1 Samweli 16

1 Samweli 16

Dawidi anachaguliwa kuwa mfalme.

1Bwana akamwambia Samweli: Utamsikitikia Sauli mpaka lini? Nami ndiye niliyemtangua, asiwe mfalme wa kuwatawala Waisiraeli. Jaza pembe yako mafuta, nikutume kwa Isai wa Beti-Lehemu! Kwani nimejionea mfalme katika wanawe.[#1 Sam. 15:23,34.]

2Samweli akasema: Nitakwendaje? Sauli akivisikia ataniua. Bwana akasema: Chukua mori ya ng'ombe mkononi mwako, useme: Nimekuja kumtambikia Bwana!

3Mwalike Isai, naye aje kwenye tambiko hilo! Nami nitakujulisha utakayoyafanya, unipakie mafuta yeye, nitakayekuonyesha.

4Samweli akayafanya, Bwana aliyomwambia. Alipofika Beti-Lehemu, wazee wa mji wakamjia njiani na kutetemeka, wakamwamkia kwamba: Kuja kwako ni kwema?[#2 Fal. 9:18.]

5Akawaitikia: Ni kwema, nimekuja kumtambikia Bwana: jieueni, nanyi mje pamoja nami kutambika! Isai na wanawe akawaeua mwenyewe, alipowaalika nao kuja kutambika.

6Ikawa, walipokuja, alipomwona Eliabu akasema moyoni: Labda ni yeye atakayepakwa mafuta mbele yake Bwana.

7Lakini Bwana akamwambia Samweli: Usiitazame sura yake wala ukubwa wa umbo lake! Kwani nimemkataa; maana Bwana havitazami vile, mtu anavyovitazama, kwani mtu huvitazama vilivyopo machoni, lakini Bwana huvitazama vilivyomo moyoni.[#Tume. 10:34; Sh. 7:10.]

8Kisha Isai akamwita Abinadabu, akampitisha machoni pa Samweli, naye akasema: Huyu naye siye, Bwana aliyemchagua.

9Kisha Isai akampitisha Sama, lakini akasema: Huyu naye siye, Bwana aliyemchagua.

10Vivyo hivyo Isai akawapitisha wanawe wote saba machoni pa Samweli, lakini Samweli akamwambia Isai: Hawa sio, Bwana aliowachagua.[#1 Mambo 2:13-15.]

11Kisha Samweli akamwuliza Isai: Wanao wote ni hao tu? Akasema: Amesalia yule mdogo, naye anachunga kondoo. Samweli akamwambia Isai: Tuma, wamlete! Kwani hatutakaa mezani, mpaka atakapofika hapa.[#1 Sam. 17:14.]

12Basi, akatuma, wakamleta, naye alikuwa mwekundu mwenye macho mazuri na umbo jema. Ndipo, Bwana alipomwambia: Haya! Umpake mafuta! Kwani huyu ndiye.

13Samweli akaichukua pembe yake ya mafuta, akampaka mafuta katikati ya kaka zake. Ndipo, Roho ya Bwana ilipomjia Dawidi kuanzia siku hiyo, ikamkalia siku zote. Kisha Samweli akaondoka kwenda Rama.[#2 Sam. 2:4; 5:3.]

Dawidi anampendeza Sauli kwa kupiga zeze.

14Royo yake Bwana ikaondoka mwake Sauli, nayo roho mbaya iliyotoka kwa Bwana ikamhangaisha.[#1 Sam. 18:10.]

15Ndipo, watumishi wa Sauli walipomwambia: Tazama, roho mbaya ya Mungu inakuhangaisha!

16Wewe bwana wetu na uwaagize watumishi wako wanaokutumikia, watafute mtu aliye fundi wa kupiga zeze. Napo, itakapokujia ile roho mbaya ya Mungu, basi, akikupigia zeze kwa mkono wake, utaona vema.[#2 Fal. 3:15.]

17Sauli akawaambia watumishi wake: Nitafutieni mtu anayejua vema kupiga zeze, kamleteni kwangu!

18Mmoja wao wale vijana akajibu akisema: Nimemwona mwana wa Isai wa Beti-Lehemu, ya kuwa anajua kupiga zeze, tena ni fundi wa vita menye nguvu za kupigana vitani na za kusemea watu, ni mtu mzuri wa kupendeza, naye Bwana yuko pamoja naye.

19Ndipo, Sauli alipotuma wajumbe kwa Isai na kumwambia: Mtume mwanao Dawidi achungaye kondoo, aje kwangu!

20Isai akatoa punda wa kuchukua mzigo wa chakula na kiriba cha mvinyo, tena akampa mwana mbuzi mmoja, akavituma kwa Sauli mkononi mwa mwanawe Dawidi.

21Ndivyo, Dawidi alivyokwenda kwake Sauli, akamfanyizia kazi. Sauli akampenda sana, akawa mchukua mata yake.

22Sauli akatuma kwa Isai kwamba: Dawidi na akae kwangu, kwani macho yangu yanamwona kuwa mpole.

23Ikawa kila mara, ile roho ya Mungu ilipomjia Sauli, Dawidi akalichukua zeze lake, akalipiga kwa mkono wake; ndipo, Sauli alipotulia na kuona vema, ile roho mbaya ikaondoka kwake.[#1 Sam. 16:14.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania