The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, Sauli aliporudi kwa kuwafuatia Wafilisti, wakampasha habari kwamba: Tazama, Dawidi yuko Engedi nyikani!
2Ndipo, Sauli alipochukua watu 3000 waliochaguliwa katika Waisiraeli wote, akaenda kumtafuta Dawidi na watu wake kwenye miamba ya minde.
3Alipofika njiani kwenye mazizi ya kondoo na mbuzi, kulikuwako pango; Sauli akaingia humo kuifunika miguu yake. Namo humo pangoni ndani Dawidi alikuwamo akikaa na watu wake.
4Watu wa Dawidi wakamwwambia: Basi, leo hivi ni siku hiyo, Bwana aliyokuambia: Utaniona mimi, nikimtia mchukivu wako mkononi mwako, umfanyizie yaliyo mema machoni pako. Dawidi akainuka, akakata pindo la kanzu yake Sauli, asivijue.[#Sh. 142:1.]
5Lakini baadaye moyo ukamkung'uta Dawidi, kwa kuwa amelikata pindo la kanzu ya Sauli;
6akawaambia watu wake: Bwana na anizuie kabisa nisimfanyizie bwana wangu, Bwana aliyempaka mafuta, jambo kama hilo la kuuinua mkono wangu, nimguse tu! Kwani Bwana alimpaka mafuta yeye.
7Kwa maneno haya Dawidi akawazuia watu wake, hakuwapa ruhusa kumwinukia Sauli. Kisha Sauli akaondoka mle pangoni, akaenda zake.[#2 Sam. 1:14; Sh. 105:15.]
8Baadaye Dawidi naye akaondoka, akatoka mle pangoni, akapaza zauti nyuma yake Sauli kwamba: Bwana wangu mfalme! Sauli alipotazama nyuma, Dawidi akamwinamia mara mbili na kumwangukia chini.
9Kisha Dawidi akamwambia Sauli: Mbona unayasikiliza maneno ya watu kwamba: Tazama, Dawidi anakutakia mabaya?
10Tazama! Leo hivi macho yako yanaweza kuona, ya kuwa Bwana amekutia mkononi mwangu mle pangoni. Lakini watu waliposema, nikuue, jicho langu likakuonea uchungu, nikasema: Sitaukunjua mkono wangu, nimguse tu bwana wangu, kwani Bwana alimpaka mafuta.
11Baba yangu, tazama, uone nawe! Pindo la kanzu yako limo mkononi mwangu! Kwani nilipolikata hili pindo la kanzu yako, sikukuua. Kwa kuliona ujue, ya kuwa mkononi mwangu hamna kibaya wala kipotovu, wala sijakukosea. Mbona wewe unaniwinda, unipate?
12Bwana na atuamue, mimi na wewe! Yeye Bwana na anilipizie kwako! Lakini mkono wangu hautakuinukia.
13Ni hivyo, kama fumbo la kale linavyosema: Kwao waovu hutoka uovu, lakini mkono wangu hautakujia.[#Rom. 12:9; 1 Petr. 2:23.]
14Mfalme wa Waisiraeli ametoka kumtafuta nani? Wewe unamkimbiza nani? Ni mbwa mfu au kiroboto kimoja tu!
15Basi, Bwana na atuhukumu na kutuamua mimi na wewe akitutazama! Kisha na anigombee huu ugomvi wangu na kuniponya mkononi mwako!
16Ikawa, Dawidi alipokwisha kumwambia Sauli maneno haya, Sauli akasema: Kumbe hii si sauti yako, mwanangu Dawidi? Kisha Sauli akapaza sauti na kulia machozi.
17Akamwambia Dawidi: Wewe u mwenye wongofu kuliko mimi, kwani wewe umenifanyizia mema mimi niliyekufanyizia mabaya.
18Wewe umeuonyesha leo huo wema, ulionifanyizia, usiponiua, Bwana aliponitoa na kunitia mkononi mwako.
19Je? Mtu akimwona mchukivu wake atamwacha, ajiendee, pasipo kumfanyizia kibaya? Bwana na akulipe na kukupatia mema kwa hayo, uliyonifanyizia leo.
20Sasa tazama! Ninajua, ya kuwa utapata kuwa mfalme, nao ufalme wa Waisiraeli utashupaa kwa nguvu za mkono wako.
21Sasa uniapie ukimtaja Bwana, ya kuwa hutawaangamiza wao wa uzao wangu watakaokuwa nyuma yangu, wala hutalitowesha jina langu katika mlango wa baba yangu.[#1 Sam. 23:17.]
22Dawidi akamwapia Sauli haya, kisha Sauli akaenda nyumbani kwake, naye Dawidi akapanda gengeni pamoja na watu wake.