1 Samweli 14

1 Samweli 14

Tendo kuu la Yonatani la kuwashinda Wafilisti.

1Siku moja Yonatani, mwanawe Sauli, akamwambia kijana aliyemchukulia mata yake: Njoo, twende, tuwashambulie wale Wafilisti wanaongoja zamu hapo ng'ambo! Lakini baba yake hakumwambia.

2Naye Sauli alikuwa akikaa kwenye mpaka wa Gibea chini ya mkomamanga ulioko Migroni, nao watu waliokuwa naye walikuwa kama 600 tu.

3Naye Ahia, mwana wa Ahitubu, ndugu ya Ikabodi, mwana wa Pinehasi, mwana wa Eli aliyekuwa mtambikaji wa Bwana huko Silo, ndiye aliyevaa kisibau cha mtambikaji. Hata watu hawakujua, ya kuwa Yonatani amekwenda zake.[#1 Sam. 4:19,21.]

4Napo magemani, Yonatani alipotafua njia ya kupitita, afike kwa Wafilisti waliongoja zamu hapo, palikuwa na jino la mwamba upande wa huku na jino jingie la mwamba upande wa huko, jina lake moja ni Bosesi, jina lake la pili Sene.

5Genge moja likasimama sawa upande wa kaskazini kuelekea Mikimasi, la pili upande wa kusini kuelekea Geba.

6Yonatani akamwambia kijana aliyemchukulia mata: Haya! Twende, tuwavumbukie hao wamizimu wasiotahiriwa wanaongoja zamu! Labda Bwana atatupigania, kwani Bwana hashindwi na kuokoa, ikiwa anatumia wengi au wachache.[#Amu. 7:7; 2 Mambo 14:11.]

7Mchukua mata yake akamwambia: Yafanye yote yaliyomo moyoni mwako! Jielekeze kwenda kwao! Tazama, niko pamoja na wewe po pote, moyo wako unapotaka.

8Yonatani akasema: Tazama! Tukipita kwenda kwao hao watu, tutaonwa nao.

9Itakapokuwa, watuambie: Simameni, mpaka tuwafikie karibu! tutasimama hapo chini, tusiwapandie;

10lakini itakapokuwa, watuambie: Tupandieni! basi, tutapanda, kwani Bwana amewatia mikononi mwetu. Hiki kitakuwa kielekezo chetu.

11Walipowaonekea Wafilisti waliongoja zamu, Wafilisti wakasema: Tazameni! Waebureo wametoka mashimoni, walimokuwa wamejificha.

12Wale watu wa zamu wakaanza kusema naye Yonatani na mchukua mata yake wakiwaambia: Tupandieni, tuwajulishe neno! Ndipo, Yonatani alipomwambia mchukua mata yake: Panda nyuma yangu! Kwani Bwana amewatia mikononi mwa Waisiraeli.

13Yonatani akapanda na kutumia mikono na miguu yake, naye mchukua mata yake nyuma yake. Kisha wakaangushwa na Yonatani, naye mchukua mata yake akamaliza kuwaua nyuma yake.[#3 Mose 26:7-8.]

14Hivyo hili pigo la kwanza, alilolipiga Yonatani na mchukua mata yake, liliua watu kama 20, napo mahali pale palikuwa kama nusu tu ya shamba linalolimwa na ng'ombe wawili siku moja.

15Ndipo, watu wote walipostushwa waliokuwako makambini na mashambani, waliongoja zamu nao waliotembea kuangamiza tu, hao nao wakastushwa kweli, kwani hata nchi ilikuwa imetetemeka, wakawa wakimstukia Mungu.

16Nao walinzi wa Sauli waliokuwa huko Gibea wa Benyamini walikuwa wakichungulia, mara wakaona, huo mtutumo wa watu ulivyotoweka, wakienda huko na huko.

17Nipo, Sauli alipowaambia watu waliokuwa naye: Wakagueni watu, mwone, kama ni wa nani walioondoka kwetu. Walipowakagua watu wakaona, Yonatani na mchukua mata yake hawako.

18Kisha Sauli akamwambia Ahia: Lilete Sanduku la Mungu! Kwani Sanduku la Mungu lilikuwako siku hiyo kwao wana wa Isiraeli.[#1 Sam. 4:3.]

19Ikawa, Sauli aliposema na mtambikaji, makelele yaliyoko makambini kwa Wafilisti yakaendelea kuzidi sana; ndipo, Sauli alipomwamba mtambikaji: Urudishe mkono wako!

20Sauli na watu waliokuwa naye wakaitana; walipofika penye mapigano wakaona, ya kuwa wanapigana wao kwa wao kwa panga, kila mtu na mwenziwe, kukawa hangaiko kubwa sana.[#Amu. 7:22; 2 Mambo 20:23.]

21Kwani kwao Wafilisti kulikuwako Waebureo waliotekwa kale, nao walikuwa wamepanda nao kukaa makambini; nao waligeuka, wawe upande wa Waisiraeli pamoja na Sauli na Yonatani.

22Hata Waisiraeli wote waliojificha mlimani kwa Efuraimu waliposikia, ya kuwa Wafilisti wamekimbizwa, wakaja kuandamana nao wenye kuwafukuza Wafilisti vitani.

23Hivyo Bwana akawaokoa Waisiraeli siku hiyo; nayo mapigano yakaendelea kufika hata Beti-Aweni.

Sauli anazidi kuwahimiza Waisiraeli kupita kiasi.

24Siku hiyo watu wa Waisiraeli wakachoka sana, lakini Sauli akawaapisha kwamba: Na aapizwe kila mtu atakayekula chakula mpaka jioni, nipate kuwalipiza adui zangu! Kwa hiyo hakuna mtu aliyeonja chakula

25Watu wote wa huko walipoingia mwituni, basi, kukawa na asali huko porini.

26Watu wote walipoingia mle mwituni, wakaona, asali inavyomwagika, lakini hakuwako mtu aliyeukunjua mkono wake kuipeleka kinywani mwake, kwani watu walikiogopa hicho kiapo.

27Lakini Yonatani hakusikia, baba yake alipowaapisha watu, kwa hiyo akaipeleka ncha ya fimbo yake, aliyoishika mkononi, akaichovya katika ute wa masega ya asali, akaurudisha mkono wake kinywani mwake; ndipo, macho yake yalipong'aa.

28Mtu mmoja akaanza kusema na kumwambia: Baba yako amewaapisha watu kwamba: Na aapizwe kila mtu atakayekula chakula leo! Watu walipotaka kuzimia,

29Yonatani akasema: Baba yangu anaiponza nchi hii. Nitazameni, macho yangu yanavyong'aa kwa kuwa nimeionja asali hii kidogo tu!

30Kama watu wangalikula leo nyara za adui zao, walizoziona, wangezidisha kazi, lakini sasa mapigo yao ya kuwapiga Wafilisti si mengi sana.

31Siku hiyo wakawapiga Wafilisti toka Mikimasi hata Ayaloni, kisha wakawa wenye kuzimia kabisa.

32Ndipo, watu walipozirukia hizo nyara, wakachukua mbuzi na kondoo na ng'ombe na ndama, wakawachinja papo hapo, nao watu wakawala pamoja na damu.[#3 Mose 3:17.]

33Wengine walipompasha Sauli habari kwamba: Watu wanamkosea Bwana wakila nazo damu, akasema: Mwavunja maagano! Sasa hivi fingirisheni jiwe kubwa, lije huku kwangu!

34Kisha Sauli akaagiza: Tawanyikeni katika watu na kuwaambia, kila mtu alete ng'ombe wake na mbuzi au kondoo wake huku kwangu, mwachinje hapa! Kisha mtawala pasipo kumkosea Bwana kwa kula damu. Ndipo, watu wote walipopeleka usiku huo kwa mikono yao kila mtu ng'ombe wake, wakawachinja hapo.

35Naye Sauli akajenga pa kumtambikia Bwana; hii ndio mara ya kwanza akimjengea Bwana pa kumtambikia.

36Sauli akasema: Na tutelemke kuwafukuza Wafilisti na usiku, tupate kuteka mateka kwao, mpaka kuche, tusisaze kwao mtu hata mmoja! Watu wakasema: Yote yaliyo mema machoni pako yafanye! Lakini mtambikaji akasema: Kwanza tumkaribie Mungu hapa!

37Ndipo, Sauli alipomwuliza Mungu: Nitelemke kuwafukuza Wafilisti? Hukuwatia mikononi mwa Waisiraeli? Lakini siku hiyo hakumjibu.[#1 Sam. 14:18; 23:9.]

38Ndipo, Sauli aliposema: Njoni hapa, ninyi wakuu wote mnaosimama pembeni kwa watu! Haya! Vumbueni, mwone, kama huku liko kosa gani lililofanyika leo!

39Hivyo, Bwana aliyewaokoa Waisiraeli alivyo Mwenye uzima, ijapo awe mwanangu Yonatani mwenyewe, hana budi kuuawa kabisa! Kwao watu wote hakuna aliyejibu.

40Kisha akawaambia Waisiraeli wote: Ninyi mwe upande mmoja, mimi nami na mwanagu Yonatani tuwe upande mmoja! Watu wakamwambia Sauli: Yaliyo mema machoni pako yafanye!

41Kisha Sauli akamwambia Bwana Mungu wa Isiraeli: Yaumbue yaliyokwisha kufanywa! Wakashikwa Yonatani na Sauli, nao watu wakapona.[#1 Sam. 10:20.]

42Sauli akasema: Nipigieni kura mimi na mwanangu Yonatani! Akashikwa Yonatani.

43Ndipo, Sauli alipomwambia Yonatani; Niambie! Umefanya nini? Yonatani akamsimulia kwamba: Nimeonja asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu, niliyoishika mkononi, sasa basi, nitakufa.[#Yos. 7:19.]

44Sauli akasema: Mungu na anifanyizie hivi na hivi, wewe Yonatani usipokufa kweli!

45Ndipo, watu walipomwambia Sauli: Je? Yonatani atakufa namna gani? Siye aliyewapatia Waisiraeli wokovu huu mkubwa? Hili na lituendee mbali! Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, unywele mmoja tu hautaanguka chini na kutoka kichwani pake! Ndivyo, watu walivyomwokoa Yonatani, asife.

46Kisha Sauli akaacha kuwafuata Wafilisti, akapanda kwenda zake; nao Wafilisti wakaenda zao kwao, walikokaa.

Vita, Sauli alivyovipiga.

47Sauli alipoutwaa ufalme wa Waisiraeli akawapelekea vita adui zake wote waliokaa na kumzunguka: Wamoabu na wana wa Amoni na Waedomu na wafalme wa Soba na Wafilisti, napo pote, alipojielekezea, akawapatiliza vibaya.

48Hivyo akaendelea kupata nguvu, akawapiga Waamaleki, akawaponya Waisiraeli mwao waliowanyang'anya mali zao.

Mlango wa Sauli.

49Wana wa Sauli walikuwa Yonatani na Iswi na Malkisua; wanawe wawili wa kike wa kwanza jina lake ni Merabu, naye mdogo ni Mikali.[#1 Mambo 9:39.]

50Naye mkewe Sauli jina lake ni Ahinoamu, binti Ahimasi, nalo jina la mkuu wa vikosi vyake ni Abineri, mwana wa Neri aliyekuwa baba mdogo wa Sauli,[#1 Sam. 17:55.]

51kwani Kisi, babake Sauli, na Neri, babake Abineri, walikuwa wana wa Abieli.

52Vita vya kupigana na Wafilisti vikawa vikali siku zote za Sauli. Kwa hiyo kila mtu, Sauli aliyemwona kuwa fundi wa vita, na kila mtu mwenye nguvu akamchukua kuandamana naye.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania