1 Samweli 29

1 Samweli 29

Dawidi anarudishwa na Wafilisti, aende kwao.

1Wafilisti wakavikusanya vikosi vyao vyote Afeki, nao Waisiraeli wakapiga makambi yao kwenye chemchemi iliyoko Izireeli.[#1 Sam. 4:1.]

2Wao wakuu wa Wafilisti wakafika hapo kuyapanga mamia na maelfu yao; naye Dawidi akafika na watu wake kuwapanga nyuma ya Akisi.

3Lakini wakuu wa Wafilisti wakasema: Hawa Waebureo ni wa nini? Akisi akawaambia wakuu wa Wafilisti: Huyu siye Dawidi, mtumishi wa Sauli, mfalme wa Waisiraeli? Amekuwa kwangu siku hizi nayo miaka hii, nami sikuona kwake cho chote tangu siku ile, aliponiangukia, hata siku hii ya leo.

4Lakini wakuu wa Wafilisti wakamkasirikia, nao hao wakuu wa Wafilisti wakamwambia: Mrudishe mtu huyu, akae mahali pake, ulipompatia! Asishuke pamoja nasi kupigana, asiwe mpingani wetu kwenye mapigano. Kwani liko jambo gani liwezalo kumpatia upendeleo wa bwana wake, lisipokuwa hilo la kuvitoa vichwa vya watu hawa?

5Je? Huyu Dawidi siye, waliyemwimbia na kuitikiana katika michezo kwamba:

Sauli ameua elfu lake, lakini Dawidi ameua maelfu yake kumi?

6Ndipo, Akisi alipomwita Dawidi, akamwambia: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, wewe u mtu mnyofu! Kwa hiyo ilifaa machoni pangu, utoke pamoja nami, uingie katika vita hivi pamoja nami, kwani sikuona kwako kibaya cho chote tangu siku hiyo, ulipokuja kwangu, hata siku hii ya leo; lakini machoni pao wakuu wewe hufai.

7Sasa rudi, ujiendee na kutengemana, usifanye kilicho kibaya machoni pao wakuu wa Wafilisti!

8Ndipo, Dawidi alipomwambia Akisi: Nimefanya nini? Au umeona nini kwa mtumishi wako tangu siku hiyo, nilipokutokea, hata siku hii ya leo, nisije kupiga vita nao adui wa bwana wangu mfalme?

9Akisi akamjibu na kumwambia: Ninakujua, ya kuwa wewe u mwema machoni pangu kama malaika wa Mungu; ni wao wakuu wa Wafilisti waliosema: Asipande pamoja nasi kupiga vita![#2 Sam. 19:27.]

10Sasa uamke na mapema! Nao watumishi wa bwana wako waliokuja pamoja nawe nanyi mwamke na mapema, mkipata kuona, mwende zenu!

11Kwa hiyo yeye Dawidi na watu wake wakaamka na mapema kwenda zao, warudi katika nchi ya Wafilisti, nao Wafilisti wakapanda kwenda Izireeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania