The chat will start when you send the first message.
1Dawidi akaja Nobe kwa mtambikaji Ahimeleki; Ahimeleki akashikwa na woga, akamwendea Dawidi njiani, akamwuliza: Mbona unakuja peke yako, usiwe na mtu wa kufuatana na wewe?
2Dawidi akamwambia mtambikaji Ahimeleki: Mfalme ameniagiza neno na kuniambia: Mtu asilijue hili neno, ninalokutuma nililokuagiza! Wako vijana, niliowaagiza, waje mahali fulani.
3Una chakula gani sasa? Kama ni mikate mitano, nipe, niende nayo, au cho chote kingine kinachoonekana!
4Mtambikaji akamjibu Dawidi akisema: Sinayo mikate ya kula, ila iko mikate mitakatifu tu; ingewezekana, kama vijana wale wangalijiangalia, wasiguse wanawake.[#2 Mose 19:15; 3 Mose 22:3-7; 24:5-9.]
5Dawidi akamjibu mtambikaji akimwambia: Tangu jana na juzi tumenyimwa wanawake; napo, nilipotoka, miili ya vijana hao ilikuwa mitakatifu, nayo hii njia yetu ni ya kujiendea tu, pasipo shaka wametakata miili yao hata leo.
6Ndipo, mtambikaji alipompa ile mikate mitakatifu, kwani haikuwako mikate mingine, isipokuwa ile mikate, aliyowekewa Bwana, nayo huondolewa machoni pa Bwana, wakiweka hapo mikate mingine yenye moto; ni siku ileile, hiyo ya mbele inapochukuliwa.[#Mat. 12:3.]
7Siku ile kukawako mmoja wao watumishi wa Sauli, naye alikuwa ametengwa, akae machoni pa Bwana, jina lake Doegi wa Edomu aliyekuwa mkuu wa wachungaji wa Sauli.[#1 Sam. 22:9,18.]
8Kisha Dawidi akamwuliza Ahimeleki: Hunao mkuki au upanga? Kwani sikuchukua upanga wangu wala mata yangu mengine, kwani shauri la mfalme lilikuwa la haraka.
9Mtambikaji akamwambia: Upanga wa yule Mfilisti Goliati, uliyemwua katika Bonde la Mkwaju, uko, umezingwa na nguo, uko nyuma ya kisibau cha mtambikaji; kama unataka kuuchukua, jichukulie! Kwani hakuna mwingine, usipokuwa huo. Dawidi akasema: Hakuna mwingine wa kufanana nao, nipe, niuchukue![#1 Sam. 17:50-51.]
10Kisha Dawidi akaondoka, akamkimbia Sauli siku hiyo, akaja kwa Akisi, mfalme wa Gati.[#Sh. 56:1.]
11Watumishi wa Akisi wakamwambia: Kumbe huyu siye Dawidi, mfalme wa nchi ile? Siye yeye, waliyemwimbia na kuitikiana na kumchezea kwamba:
Sauli ameua elfu lake, lakini Dawidi ameua maelfu yake kumi?
12Dawidi alipoyafikisha maneno haya moyoni mwake, akamwogopa sana Akisi, mfalme wa Gati.
13Kwa hiyo akayageuza mawazo yake mbele yao, akawa kama mwenye wazimu huko kwao, akaipiga milango ya lango la mji kama ngoma, nayo mate yake akayachuruzisha madevuni mwake.[#Sh. 34:1.]
14Akisi akawaambia watumishi wake: Mnamwona mtu huyu kuwa mwenye kichaa, sababu gani mmemleta kwangu?
15Je? Mimi nimekosa wenye kichaa, mkimleta huyu, anitolee wazimu wake? Ananijiliaje nyumbani mwangu?