1 Samweli 7

1 Samweli 7

Kwa majuto yao Waisiraeli wanawashinda Wafilisti huko Ebeni-Ezeri.

1Watu wa Kiriati-Yearimu wakaja, wakalichukua Sanduku la Bwana kwao, wakaliingiza nyumbani mwa Abinadabu kilimani juu, naye mwanawe Elazari wakamweua, aliangalie Sanduku la Bwana.

2Tangu siku hiyo, Sanduku la Bwana lilipokuja kukaa Kiriati-Yearimu, siku zikapita nyingi, zikawa miaka 20. Kisha mlango wote wa Waisiraeli wakageuka kumfuata Bwana na kumlilia.[#1 Mambo 13:6.]

3Ndipo, Samweli alipouambia mlango wote wa Waisiraeli kwamba: Ninyi mkimgeukia Bwana kwa mioyo yote, iondoeni miungu migeni kwenu pamoja na Maastaroti! Kisha ielekezeni mioyo yenu kwake Bwana na kumtumikia yeye peke yake! Ndivyo, atakavyowaponya mikononi mwa wafilisti.[#1 Mose 35:2; Yos. 24:23.]

4Ndipo, wana wa Isiraeli walipoyaondoa Mabaali na Maastaroti, wakamtumikia Bwana peke yake.[#Amu. 10:6,16.]

5Kisha Samweli akasema: Wakusanyeni Waisiraeli wote Misipa, niwaombee kwake Bwana![#1 Sam. 10:17; Amu. 11:11; 20:1.]

6Wakakusanyika Misipa, wakachota maji, wakayamwaga mbele ya Bwana na kufunga mfungo siku hiyo na kusema huko: Tumemkosea Bwana! Kisha Samweli akawakatia wana wa Isiraeli mashauri huko Misipa.

7Wafilisti waliposikia, ya kuwa wana wa Isiraeli wamekusanyika Misipa, wakuu wa Wafilisti wakawapandia Waisiraeli; nao Waisiraeli walipovisikia, wakawaogopa Wafilisti.

8Ndipo, wana wa Isiraeli walipomwambia Samweli: Usikome kumlilia Bwana Mungu wetu kwa ajili yetu, atuokoe mikononi mwa Wafilisti![#1 Sam. 12:23.]

9Samweli akachukua mwana kondoo mwenye kunyonya, akamatolea Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima; samweli alipomlilia Bwana hivyo kwa ajili ya Waisiraeli, Bwana akamwitikia.

10Ikawa, Samweli alipoiteketeza hiyo ng'ombe ya tambiko, Wafilisti wakafika kupigana nao Waisiraeli. Papo hapo Bwana akanguruma kwa sauti kubwa sana juu ya Wafilisti; ndivyo, alivyowastusha sana, kwa hiyo wakapigwa mbele yao Waisiraeli.

11Kisha waume wa Waisiraeli wakatoka Misipa, wakawakimbiza na kuwapiga hata chini ya Beti-Kari.

12Ndipo, Samweli alipotwaa jiwe moja, akalisimika katikati ya Misipa na Seni, akaliita jina lake Ebeni-Ezeri (Jiwe la Msaada) akisema: Bwana ametusaidia mpaka hapa.

13Ndivyo, Wafilisti walivyonyenyekezwa, hawakurudi tena kuingia katika mipaka ya Waisiraeli, nao mkono wa Bwana ukawapinga Wafilisti siku zote za Samweli.

14Nayo miji, Wafilisti waliyoichukua kwa Waisiraeli, ikarudi tena kuwa yao Waisiraeli toka Ekroni hata Gati, nazo nchi zao Waisiraeli wakaziponya mikononi mwa Wafilisti. Tena Waisiraeli na Waamori walikuwa wakipatana.

15Naye Samweli akawa mwamuzi wa Waisiraeli siku zote za maisha yake.

16Mwaka kwa mwaka akaenda kuzunguka Beteli na Gilgali na Misipa, akikata mashauri yao Waisiraeli mahali hapo pote.

17Kisha hurudi Rama, kwani ndiko, nyumba yake ilikokuwa, tena ndiko, alikowaamulia Waisiraeli. Kisha akajenga huko pa kumtambikia Bwana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania