The chat will start when you send the first message.
1Dawidi akakimbia Nayoti kule Rama, akaja kuonana na Yonatani, akamwuliza: Nimefanya nini? Nimekora manza gani kwake baba yako au nimemkosea nini, akitafuta njia ya kuniua?
2Akamwambia: Sivyo kabisa, hutauawa. Tazama, baba yangu hafanyi jambo, kama ni kubwa au kama ni dogo, asiponitolea masikioni pangu. Basi, jambo hili baba yangu angenifichaje? Hanalo kweli.
3Dawidi akasema tena na kuapa: Baba yako anajua kabisa, ya kuwa nimepata upendeleo machoni pako, kwa hiyo alisema: Yonatani asilijue, asisikitishwe. Lakini hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena hivyo, roho yako ilivyo nzima, kwangu kutoka maishani kwenda kufani ni hatua moja tu.
4Yonatani akamwambia Dawidi: Mwenyewe utakayoniambia, nitakufanyizia.
5Dawidi akamwambia Yonatani: Tazama, kesho ni mwandamo wa mwezi; hapo inanipasa kula mezani pa mfalme, lakini nipe ruhusa, nijifiche shambani hata siku ya tatu jioni.
6Baba yako akiniuliza, useme: Dawidi ameomba ruhusa kwangu kwenda upesi Beti-Lehemu, kwani siku hizi liko tambiko lao la ukoo wao mzima.
7Naye akikuambia: Ni vema, basi, mtumishi wako amepata kutengemana; lakini makali yake yakiwaka moto, ndipo, utakapojua, ya kuwa mabaya yamekwisha kujaa moyoni mwake.
8Umhurumie mtumishi wako na kufanya hivyo! Kwani mtumishi wako umefanya agano naye machoni pa Bwana. Kama ziko manza, nilizozikora, niue wewe! Lakini usinipeleke kwa baba yako![#1 Sam. 18:3.]
9Yonatani akasema: Hili lisikupate! Hapo, nitakapojua, ya kuwa mabaya yamekwisha kujaa moyoni mwa baba yangu, na nije kwako, nikusimulie yote.
10Dawidi akamwuliza Yonatani: Ni nani atakayenipasha habari, kama baba yako amekujibu neno gumu?
11Yonatani akamwambia Dawidi: Haya! Tutoke hapa kwenda shambani! Wakatoka wote wawili kwenda shambani.
12Yonatani akamwambia Dawidi: Bwana Mungu wa Isiraeli ni shahidi! Kesho wakati kama huu au kesho kutwa nikimchunguza baba yangu na kuona, ya kuwa anayo mema ya kumfanyizia Dawidi, basi, nisipotuma mtu kwako, niyafunue masikioni pako,
13Bwana na aendelee kumfanyizia Yonatani hivi na hivi! Lakini baba yangu akiona kuwa vema kukufanyizia mabaya, nitayafunua nayo masikioni pako, upate kwenda zako na kutengemana; naye Bwana awe na wewe, kama alivyokuwa na baba yangu!
14Lakini nawe usinifanyie huruma ya Bwana siku hizi tu, nikiwa nipo bado, nisipate kufa,
15ila nao mlango wangu usiunyime huruma yako kale na kale, hata hapo, Bwana atakapowatowesha wachukivu wa Dawidi, kila mtu mahali pake juu ya nchi hii!
16Ndivyo, Yonatani alivyoagana na mlango wa Dawidi akisema: Bwana na awalipishe wachukivu wa Dawidi!
17Yonatani akamwapisha Dawidi tena kwa hivyo, alivyompenda, kwa kuwa alimpenda, kama alivyojipenda mwenyewe.[#1 Sam. 18:3.]
18Kisha Yonatani akamwambia: Kesho ni mwandamo wa mwezi; ndipo, utakapoulizwa, kwani kiti chako kitakuwa hakina mtu.
19Kesho kutwa sharti ushuke kabisa kuja mahali pale, ulipojificha siku ile, tulipoanza shauri, ukae hapo kando ya jiwe la Ezeli.
20Nami nitapiga mishale mitatu kando yake, kama nitapiga shabaha.
21Kisha nitatuma mtoto na kumwambia: Nenda, itafute mishale! Hapo, nitakapomwitia huyu mtoto kwamba: Tazama, mishale iko nyuma yako, iokote upande wa huku! utakuja, kwani kutakuwa kumetengemana, hakuna neno baya hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima!
