1 Samweli 26

1 Samweli 26

Dawidi anaacha mara ya pili kumwua Sauli.

(Taz. 1 Sam. 24.)

1Kulikuwako Wazifu waliokuja Gibea kwa Sauli kumwambia: Je? Dawidi hajifichi katika kilima cha Hakila kinachoelekea jangwani?[#1 Sam. 23:19; Sh. 54:2.]

2Ndipo, Sauli alipoondoka, akatelemka kwenda nyikani kwa Zifu; naye alikuwa na watu 3000 waliochaguliwa katika Waisiraeli, wamtafute Dawidi katika nyika ya Zifu.

3Sauli akapiga kambi njiani kwenye kilima cha Hakila kinachoelekea jangwani, naye Dawidi alikuwa akikaa kule nyikani. Dawidi alipoona, ya kuwa Sauli anamfuata huko nyikani,

4Dawidi akatuma wapelelezi; ndivyo, alivyojua, ya kuwa Sauli amefika kweli.

5Kisha Dawidi akaondoka, akaja mahali pale, Sauli alipopiga kambi; ndipo, Dawidi alipopaona mahali pale, Sauli alipolala pamoja na mkuu wa vikosi vyake Abineri, mwana wa Neri; maana Sauli alikuwa akilala katika boma la magari, nao watu walikuwa wamelala na kumzunguka.[#1 Sam. 14:50; 17:55.]

6Ndipo, Dawidi alipopiga shauri akimwuliza Mhiti Ahimeleki na Abisai, mwana na Seruya, ndugu yake Yoabu, kwamba: Ni nani atakayeshuka pamoja nami kuingia kambini kwa Sauli? Abisai akaitikia kwamba: Mimi nitashuka pamoja na wewe.

7Ulipokuwa usiku, Dawidi na Abisai wakaingia kwenye wale watu, wakamkuta Sauli, akilala usingizi katika boma la magari, nao mkuki wake ulikuwa umechomekwa nchini kichwani pake, naye Abineri pamoja na watu wote walikuwa wamelala na kumzunguka.

8Ndipo, Abisai alipomwambia Dawidi: Leo hivi Mungu amemtoa mchukivu wako na kumtia mkononi mwako; sasa nitamchoma hapa chini kwa mara moja kwa mkuki wake, nisimchome mara ya pili.[#2 Sam. 16:9.]

9Lakini Dawidi akamwambia Abisai: Usimfanyizie kibaya! Kwani yuko nani atakayeukunjua mkono wake, amwue aliyepakwa mafuta na Bwana, pasipo kulipizwa?

10Kisha Dawidi akasema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, isifanyike! Ila Bwana atampiga, au itakuja siku yake, afe, au atakaposhuka kupiga vita ataangamia.[#1 Sam. 24:13; 28:10.]

11Hili Bwana anizuilie, nisiukunjue mkono wangu, nimwue aliyepakwa mafuta na Bwana! Sasa uchukue tu mkuki uliochomekwa kichwani pake na mtungi wa maji! Kisha twende zetu!

12Ndipo, Dawidi alipouchukua mkuki na mtungi wa maji kichwani pake Sauli, kisha wakaenda zao, Hakuna aliyewaona, wala hakuna aliyevijua, wala hakuna aliyeamka, kwani wote walikuwa wamelala, kwani Bwana aliwatia usingizi mwingi.[#1 Mose 2:21; 15:12.]

13Dawidi akaenda ng'ambo ya huko, akasimama mbali mlimani juu, pakawa mahali pakubwa katikati yao.

14Kisha Dawidi akapaza sauti kuwaita wale watu wa Abineri, mwana wa Neri, kwamba: Hujibu Abineri? Abineri akajibu akiuliza: Wewe ndiwe nani ukimwita mfalme?

15Dawidi akamwuliza Abineri: Wewe si mtu wa kiume? Kwao Waisiraeli yuko nani afananaye na wewe? Mbona humwangalii bwana wako mfalme, mtu mmoja akifika kumfanyizia mabaya bwana wako mfalme?

16Neno hili, ulilolifanya, halifai; hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, m watu wa kufa ninyi msiomwangalia bwana wenu aliyepakwa mafuta na Bwana! Sasa tazameni! Mkuki wa mfalme na mtungi wa maji uliokuwa kichwani pake uko hapa!

17Ndipo, Sauli alipoitambua sauti kuwa ya Dawidi, akasema: Kumbe hii si sauti yako, mwanangu Dawidi? Dawidi akasema: Ni sauti yangu, bwana wangu mfalme.

18Akaendelea akisema: Mbona bwana wangu anamkimbiza mtumishi wake? Nimefanya nini? Au kiko kibaya gani mkononi mwangu?

19Sasa bwana wangu mfalme na ayasikilize maneno ya mtumishi wake! Kama ni Bwana aliyekuhimiza kunijia, na asikie mnuko wa kipaji cha tambiko! Lakini kama ni watu, na wawe wameapizwa mbele ya Bwana! Kwani wamenifukuza, siku hizi nisiandamane nao walio fungu lake Bwana, wakaniambia: Jiendee kutumikia miungu mingine!

20Sasa damu yangu isimwagike chini, nikiwa ninamkalia Bwana mbali! Kwani mfalme wa Waisiraeli ametoka kutafuta kiroboto kimoja, kama watu wanavyowinda kwale milimani.

21Ndipo, Sauli aliposema: Nimekosa! Rudi, mwanangu Dawidi! Sitakufanyizia mabaya tena, kwa kuwa roho yangu imekuwa machoni pako yenye kima kikuu siku hii ya leo. Nimefanya ujinga kweli kwa kupotelewa kabisa.

22Dawidi akajibu akisema: Huu ni mkuki wa mfalme! Na aje kijana mmoja ng'ambo ya huku, auchukue!

23Naye Bwana atamlipa kila mtu yaupasayo wongofu wake na welekevu wake, maana Bwana amekutia leo mkononi mwangu, lakini nikakataa kuukunjua mkono wangu, nimwue aliyepakwa mafuta na Bwana.

24Utaona! Kama roho yako ilivyokuwa kuu machoni pangu, ndivyo, roho yangu nayo itakavyokuwa kuu machoni pa Bwana, aniponye katika masongano yote.

25Ndipo, Sauli alipomwambia Dawidi: Na ubarikiwe, mwanangu Dawidi! Utakayoyafanya utayatimiza, maana utakuwa mwenye uwezo wa kweli. Kisha Dawidi akashika njia kwenda zake, naye Sauli akarudi kwao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania