze Waisiraeli wote.[#Yer. 39:7.]
3Wazee wa Yabesi wakamwambia: Tupe siku saba, tutume wajumbe kwenda katika mipaka yote ya Waisiraeli! Asipopatikana mwokozi wetu, tutakutokea.
4Wajumbe walipofika Gibea kwa Sauli na kuyasema maneno hayo masikioni pa watu, watu wote wakalia na kupaza sauti zao.
5Naye Sauli alikuwa anarudi malishoni akiwafuata ng'ombe; hapo Sauli akauliza: Watu wanalilia nini? Wakamsimulia habari, watu wa Yabesi walizozileta.
6Ndipo, roho ya Mungu ilipomjia Sauli, alipozisikia habari hizo, makali yake yakawaka moto.[#Amu. 14:6.]
7Akakamata ng'ombe wawili, akawakatakata, akawatuma wale wajumbe kwenda katika nchi zote za Waisiraeli na kuwapelekea watu vipande vya nyama kwamba: Kila mtu asiyetoka kumfuata Sauli na Samweli ng'ombe wake watafanyiziwa hivyo. Ndipo, watu walipoguiwa na kituko cha Bwana, wakatoka kama mtu mmoja.[#Amu. 19:29.]
8Alipowakagua huko Bezeki, wana wa Isiraeli walikuwa 300000, nao watu wa Yuda 30000.
9Wakawaambia wale wajumbe waliokuja: Hivi ndivyo, mtakavyowaambia watu wa Yabesi katika nchi ya Gileadi: Kesho, jua likianza kuwa kali, mtaona wokovu. Hao wajumbe waliporudi na kuwapasha habari hii, watu wa Yabesi wakafurahi.
10Nao watu wa Yabesi wakawaambia wale: Kesho tutawatokea, mtufanyizie yote yaliyo mema machoni penu.
11Kesho yake Sauli akawagawanya watu wake kuwa vikosi vitatu, wakaingia katikati ya makambi penye zamu ya kungoja, kuche, wakawapiga Waamoni, hata jua lilipokuwa kali mchana huo. Nao waliosalia wakatawanyika, wasisalie kwao wawili tu waliokuwa pamoja.
12Ndipo, watu walipomwambia Samweli: Wako wapi waliosema: Huyu Sauli awe mfalme wetu? Watoeni watu hawa, tuwaue![#1 Sam. 10:27.]
13Lakini Sauli akasema: Asiuawe mtu wa kwetu siku hii ya leo! Kwani leo Bwana amewapatia Waisiraeli wokovu.[#1 Sam. 14:45.]
14Samweli akawaambia watu: Njoni, twende Gilgali, tuurudishie ufalme upya![#1 Sam. 10:8.]
15Watu wote wakaja Gilgali, kisha wakamweka Sauli machoni pake Bwana huko Gilgali kuwa mfalme wao wakachinja huko machoni pake Bwana ng'ombe za tambiko za shukrani, naye Sauli akachangamka sanasana pamoja na Waisiraeli wote.