1 Samweli 19

1 Samweli 19

Dawidi anamkimbilia Samweli kwa kunyatiwa na Sauli.

1Sauli akala njama na mwanawe Yonatani na watumishi wake wote ya kumwua Dawidi. Lakini Yonatani, mwana wa Sauli, alikuwa amependezwa sana na Dawidi.[#1 Sam. 18:3.]

2Kwa hiyo Yonatani akampasha Dawidi habari kwamba: Baba yangu Sauli anatafuta njia ya kukuua; sasa ujiangalie kesho! Kaa mafichoni na kujificha kabisa!

3Mimi nitatoka, nisimame kando yake baba yangu huko shambani, utakakokuwa, niseme na baba yangu kwa ajili yako, nipate habari za kukupasha wewe.

4Kisha Yonatani akamsemea mema kwa baba yake Sauli kwamba: Mfalme asije kumkosea mtumishi wake Dawidi! Kwani hakukukosea neno, ila amekufanyizia mema sana.

5Alipokwenda kumwua yule Mfilisti alijitoa mwenyewe; ndipo, Bwana alipowapatia Waisiraeli wote wokovu mkubwa, nawe ukaviona, ukafurahi. Mbona unataka kujikosesha kwa kumwaga damu ya mtu asiyekosa ukimwua Dawidi bure tu?[#1 Sam. 17:50.]

6Sauli akakiitikia kinywa cha Yonatani, yeye Sauli akaapa kwamba: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, hatauawa kabisa!

7Kisha Yonatani akamwita Dawidi, akamsimulia maneno haya yote; kisha Yonatani akampeleka Dawidi kwa Sauli, akakaa kwake kama siku zote za mbele.

8Vita vilipoendelea kuwapo, Dawidi akatoka kupigana na Wafilisti, akawapiga pigo kubwa, nao wakamkimbia.

9Ndipo, ile roho mbaya ya Bwana ilipomjia Sauli, naye alikuwa anakaa nyumbani mwake akishika mkuki wake mkononi, naye Dawidi alikuwa akimpigia zeze kwa mkono wake.[#1 Sam. 18:10-11.]

10Sauli akataka kumchoma Dawidi ukutani kwa mkuki, lakini Dawidi akajiepusha, Sauli asimpate, mkuki ukauchoma ukuta tu. Ndipo, Dawidi alipokimbia kwa hivyo, alivyopona. Usiku huo

11Sauli akatuma wajumbe kwenda kuivizia nyumba ya Dawidi, wapate kumwua asubuhi. Lakini mkewe Mikali akampasha Dawidi habari kwamba: Usipojiponya usiku huu, utauawa kesho![#Sh. 59:1.]

12Kisha Mikali akamshusha Dawidi dirishani, akaenda zake na kukimbia; ndivyo, alivyopona.

13Kisha Mikali akakichukua kinyago cha nyumbani, akakilaza kitandani, kichwani pake akaweka mto wa manyoya ya mbuzi, akakifunika kwa nguo.

14Sauli alipotuma wajumbe kumchukua Dawidi, akawaambia: Ni mgonjwa.

15Sauli akawatuma wale wajumbe tena kumtazama Dawidi akiwaambia: Mleteni kwangu, akilala kitandani, nipate kumwua!

16Wajumbe walipoingia nyumbani wakakiona kile kinyago, kimelala kitandani, nao mto wa manyoya ya mbuzi uko kichwani pake.

17Sauli akamwuliza Mikali: Kwa sababu gani umenidanganya hivyo, ukamwacha mchukivu wangu, apone? Mikali akamwambia Sauli: Ameniambia: Niache, nijiendee! Mbona unataka nikuue?

18Naye Dawidi alipopona kwa kukimbia akaenda Rama kwa Samweli, akamsimulia yote, Sauli aliyomfanyizia, kisha wakaenda yeye na Samweli, wakakaa Nayoti.

Sauli anaingia kundini mwa wafumbuaji.

19Sauli akapashwa habari za kwamba: Tazama, Dawidi yuko Nayoti kule Rama!

20Ndipo, Sauli alipotuma wajumbe kumchukua Dawidi. Hao walipoona kundi la wafumbuaji wakifumbua mambo, naye Samweli akisimama kwao kama kiongozi wao, ndipo, roho ya Mungu ilipowajia wajumbe wa Sauli, nao wakafumbua mambo.[#1 Sam. 10:10-12.]

21Walipompasha Sauli habari hizi, akatuma wajumbe wengine, lakini nao wakaja kufumbua mambo. Ndipo, Sauli alipoendelea kutuma wajumbe mara ya tatu, lakini nao wakaja kufumbua mambo.

22Kisha naye mwenyewe akaenda Rama; alipofika penye shimo kubwa la maji lililoko Seku akauliza kwamba: Samweli na Dawidi wako wapi? Wakamwambia: Utawaona Nayoti kule Rama.

23Alipokwenda Nayoti kule Rama, yeye naye roho ya Mungu ikamjia; ndipo, alipokwenda hapo njiani na kufumbua mambo, hata akifika Nayoti kule Rama.

24Ndipo, yeye naye alipoyavua mavazi yake, naye akafumbua mambo mbele ya Samweli, akalala chini mwenye uchi mchana huo wote na usiku huo wote, kwa hiyo watu husema: Kumbe Sauli naye yumo katika wafumbuaji!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania