The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, Samweli alipokuwa mzee, akawaweka wanawe wawili kuwa waamuzi wa Waisiraeli.[#1 Mambo 6:28.]
2Jina la mwanawe wa kwanza ni Yoeli, nalo lake wa pili ni Abia, nao walikaa Beri-Seba, walipokuwa waamuzi.
3Lakini wanawe hawakuendelea na kuzishika njia zake, maana waligeukia kutafuta mali, kwa hiyo wakachukua fedha za kupenyezewa, wakayapotoa mashauri.[#5 Mose 16:19.]
4Ndipo, wazee wote wa Waisiraeli walipokusanyika, wakaja Rama kwa Samweli,[#1 Sam. 7:17.]
5wakamwambia: Tazama! Wewe umekwisha kuwa mzee, nao wanao hawaendelei na kuzishika njia zako, sasa tuwekee mfalme wa kutuamulia, kama mataifa yote yanavyoamuliwa![#5 Mose 17:14; Hos. 13:10; Tume. 13:21.]
6Neno hili likawa baya machoni pake Samweli, kwa kuwa wamesema: Tupe mfalme wa kutuamulia! Kwa hiyo Samweli akamwomba Bwana.
7Bwana akamwambia Samweli: Viitikie vinywa vyao watu hawa ukiyafanya yote, waliyokuambia! Kwani hawakukatai wewe, ila ni mimi, waliyenikataa kuwa mfalme wao.
8Ndivyo, matendo yao yote yalivyo, waliyoyatenda tangu siku ile, nilipowatoa Misri, mpaka siku hii ya leo wakiniacha na kutumikia miungu mingine. Hivi ndivyo, wanavyokufanyia hata wewe.
9Sasa viitikie vinywa vyao! Lakini sharti uwashuhudie vema na kuieleza haki yake mfalme atakayewatawala.
10Kisha Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme haya maneno yote ya Bwana
11akisema: Hii ndiyo haki yake mfalme atakayewatawala: atawachukua wana wenu wa kiume, awaweke katika magari yake wa kuyaendesha, wengine atawapandisha farasi, wengine atawaweka kuyatangulia magari yake kwa kupiga mbio.
12Wengine atawaweka kuwa wakuu wa maelfu na wakuu wa hamsini tu; wengine atawaweka kuyalima mashamba yake na kuyavuna mavuno yake na kuyatengeneza mata ya vita vyake na vyombo vya magari yake.
13Nao wana wenu wa kike atawachukua, wawe watengeneza manukato na wapishi na waoka mikate.
14Nayo mashamba na mizabibu na michekele yenu iliyo mizuri zaidi ataichukua na kuwapa watumishi wake.
15Tena mbegu zenu na mizabibu yenu atatoza mafungu ya kumi, awape watumishi wake wa nyumbani na watumishi wake wengine.
16Nao watumishi wenu wa kiume na wa kike na vijana wenu walio wazuri zaidi na punda wenu atachukua, awatumie katika kazi zake.
17Mbuzi na kondoo wenu atatoza mafungu ya kumi, nanyi sharti mmtumikie kitumwa.
18Tena siku hiyo, mtakapolia kwa ajili ya mfalme wenu, mliyejichagulia, siku hiyo Bwana hatawajibu.
19Lakini watu wakakataa kukiitikia kinywa cha Samweli, wakasema: Haidhuru, sharti tuwe na mfalme wa kututawala!
20Nasi tunataka kuwa kama mataifa yote, mfalme wetu atukatie mashauri yetu, tena atutangulie, avipige vita vyetu.
21Samweli alipokwisha kuyasikia maneno yote ya watu, akaja kuyasema masikioni mwa Bwana.
22Bwana akamwambia Samweli: Viitikie vinywa vyao na kuwapatia mfalme! Ndipo, Samweli alipowaambia waume wa Waisiraeli: Nendeni zenu kila mtu mjini kwake![#1 Sam. 8:7-9.]