1 Samweli 17

1 Samweli 17

Dawidi anamwua Goliati.

1Wafilisti wakavikusanya vikosi vyao kwenda vitani, wakakusanyika Soko katika nchi ya Yuda, wakapiga makambi Efesi-Damimu katikati ya Soko na Azeka.

2Sauli naye na watu wa Waisiraeli wakakusanyika, wakapiga makambi kwenye Bonde la Mkwaju, wakajitengeneza kuja kupigana na Wafilisti.

3Wafilisti wakawa wamesimama mlimani ng'ambo ya huko, nao Waisiraeli wakawa wamesimama ng'ambo ya huku, bonde likiwa katikati yao.

4Katika makambi ya Wafilisti kukatokea jitu, jina lake Goliati wa Gati, urefu wake ulikuwa mikono sita na nusu.[#Yos. 11:22.]

5Alikuwa amevaa kofia ya shaba kichwani, tena kifuani fulana ya chuma, nao uzito wa hiyo fulana ulikuwa sekeli 5000, ndio frasila 5 za shaba.

6Miguuni alikuwa amevaa shaba vilevile penye miundi, namo mabegani kikingio cha shaba.

7Uti wa mkuki wake ulikuwa nguzo kama mti wa mfuma nguo, nayo ncha ya chuma ya mkuki wake ilikuwa sekeli 600, ndio nusu kubwa ya frasila ya chuma; naye mchukua ngao humtangulia.

8Akaja kusimama mbele akipaza sauti sana na kuwaita Waisiraeli waliojipanga, akawaambia: Mbona mmetoka, mkajipanga kupiga vita? Mimi si Mfilisti? Nanyi sio watu wa Sauli? Chagueni mtu wa kwenu, ashuke kuja kwangu!

9Akiweza kupigana na mimi na kunishinda, basi, tutakuwa watumwa wenu; lakini mimi nikimweza na kumshinda, ninyi mtakuwa watumwa wetu, mtutumikie.

10Kisha huyo Mfilisti akasema: Siku hii ya leo nimewabeza Waisiraeli waliojipanga, nikiwaambia: Nipeni mtu, tupigane naye![#2 Fal. 19:4,16.]

11Sauli na Waisiraeli wote walipoyasikia hayo maneno ya huyo Mfilisti wakaingiwa na vituko, wakaogopa sana.

12Dawidi alikuwa mwana wa yule mtu wa Efurata, ndio Beti-Lehemu wa Yuda, jina lake Isai, aliyekuwa mwenye wana wanane; siku zile za Sauli mwenyewe alikuwa mzee mwenye miaka kuliko wengine.[#1 Sam. 16.]

13Lakini wana watatu wakubwa wa Isai walikuwa wamemfuata Sauli kwenda vitani, nayo majina yao hawa wanawe watatu waliokwenda vitani ni haya: wa kwanza ni Eliabu, wa pili Abinadabu, wa tatu Sama.[#1 Sam. 16:6,8-9.]

14Naye Dawidi alikuwa mdogo; kwa kuwa wale wakubwa watatu walikuwa wamemfuata Sauli,

15Dawidi akatoka mara kwa mara kwake Sauli kwenda kuchunga kondoo wa baba yake huko Beti-Lehemu, kisha akarudi.

16Lakini yule Mfilisti akatoka asubuhi na jioni siku 40 akija kujisimamisha papo hapo.

17Kisha Isai akamwambia mwanawe Dawidi: Wapelekee kaka zako mzigo huu wa bisi na hii mikate kumi. Upige mbio, uifikishe upesi kambini kwa kaka zako!

18Navyo hivi vikate kumi vya maziwa yaliyoganda umpelekee mkuu wa elfu, upate kuwatazama kaka zako, kama hawajambo, nao na wakupe kitu cha kwao, ukilete!

19Kwani Sauli nao hao na Waisiraeli wote walikuwako kule kwenye Bonde la Mkwaju wakipigana na Wafilisti.

20Kesho yake Dawidi akaamka na mapema akimwachia mwangaliaji mwingine kondoo na mbuzi, akavichukua alivyopewa, akaenda zake, kama Isai alivyomwagiza; akafika penye magari, vikosi vilipotoka kujipanga na kupiga yowe za vita.

21Nao Waisiraeli wakajipanga ng'ambo ya huku, nao Wafilisti ng'ambo ya huko, wakaelekeana.

22Dawidi akautua ule mzigo, akauacha mkononi mwake mlinda mizigo, akakimbilia hapo, walipojipanga, alipofika akaamkiana na kaka zake.

23Akingali katika kusema nao, mara hapo, Wafilisti walipojipanga, lile jitu likatokea, jina lake Goliati, Mfilisti wa Gati, akayasema maneno yaleyale; Dawidi naye akayasikia.

24Watu wote wa Waisiraeli walipomwona mtu huyo wakamkimbia wote, kwani wakaogopa sana.

25Kukawa na mtu wa Kiisiraeli akasema: Mmemwona huyo mtu aliyepanda? Hupanda tu kuwatweza Waisiraeli. Mtu atakayempiga mfalme atampa mali nyingi, hata mwanawe wa kike atampa, awe mkewe, nao mlango wa baba yake utafunguliwa, usitoe kodi kwao Waisiraeli.

26Dawidi akawauliza wale watu waliosimama pamoja naye akisema: Mtu akimpiga huyo Mfilisti na kuiondoa soni kwao Waisiraeli atafanyiziwa nini? Kwani huyo Mfilisti asiyetahiriwa ni mtu gani akiwatweza wapiga vita wa Mungu aliye Mwenye uzima?

27Watu wale wakamwambia neno lilelile la kwamba: Hivi ndivyo, atakavyofanyiziwa mtu atakayempiga.

28Kaka yake Eliabu aliposikia, alivyosemezana na wale watu, makali yake Eliabu yakawaka moto kwa kumkasirikia Dawidi, akamwuliza: Umeshukia nini? Tena hivyo vikondoo vyetu umemwachia nani huko nyikani? Mimi ninayajua majivuno yako na ubaya wa moyo wako, kwani umeshuka tu kutazama vita.

29Dawidi akamwuliza: Nimekosa nini sasa? Hilo si neno la kuuliza tu?

30Kisha akaondoka hapo pake, akaja pengine kuulizana na watu neno lilo hilo, nao wakamjibu maneno yayo hayo ya kwanza.

31Watu walipoyasikia, Dawidi aliyoyasema, wakaja kwa Sauli kumsimulia habari hizo, kisha wakamchukua.

32Dawidi akamwambia Sauli: Mtu asipotelewe na moyo kwa ajili yake yeye! Mtoto wako atakwenda kupigana na huyo Mfilisti.

33Sauli akamwambia Dawidi: Hutaweza kumwendea huyo Mfilisti, upigane naye, kwani u kijana, naye yeye ni mpiga vita tangu utoto wake.

34Dawidi akamwambia Sauli: Mtoto wako alipokuwa anachunga kondoo wa baba yake, basi, simba au chui walipokuja kukamata kondoo kundini,

35nikatoka kuwafuata, nikawapiga, nikawaopoa vinywani mwao; kama aliniinukia, nikamkamata ndevu zake, nikampiga, hata nikamwua.

36Kama mtoto wako alivyowapiga simba na chui, vivyo hivyo hata huyo Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwani amewatweza wapiga vita wa Mungu aliye Mwenye uzima.

37Kisha Dawidi akasema: Bwana aliyeniponya mikononi mwa simba namo mikononi mwa chui ndiye atakayeniponya namo mkononi mwa huyo Mfilisti. Ndipo, Sauli alipomwambia Dawidi: Basi, nenda! Bwana awe nawe!

38Sauli akamvika Dawidi mavazi yake ya vitani, kichwani pake akamtia kofia ya shaba, akamvika hata fulana ya chuma.

39Dawidi akajifunga nao upanga wake juu ya hayo mavazi ya vitani. Lakini alipotaka kwenda, kwani alikuwa hajavijaribu, Dawidi akamwambia Sauli: Siwezi kwenda nayo haya, kwani sikuyajaribu bado; kisha Dawidi akayavua, akayaweka,

40akaichukua fimbo yake mkononi mwake, akajichagulia mtoni vijiwe vitano vilivyoviringana vizuri, akavitia katika mkoba, aliokuwa nao, maana ni mfuko wake, akashika nalo kombeo, kisha akamwendea yule Mfilisti.[#1 Mambo 11:23.]

41Yule Mfilisti naye akaja kumfikia Dawidi karibu, naye mchukua ngao akamtangulia.

42Yule Mfilisti alipochungulia, amwone Dawidi, akambeza, kwa kuwa ni kijana bado, tena ni mwekundu na mwenye umbo zuri.[#1 Sam. 16:12.]

43Ndipo, yule Mfilisti alipomwambia Dawidi: Mimi ni mbwa, ukinijia na fimbo? Kisha Mfilisti akamwapiza Dawidi na kuitaja miungu yake.

44Mfilisti akamwambia Dawidi: Njoo kwangu! Nyama za mwili wako nitawapa ndege wa angani na nyama wa porini![#Ez. 29:5.]

45Lakini Dawidi akamwambia Mfilisti: Wewe unanijia na kushika upanga na mkuki na ngao, lakini mimi ninakujia katika Jina la Bwana Mwenye vikosi, aliye Mungu wao wapiga vita vya Waisiraeli, uliyemtukana!

46Siku hii ya leo Bwana amekutia mkononi mwangu, nikupige, nikukate kichwa mwilini pako, nayo mizoga ya vikosi vya Wafilisti siku hii ya leo nitawapa ndege wa angani na nyama wa porini, watu wote wa nchini wapate kujua, ya kuwa aliye Mungu yuko kwao Waisiraeli.

47Nao wote wa mkutano huu watajua, ya kuwa Bwana haokoi kwa nguvu za upanga wala za mkuki, kwani vita hivi ni vyake Bwana, naye amewatia mikononi mwetu.

48Ikawa, yule Mfilisti alipoinuka, aje kumfikia Dawidi karibu, Dawidi naye akapiga mbio, afike upesi hapo, walipojipanga, akutane na yule Mfilisti.

49Dawidi akautia mkono wake upesi mkobani, akatoa humo kijiwe, akakitupa kwa kombeo, akampiga yule Mfilisti pajini, nacho kijiwe kikaingia pajini ndani; ndipo, alipoanguka kifudifudi hapo chini.

50Hivyo ndivyo, Dawidi alivyomshinda yule Mfilisti kwa kombeo na kwa kijiwe, akampiga yule Mfilisti na kumwua pasipo kushika upanga mkononi mwake yeye Dawidi.

51Kisha Dawidi akapiga mbio, akasimama pake yule Mfilisti, akauchukua upanga wake akiuchomoa alani mwake, akamwua kabisa na kukikata kichwa chake; Wafilisti walipoona, ya kuwa fundi wao wa vita amekufa, ndipo, walipokimbia.

52Lakini watu wa Waisiraeli na Wayuda wakainuka, wakaondoka na kupiga yowe, wakawakimbiza Wafilisti mpaka kufika Gai na malango ya Ekroni, nao Wafilisti walioumizwa wakaanguka njiani kwenda Saraimu, hata Gati na Ekroni.

53Kisha wana wa Isiraeli wakarudi walipokwisha kuwafukuza sana Wafilisti, wakayateka yaliyokuwapo makambini mwao.

54Dawidi akakichukua kichwa chake yule Mfilisti, akakipeleka Yerusalemu, lakini mata yake akayaweka hemani mwake.

55Sauli alipoona, Dawidi alivyotoka, akutane na yule Mfilisti, akamwuliza Abineri, mkuu wa vikosi: Huyu kijana ni mwana wa nani? Abineri akasema: Hivyo roho yako, mfalme, ilivyo nzima, sijui.[#1 Sam. 14:50.]

56Mfalme akamwambia: Uliza, kama hili jana ni mwana wa nani?

57Dawidi aliporudi akiisha kumwua yule Mfilisti, Abineri akamchukua, akampeleka kwa Sauli, akikishika kichwa chake yule Mfilisti mkononi mwake.

58Sauli akamwuliza: Wewe kijana, u mwana wa nani? Dawidi akasema: Ni mwana wa mtumishi wako Isai wa Beti-Lehemu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania