The chat will start when you send the first message.
1Samweli akamwambia Sauli: Bwana alinituma, nikupake mafuta, uwe mfalme wao walio ukoo wake wa Waisiraeli. Sasa sikia maneno, Bwana aliyoyasema:[#1 Sam. 10:1.]
2Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Nitayalipiza, Waamaleki waliyowafanyizia Waisiraeli na kuwazibia njia, walipotoka Misri.[#2 Mose 17:8-16; 5 Mose 25:17-19.]
3Sasa nenda, uwapige Waamaleki! Lakini vyote pia, walivyo navyo, sharti viwe mwiko kwenu wa kuwapo, msivionee uchungu, ila sharti mwaue waume hata wake, watoto hata wachanga, ng'ombe hata kondoo, ngamia hata punda![#4 Mose 21:2.]
4Sauli akawapasha watu habari hii, akawakagua huko Telaimu, wakawa 200000 wanaokwenda kwa miguu, nao Wayuda 10000.
5Sauli alipofika penye mji wa Waamaleki, akawavizia mtoni.
6Nao Wakeni Sauli akawaambia: Haya! Ondokeni, mshuke na kujitenga na Waamaleki, nisije kuwamaliza pamoja nao! Kwani ninyi mliwaendea wana wote wa Waisiraeli kwa upole, walipotoka Misri. Ndipo, Wakeni walipoondoka katikati ya Waamaleki.[#Amu. 1:16.]
7Kisha Sauli akawapiga Waamaleki toka Hawila, hata mtu afike Suri ulioelekea Misri.
8Akamteka Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai, lakini watu wote akawaua kwa ukali wa panga kwa kuwatia mwiko wa kuwapo.
9Lakini Sauli pamoja na watu wake wakamhurumia Agagi na mbuzi na kondoo na ng'ombe waliokuwa wazuri kwa kunona na wana kondoo na nyama wengine wa kufuga waliokuwa wazuri, hawakutaka kuwatia mwiko wa kuwapo, wawaue; lakini nyama wote waliokuwa wabayabaya kwa kuugua, ndio, waliowatia mwiko wa kuwapo, wakawaua.
10Ndipo, neno la Bwana lilipomjia Samweli kwamba:
11Ninaona majonzi, kwa kuwa nilimweka Sauli kuwa mfalme, kwani ameacha kunifuata, wala hayatimizi maneno yangu. Kwa hiyo moyo wake Samweli ukachafuka, akamlilia Bwana usiku wote.
12Asubuhi na mapema Samweli akaondoka aje kuonana na Sauli. Samweli akapashwa habari kwamba: Sauli amefika Karmeli, akajisimamishia ukumbusho, kisha akageuka kwenda zake, ashukie Gilgali.
13Samweli alipofika kwake Sauli, Sauli akamwambia: Ubarikiwe na Bwana! Neno la Bwana nimelitimiza.
14Samweli akajibu: Je? Hiki kilio cha mbuzi na cha kondoo masikioni mwangu kinatoka wapi? Nacho kilio cha ng'ombe, ninachokisikia, kinatoka wapi?
15Sauli akasema: Wamewateka kwao Waamaleki; mbuzi na kondoo na ng'ombe walio wazuri watu wamewalimbika kuwa ng'ombe za kumtambikia Bwana Mungu wako; wengine wote tumewatia mwiko wa kuwapo, tukawaua.
16Ndipo, Samweli alipomwambia Sauli: Acha, nikutolee, Bwana aliyoniambia usiku huu! Akamwambia: Sema!
17Samweli akasema: Ulipokuwa mdogo machoni pako, ulipata kuwa kichwa chao mashina ya Waisiraeli, Bwana akakupaka mafuta, uwe mfalme wa kuwatawala Waisiraeli, au sivyo?[#1 Sam. 9:21.]
18Bwana akakutuma kushika njia aliposema: Nenda, uwatie mwiko wa kuwapo, uwaue hao Waamaleki walio wakosaji! Upigane nao, mpaka uwamalize kabisa!
19Mbona hukukiitikia kinywa cha Bwana? Mbona umeyageukia hayo mateka, ukayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana?
20Sauli akamwambia Samweli: Kweli, nimekiitikia kinywa cha Bwana nikaishika njia, Bwana aliyonituma, nikamteka Agagi, mfalme wa Waamaleki, nao Waamaleki nikawatia mwiko wa kuwapo, wauawe;
21ni watu tu waliovunja mwiko kwa kuchukua katika hayo mateka mbuzi na kondoo na ng'ombe waliokuwa wazuri mno, wawe ng'ombe za kumtambikia Bwana Mungu wako huku Gilgali.
22Samweli akamwambia: Je? Bwana anapendezwa na vipaji vya tambiko, ijapo ziwe ng'ombe za kuteketezwa nzima, kama anavyopendezwa ukikiitikia kinywa chake Bwana? Tazama, kutii ni kwema kuliko vipaji vya tambiko, nako kusikiliza ni kwema kuliko mafuta ya kondoo;[#Yes. 1:11; Hos. 6:6; Mat. 9:13; 12:7.]
23kwani upingani ni ukosaji sawasawa kama uchawi, nao ubishi ni upotovu kama kutambikia mizimu. Kwa kuwa umelitangua neno lake Bwana, naye amekutangua, usiwe mfalme tena.[#1 Sam. 16:1.]
24Ndipo, Sauli alipomwambia Samweli: Nimekosa nilipokipita kinywa chake Bwana, nisiyafanye, uliyoniambia; kwani niliwaogopa watu, nikawaitikia sauti zao.
25Sasa liondoe hili kosa langu! Rudi pamoja na mimi, nije kumwangukia Bwana!
26Samweli akamwambia Sauli: Sitarudi pamoja na wewe, kwani umelitangua neno lake Bwana, naye Bwana amekutangua, usiwe mfalme tena wa kuwatawala Waisiraeli.
27Samweli alipogeuka, ajiendee, Sauli akamkamata pindo la kanzu yake, ikararuka.
28Samweli akamwambia: Bwana amekunyang'anya leo ufalme wa Waisiraeli, akampa mwenzako aliye mwema kuliko wewe.[#1 Sam. 28:17.]
29Naye yeye aliye utukufu wa Waisiraeli hasemi uwongo, wala hageuzi moyo, kwani si mtu, ageuze moyo.[#4 Mose 23:19.]
30Sauli akasema: Nimekosa kweli, lakini sasa unipe macheo kwenye hawa wazee wao walio ukoo wangu nako kwao Waisiraeli ukirudi pamoja nami, nije kumwangukia Bwana Mungu wako!
31Ndipo, Samweli aliporudi na kumfuata Sauli, naye Sauli akaja kumwangukia Bwana.
32Samweli akasema: Nileteeni Agagi, mfalme wa Waamaleki! Agagi akafika kwake na kuchangamka, akasema: Kweli uchungu wa kufa umenitoka!
33Lakini Samweli akamwambia: Kama upanga wako ulivyowanyang'anya wanawake wana wao, ndivyo, mama yako anavyongang'anywa leo mwanawe, aondoke kwa wamama wenzake. Kisha Samweli akamkatakata Agagi hapo Gilgali machoni pa Bwana.
34Kisha Samweli akaenda Rama, naye Sauli akapanda nyumbani kwake huko Gibea wa Sauli. Samweli hakumwona Sauli tena mpaka siku ya kufa kwake; kwani Samweli alisikitika kwa ajili ya Sauli, kwa sababu Bwana ameona majonzi, kwa kuwa alimweka Sauli kuwa mfalme wa kuwatawala Waisiraeli.