22Lakini kama nitamwitia yule kijana kwamba: Tazama, mishale iko mbele yako! basi, jiendee! Kwani Bwana amekutuma.
23Neno hili, tulilolisemezana mimi na wewe, tazama, Bwana ni shahidi wangu na wako kale na kale!
24Kisha Dawidi akajificha shambani. Siku ya mwandamo wa mwezi ilipotimia, mfalme akajikalisha penye chakula, ale.
25Naye mfalme akakaa mahali pake pa siku zote, ni hapo ukutani; naye Yonatani akaja kusimama hapo, naye Abineri akakaa kando yake Sauli; lakini kiti chake Dawidi kikawa hakina mtu.
26Lakini siku hiyo Sauli hakusema neno, kwani alisema moyoni: Labda liko tukio lililompata, asiwe ametakata, kwa kuwa hakueuliwa.[#3 Mose 15; 5 Mose 23:10.]
27Hata kesho yake, ndio siku ya pili ya mwezi, kiti chake kikawa tena hakina mtu. Ndipo, Sauli alipomwuliza mwanawe Yonatani: Mbona mwana wa Isai hakuja jana na leo chakulani?
28Yonatani akamjibu Sauli: Dawidi ameomba ruhusa kwangu kwenda Beti-Lehemu,
29akasema: Nipe ruhusa, kwani liko tambiko la ukoo wetu katika mji huo, kaka yangu akaniagiza kwenda. Sasa kama nimeona upendeleo machoni pako, acha, niende upesi kuonana na ndugu zangu! Kwa hiyo hakufika mezani pa mfalme.
30Ndipo, makali ya Sauli yalipomwakia Yonatani, akamwambia: Wewe mwana wa mama mpotovu mwenye ukatavu wa kutii, sikujui, ya kuwa umemchagua mwana wa Isai? Ndivyo, unavyojitweza mwenyewe, hata mama yako utamtokeza, akiwa mwenye uchi!
31Kwani siku zote, huyu mwana wa Isai akiwa yu hai hapa nchini, wewe hutashupaa wala ufalme wako. Sasa hivi tuma mtu, amchukue kumleta kwangu! Kwani hana budi kufa.
32Yonatani akamjibu baba yake Sauli akimwuliza: Auawe kwa sababu gani? Amefanya nini?
33Ndipo, Sauli alipomtupia Yonatani mkuki wake, amchome; kwa hiyo Yonatani akajua, ya kuwa baba amekwisha kukata shauri la kumwua Dawidi.[#1 Sam. 18:11.]
34Yonatani akaondoka hapo mezani kwa makali yaliyowaka moto, hakula chakula cho chote siku hiyo ya pili ya mwandamo wa mwezi, kwani alimsikitikia Dawidi, kwa kuwa baba yake amemtukana.
35Asubuhi yake Yonatani akatoka kwenda shambani pamoja na mtoto mdogo saa ileile, aliyoagana na Dawidi.
36Akamwambia mtoto: Upige mbio kuitafuta mishale, nitakayoipiga. Mtoto alipopiga mbio, yeye akapiga mshale na kupita hapo, alipo.
37Mtoto alipofika hapo, mshale, Yonatani alioutupa, ulipo, Yonatani akamwitia mtoto kwamba: Mshale hauko mbele yako?
38Kisha Yonatani akamwitia mtoto kwamba: Kaza mwendo upesiupesi, usisimame! Mtoto wa Yonatani alipokwisha kuiokota mishale akaja kwa bwana wake.
39Lakini mtoto hakujua maana, ni Yonatani na Dawidi tu waliolijua hilo jambo.
40Kisha Yonatani akampa huyu mtoto aliyekuwa naye mata yake, akamwambia: Nenda, uyapeleke mjini!
41Mtoto alipokwisha kwenda, Dawidi akatokea upande wa kusini, akauinamisha uso wake chini mara tatu na kumwangukia mara tatu, kisha wakanoneana na kulia machozi pamoja wao wawili, lakini Dawidi akazidi.[#1 Mose 33:3-4.]
42Kisha Yonatani akamwambia Dawidi: Nenda na kutengemana! Na viwe, tulivyoapiana sisi wawili na kulitaja Jina la Bwana kwamba: Bwana na atushuhudie mimi na wewe, wazao wangu na wazao wako kale na kale!
43Kisha Dawidi akaondoka kwenda zake, naye Yonatani akaenda mjini.