The chat will start when you send the first message.
1Siku zile Wafilisti wakavikusanya vikosi vyao kwenda vitani kupigana na Waisiraeli. Ndipo, Akisi alipomwambia Dawidi: Sharti ujue kabisa, ya kuwa huna budi kwenda pamoja nami vitani kupigana na Waisiraeli; wewe na watu wako.
2Dawidi akamwambia Akisi: Kweli na uyajue, mtumishi wako atakayoyafanya. Naye Akisi akmwambia Dawidi: Kweli nitakuweka kukiangalia kichwa changu siku zote.
3Hapo Samweli alipokufa, nao Waisiraeli wote walipomwombolezea na kumzika mjini kwake huko Rama, Sauli alikuwa amewaondoa wote waliojua kukweza mizimu pamoja na wachawi katika hiyo nchi.[#2 Mose 22:18; 1 Sam. 25:1.]
4Wafilisti walipokusanyika, kisha walipokuja kupiga makambi yao Sunemu, Sauli naye akawakusanya Waisiraeli, wakapiga makambi Gilboa.
5Sauli alipoyaona makambi ya Wafilisti akashikwa na woga, moyo wake ukastuka kabisa.
6Lakini Sauli alipomwuliza Bwana, Bwana hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu wa mtambikaji mkuu, wala kwa wafumbuaji.[#1 Sam. 14:37; 23:9; 2 Mose 28:30.]
7Kisha Sauli akawaambia watumishi wake: Nitafutieni mwaguaji wa kike, niende kwake kuulizana naye! Watumishi wake wakamwambia: Kule Endori yuko mwanamke anayejua kukweza mizimu.[#Tume. 16:16.]
8Ndipo, Sauli alipojitendekeza kuwa mwingine kwa kuvaa nguo nyingine, akachukua watu wawili wa kwenda naye; wakafika kwa yule mwanamke usiku, akamwambia: Niagulie kwa kukweza mizimu, ukinipandishia mzimu, nitakayekuambia!
9Yule mwanamke akamwambia: Tazama! Unayajua wewe, Sauli aliyoyafanya alipowatowesha watiisha mizimu pamoja na wachawi katika nchi hii; mbona unanitegea tanzi, upate kuniua?
10Sauli akamwapia na kumtaja Bwana kwamba: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, kwa jambo hili hutakora manza kabisa!
11Ndipo, yule mwanamke alipomwuliza: Nikupandishie nani? Akasema: Unipandishie Samweli!
12Yule mwanamke alipomwona Samweli akalia kwa sauti kuu, naye mwanamke akamwambia Sauli kwamba: Mbona umenidanganya? Ndiwe Sauli.
13Mfalme akamwambia: Usiogope! Sema tu: Unaona nini? Ndipo, mwanamke alipomwambia Sauli: Ninaona, wa Kimungu akipanda kutoka ndani ya nchi.
14Akamwuliza: Sura yake nini? Akasema: Yuko mtu mzee anayepanda, amevaa kanzu ya mtambikaji. Ndipo, Sauli alipotambua, ya kuwa ndiye Samweli, akamwinamia mara mbili na kumwangukia chini.
15Samweli akamwuliza Sauli: Mbona unanisumbua kwa kunipadisha? Sauli akasema: Nimesongeka sana, kwani Wafilisti wameniletea vita, naye Mungu ameondoka kwangu, hanijibu tena, wala kwa wafumbuaji, wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita, unionyeshe, nitakayoyafanya.
16Samweli akamwuliza: Mbona unaniuliza, Bwana akiwa ameondoka kwako na kugeuka kuwa mpingani wako?
17Bwana atakufanyizia, kama alivyosema kinywani mwangu: Bwana atauondoa ufalme mkononi mwako, ampe mwenzio Dawidi,
18kwa kuwa hukukitii kinywa chake Bwana, usipowafanyizia Waamaleki, makali yake yenye moto yaliyoyataka. Kwa sababu hiyo Bwana atakufanyizia jambo hili siku hii ya leo:[#1 Sam. 15:18-19.]
19Bwana atawatia wao Waisiraeli pamoja na wewe mikononi mwa Wafilisti; kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. Navyo vikosi vya Waisiraeli Bwana atawatia mikononi mwa Wafilisti.[#1 Sam. 31:6.]
20Papo hapo Sauli akaanguka chini kifudifudi, akashikwa na woga kabisa kwa ajili ya maneno ya Samweli, hata nguvu haikuwamo mwake, kwani alikuwa hakula chakula mchana kutwa na usiku kucha.
21Kisha yule mwanamke akamjia Sauli; alipoona, ya kuwa amezimia kwa woga, akamwambia: Tazama! Kijakazi wako amekiitikia kinywa chako, nikaiweka roho yangu mkononi mwako, nikayaitikia maneno yako, uliyoniambia;
22sasa wewe nawe kiitikie kinywa cha kijakazi wako, nikuandalie chakula kidogo, ule, upate nguvu ukienda zako.
23Akakataa akisema: Sitakula. Lakini watumishi wake walipomhimiza pamoja na yule mwanamke, akaviitikia vinywa vyao, akainuka hapo chini, akakaa kitandani.
24Yule mwanamke alikuwa na ndama mnono nyumbani, akamchinja upesi, akachukua nao unga, akaukanda, akaoka vikate visivyochachwa.
25Kisha akamletea Sauli na watumishi wake, wakala. Walipokwisha kula wakaondoka, wakaenda zao usiku uleule.