1 Samweli 3

1 Samweli 3

Bwana anamwita Samweli.

1Mtoto Samweli alipomtumikia Bwana machoni pa Eli, Neno la Bwana lilimkalia mmojammoja tu, hayakuwako maono ya wachunguzaji yaliyoenea po pote.[#Amo. 8:11.]

2Ikawa siku zile, Eli alikuwa amelala mahali pake, nayo macho yalikuwa yameanza kuguiwa na giza, asiweze kuona vema.

3Nayo taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, naye Samweli alikuwa amelala Jumbani mwa Bwana, Sanduku la Mungu lilimokuwa.

4Ndipo, Bwana alipomwita Samweli, naye akaitikia: Mimi hapa!

5Akamtokea Eli upesi, akamwambia: Mimi hapa! kwani umeniita. Akajibu: Sikukuita, rudi, ulale! Akaenda zake, akalala.

6Bwana akaita tena mara ya pili: Samweli! Samweli akaamka, akaja kwake Eli na kumwambia: Mimi hapa! kwani umeniita. Akajibu: Sikukuita, mwanangu; rudi, ulale!

7Naye Samweli alikuwa hajamjua Bwana bado, nalo Neno la Bwana halijamtokea bado.

8Bwana akaendelea kuita mara ya tatu: Samweli! Akaamka, akaenda kwake Eli na kumwambia: Mimi hapa! kwani umeniita. Ndipo, Eli alipotambua, ya kuwa ni Bwana aliyemwita mtoto.

9Kisha Eli akamwambia Samweli: Nenda, ulale! Itakapokuwa, akuite tena, itikia kwamba: Sema, Bwana! kwani mtumishi wako anasikia. Samweli akaenda, akalala mahali pake.

10Bwana akaja, akasimama, akaita, kama alivyoita mara za kwanza: Samweli! Samweli! Samweli akaitikia: Sema! kwani mtumishi wako anasikia.

11Bwana akamwambia Samweli: Utaniona, nikifanya jambo kwao Waisiraeli, nao wote watakaolisikia masikio yao yote mawili yatawavuma.

12Siku hiyo nitamtimilizia Eli yote, niliyoyasema ya mlango wake, toka mwanzo hata mwisho.

13Kwani nimempasha habari, ya kuwa nitauhukumu mlango wake kale na kale kwa ajili ya manza, walizozikora; kwani alijua, ya kuwa wanawe wanajipatia kiapizo, lakini hakuwakaripia.[#1 Sam. 2:27-36.]

14Kwa hiyo nimeuapiza mlango wa Eli kwamba: Manza, walizozikora wao wa mlango wa Eli, hazitawezekana kale na kale kupatiwa upozi, wala kwa ng'ombe ya tambiko, wala kwa kipaji cha tambiko cho chote.

15Kisha Samweli akaja kulala, mpaka kuche, kisha akaifungua milango ya Nyumba ya Bwana; lakini Samweli akaogopa kumsimulia Eli, aliyoyaona.

16Eli akamwita Samweli, akasema: Mwanagu, Samweli! Akaitikia: Mimi hapa!

17Eli akamwuliza: Ni neno gani, alilokuambia? Usinifiche kamwe! Mungu na akufanyizie hivi na hivi, ukinificha neno moja tu la hayo maneno yote, aliyokuambia.

18Ndipo, Samweli alipomsimulia hayo maneno yote, hakumficha. Akajibu: Yeye ni Bwana, na ayafanye yaliyo mema machoni pake.[#2 Sam. 15:26.]

19Samweli akakua, Bwana akiwa pamoja naye; nayo maneno yake yote hakuna hata moja, aliloliangusha chini.

20Waisiraeli wote toka Dani hata Beri-Seba wakatambua, ya kuwa Samweli amekwisha kuelekezwa kuwa mfumbuaji wa Bwana.

21Bwana akaendelea kuonekana huko Silo, kwani Bwana alimtokea Samweli huko Silo, kama Bwana alivyosema; kisha neno la Samweli likawajia Waisiraeli wote.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania