The chat will start when you send the first message.
1Wafilisti wakalichukua Sanduku la Mungu, wakalitoa Ebeni-Ezeri, wakalipeleka Asdodi.[#Amu. 16:23.]
2Wafilisti walipolichukua Sanduku la Mungu wakaliingiza nyumbani mwa Dagoni, wakaliweka kando yake Dagoni.
3Kesho yake watu wa Asdodi walipoamka asubuhi wakamkuta Dagoni, akilala usoni chini mbele ya Sanduku la Bwana; wakamchukua Dagoni, wakamrudisha mahali pake.
4Kesho yake walipoamka asubuhi wakamkuta Dagoni tena, akilala usoni chini mbele ya Sanduku la Bwana, nacho kichwa cha Dagoni na viganja vyote viwili vya mikono yake vilikuwa vimekatika, vilikuwa penye kizingiti, nao mwili ulikuwa umesalia peke yake.
5Kwa hiyo watambikaji wa Dagoni nao wote wanaoingia nyumbani mwa Dagoni hawakikanyagi kizingiti cha Dagoni huko Asdodi mpaka siku hii ya leo.
6Mkono wa Bwana ukawalemea watu wa Asdodi, akawaangamiza na kuwapiga kwa majipu mabaya waliokuwamo Asdodi namo katika mipaka yake.[#Sh. 78:66.]
7Watu wa Asdodi walipoyaona mambo hayo kuwa hivyo wakasema: Sanduku la Mungu wa Waisiraeli halitakaa tena kwetu, kwani mkono wake umetulemea sisi na mungu wetu Dagoni.
8Wakatuma, wakawakusanya wakuu wote wa Wafilisti kwao, wakauliza: Tulifanyie nini Sanduku la Mungu wa Waisiraeli? Wakasema: Sanduku la Mungu wa Waisiraeli na lihamishwe Gati! Wakalihamisha Sanduku la Mungu wa Waisiraeli.
9Ikawa, walipokwisha kulihamisha, ndipo, mkono wa Bwana ulipoustusha mji huo, likawa stusho kubwa sana, akiwapiga watu wa mji huo, wakubwa kwa wadogo, wakatoka majipu mabaya.
10Ndipo, walipolipeleka Sanduku la Mungu Ekroni; ikawa, Sanduku la Mungu lilipoingia Ekroni, watu wa Ekroni wakalia kwamba: Sanduku la Mungu wa Waisiraeli wamelihamisha kwetu, wawaue watu wa kwetu.
11Ndipo, walipotuma, wakawakusanya wakuu wote wa Wafilisti, wakasema: Lipelekeni Sanduku la Mungu wa Waisiraeli, lirudi mahali pake, lisituue sisi na watu wa kwetu! Kwani katika mji wote mzima walishikwa na kistusho cha kifo, kwani mkono wa Mungu uliwalemea sana huko.
12Nao watu wasiokufa wakapigwa kwa majipu mabaya, vilio vya humo mjini vikafika mbinguni juu.