1 Samweli 2

1 Samweli 2

Matukuzo ya Hana.

1Hana akaomba na kusema:

Moyo wangu unashangilia kwa kuwa naye Bwana, pembe yangu imetukuka kwa nguvu za Bwana, nimeasama kinywa changu, kiwatishe wachukivu wangu, kwani ninaufurahia msaada wako.

2Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana, kwani pasipo wewe hakuna Mungu, wala hakuna mwamba kama Mungu wetu.

3Msizidi kusema makuu ya kujikuza, maneno makorofi yasitoke vinywani mwenu! Kwani Bwana ni Mungu mwenye ujuzi, kwake yeye hujaribiwa matendo ya watu.

4Pindi za mafundi wa vita huvunjika, lakini waliokwazwa hujivika nguvu.

5Walioshiba hufanya kazi, wapate chakula tu, lakini waliokuwa wenye njaa, njaa zao hukoma kabisa, mwanamke mgumba huzaa watoto saba, naye mwenye wana wengi hufifia.

6Bwana huua, naye hurudisha uzimani, yeye hushusha kuzimuni, tena hupaza juu.[#5 Mose 32:39.]

7Bwana wengine huwakosesha mali, wengine huwazidishia, hunyenyekeza, tena hukuza;[#Sh. 75:8.]

8mnyonge humwinua uvumbini, mkiwa humtoa jaani, awaketishe pamoja nao walio wakuu akiwapa kiti chenye utukufu, kiwe chao, kwani misingi ya nchi ni yake Bwana, juu yao ameuweka ulimwengu.[#Sh. 113:7-8.]

9Huiangalia miguu yao wamchao, lakini wasiomcha huangamizwa penye giza, kwa kuwa hakuna mtu atakayeshinda kwa nguvu zake.[#Sh. 33:16.]

10Watakaoshindana na Bwana watapondwa, atakapovumisha ngurumo juu yao mbinguni. Bwana atayahukumu mapeo ya nchi, naye mfalme wake atampa uwezo atakapoitukuza pembe yake yeye, aliyempaka mafuta.[#Sh. 132:17.]

11Kisha Elkana akaenda Rama nyumbani kwake, lakini yule mtoto akawa akimtumikia Bwana machoni pake mtambikaji Eli.

Ubaya wa wana wa Eli.

12Wana wa Eli walikuwa watu wasiofaa kabisa, hawakumjua Bwana,

13wala haki za watambikaji, wala haki za watu: mtu ye yote alipotoa ng'ombe ya tambiko, nyama zilipotokota, mtumishi wa mtambikaji huja akishika mkononi uma mkubwa wenye michomo mitatu,[#2 Mose 27:3.]

14akakoroga nao chunguni au kaangoni au sufuriani au bakulini, nazo nyama zote, ule uma ulizozipandisha, mtambikaji huzichukua. Ndivyo, walivyowafanyizia Waisiraeli wote, wakija huko Silo.

15Napo, walipokuwa hawajachoma mafuta, mtumishi wa mtambikaji huja, amwambie mwenye kutambika: Nipe nyama ya kumchomea mtambikaji! Naye hataki kwako nyama iliyopikwa, ila mbichi.[#3 Mose 3:3-5.]

16Yule mtu akimwambia: Leo watayachoma mafuta, kisha jichukulie, roho yako iyatakayo, humwambia: Sharti unipe sasa hivi! Kama hutaki, nitachukua kwa nguvu.

17Kwa hiyo ukosaji wao hao vijana ukawa mkubwa sana machoni pake Bwana, kwani kwa hiyo watu wakavibeza vipaji vya tambiko, Bwana alivyotolewa.

18Lakini mtoto Samweli akamtumikia Bwana, akawa amevikwa kisibau cha mtambikaji cha nguo ya ukonge.

19Naye mama yake akamshonea kanzu ndogo, akampelekea mwaka kwa mwaka, alipopanda na mumewe kutoa ng'ombe ya tambiko ya mwaka.

20Eli akambariki Elkana na mkewe akisema: Bwana na akupatie kizazi kwake mwanamke huyu cha kumlipa ombo lake, alilomwomba Bwana! Kisha wakaenda zao kufika kwao.

21Naye Bwana akamkagua Hana, akapata mimba, akazaa watoto wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye mtoto Samweli akawako akikua machoni pake Bwana.[#Luk. 1:80.]

22Eli akawa mkongwe kabisa; alipoyasikia yote, wanawe wanayowafanyizia Waisiraeli wote, tena ya kuwa hulala na wanawake wanaotumikia langoni penye Hema la Mkutano,[#2 Mose 38:8.]

23akawaambia: Mbona mnafanya mambo mabaya kama hayo, mimi ninayoyasikia na hawa watu wote, ya kuwa mnayafanya?

24Msifanye hivyo wanangu! Kwani uvumi huu, ninaousikia mimi wa kuwakosesha watu wa Bwana, si mwema.

25Mtu akimkosea mtu mwenziwe, Mungu atampatiliza, lakini akimkosea Bwana, yuko nani atakayemwombea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwani Bwana alitaka kuwaua.

26Lakini mtoto Samweli akaendelea kukua na kuwa mwema machoni pake Bwana, napo machoni pa watu.[#Luk. 2:52.]

Eli anafumbuliwa yatakayompata yeye na wanawe.

27Kisha mtu wa Mungu akaja kwa Eli, akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kumbe sikujitokeza kwa mlango wa baba yako, walipoutumikia mlango wa Farao huko Misri?

28Nikauchagua katika mashina yote ya Waisiraeli kuwa watambikaji, wapande pangu pa kutambikia na kuvukiza uvumba na kuvaa kisibau cha mtambikaji mbele yangu, nikaupa mlango wa baba yako ng'ombe zote za tambiko, wana wa Isiraeli wanazozitoa za kuteketezwa motoni.[#4 Mose 18:8.]

29Mbona mnazipiga mateke ng'ombe zangu za tambiko na vipaji vyangu vya tambiko, nilivyoagiza, wavitoe katika Kao langu? Unawacha wanao kuliko mimi, mpate kujinonesha na kuvila vipande vilivyo vizuri vya vipaji vyote vya tambiko vyao walio ukoo wangu wa Isiraeli.[#Tume. 9:5.]

30Kwa hiyo ndivyo, asemavyo Bwana Mungu wa Isiraeli: Kweli nilisema, mlango wako na mlango wa baba yako na waendelee machoni pangu kale na kale. Lakini sasa ndivyo, asemavyo Bwana: Hili na liniendee mbali! Kwani anichaye nitampa macheo, lakini anibezaye atabezwa naye.[#2 Mose 28:1.]

31Utaona, siku zikija, nitakapoukata mkono wako nayo mikono yao walio wa mlango wa baba yako, asipatikane mzee katika mlango wako.[#1 Fal. 2:27.]

32Ndipo, utakapoutazama ukiwa wa kao lako ukiona mema yote, atakayowafanyizia Waisiraeli, kwani siku hizo zote hatakuwapo mzee katika mlango wako.

33Ijapo nisimwangamize ye yote wa kwako na kumtoa pangu pa kutambikia, atakuwa tu wa kuyafifiliza macho yako na wa kuikatisha roho yako tamaa, lakini wao wengi wa mlango wako watakufa watakapokuwa waume wazima.[#1 Sam. 22:20.]

34Kielekezo chako yatakuwa hayo yatakayowapata wanao wawili Hofuni na Pinehasi: hao wawili watakufa siku moja.[#1 Sam. 4:11.]

35kisha nitajiinulia mtambikaji mwelekevu atakayeyafanya mapenzi ya moyo wangu na ya Roho yangu; yeye nitamjengea nyumba ya kweli, aendelee siku zote machoni pake yule, nitakayempaka mafuta.

36Nao wote watakaosazwa katika mlango wako watamjia na kumwangukia, wapate thumuni tu au mkate mdogo na kumwomba: Nipe kazi moja tu ya utambikaji, nipate kula kipande cha mkate!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania