1 Samweli 4

1 Samweli 4

Waisiraeli wanashindwa na Wafilisti.

1Waisiraeli wakatoka kupigana na Wafilisti, wakapiga makambi huko Ebeni-Ezeri; nao Wafilisti wakapiga makambi Afeki.[#Yos. 15:53.]

2Kisha Wafilisti wakajipanga kuwaelekea Waisiraeli; mapigano yalipoenea pakubwa, Waisiraeli wakapigwa na Wafilisti, hao wakaua watu kama 4000 papo hapo porini, walipojipanga kupigana.

3Watu walipokuja kuingia makambini, wazee wa Waisiraeli wakasema: Sababu gani Bwana ametupiga leo machoni pao Wafilisti? Na tulichukue huko Silo Sanduku la Agano la Bwana, lije lituokoe mikononi mwa adui zetu.[#1 Sam. 14:18.]

4Ndipo, watu walipotuma Silo, wakalichukua huko Sanduku la Agano la Bwana Mwenye vikosi akaaye juu ya Makerubi; nao wale wana wawili wa Eli, Hofuni na Pinehasi, wakatoka huko wakilisimamia Sanduku la Agano la Mungu.[#2 Sam. 6:2.]

5Ikawa, Sanduku la Agano la Bwana lilipoingia makambini, Waisiraeli wote wakapaza sauti sana na kupiga yowe, hata nchi ikatutuma.

6Wafilisti walipozisikia sauti zao za yowe wakaulizana: Sauti hizi kuu za yowe makambini mwa Waebureo ni za nini? Wakatambua, ya kuwa Sanduku la Bwana limeingia makambini.

7Wafilisti wakashikwa na woga, kwani walisema: Mungu ameingia makambini! Yametupata sasa! Kwani jambo kama hilo halijafanyika zamani zote.

8Yametupata sasa! Yuko nani atakayetuponya mkononi mwake Mungu huyu mwenye nguvu? Huyu ni Mungu yule aliyewapiga Wamisri mapigo yote nyikani.

9Lakini ninyi Wafilisti jipeni mioyo, mwe waume, msije kuwatumikia Waebureo, kama wao wanavyowatumikia ninyi. Mwe waume, mje kupigana nao![#Amu. 13:1.]

10Basi, Wafilisti walipopigana nao, Waisiraeli wakapigwa, wakakimbilia kwao kila mtu hemani kwake; likawa pigo kubwa sana, kwao Waisiraeli wakauawa 30000 waliokwenda kwa miguu.

11Hata Sanduku la Mungu likatekwa, nao wale wana wawili wa Eli, Hofuni na Pinehasi, wakafa.

Kufa kwake Eli.

12Mtu wa Benyamini akatoka hapo, walipojipanga kupigana, akapiga mbio kufika Silo siku ileile; nguo zake zilikuwa zimerarukararuka, napo juu kichwani pake palikuwa na mavumbi.

13Alipofika akamwona Eli, akikaa langoni katika kiti chake cha ukuu kando ya njia na kuchungulia njiani, kwani moyo wake ulikuwa umehangaika kwa ajili ya Sanduku la Mungu. Yule mtu alipoingia mjini kupasha habari, watu wote wa mjini wakalia.

14Eli alipozisikia sauti za kilio akauliza: Sauti hizi za huo mtutumo ni za nini? Ndipo, yule mtu alipopiga mbio kufika kwake na kumpasha Eli hizo habari.

15Naye Eli alikuwa mwenye miaka 98, macho yake yalikuwa yametenda kiwi, asiweze kuona.[#1 Sam. 3:2.]

16Yule mtu akamwambia Eli: Mimi nimetoka hapo, walipojipanga kupigana; nami nimekimbia leo hivi kutoka hapo, walipojipanga kupigana. Akauliza: Mambo ya huko yako namna gani, mwanangu?

17Mwenye kuleta habari akajibu na kusema: Waisiraeli wamekimbizwa na Wafilisti, likawa pigo kubwa sana kwao, nao wanao wawili, Hofuni na Pinehasi, wamekufa, hata Sanduku la Mungu limetekwa.

18Ikawa, alipolitaja Sanduku la Mungu, ndipo, Eli alipoanguka chali hapo kitini kando ya lango, shingo lake likavunjika, akafa, kwani alikuwa mzee na mtu mnene sana. Nayo miaka, aliyokuwa mwamuzi wa Waisiraeli, ilikuwa 40.

19Mkwewe, mkewe Pinehasi, alikuwa mwenye mimba iliyokomaa; alipopashwa hizo habari za kutekwa kwake Sanduku la Mungu nazo za kufa kwake mkwewe na mumewe, akaanguka magotini, akazaa, kwani alishikwa na uchungu wake wa kuzaa.

20Hapo, alipotaka kufa, wanawake waliomsimamia wakamwambia: Usiogope! Kwani umezaa mtoto wa kiume; lakini hakujibu neno, wala hakusikiliza.[#1 Mose 35:17.]

21Lakini mtoto akamwita jina lake Ikabodi ni kwamba: Utukufu umeondoka kwao Waisiraeli, kwa kuwa Sanduku la Mungu lilikuwa limetekwa, nao mkwewe na mumewe walikuwa wamekufa.[#Sh. 78:61.]

22Akasema: Utukufu umeondoka kwao Waisiraeli, kwani Sanduku la Mungu limetekwa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania