2 Wakorinto 2

2 Wakorinto 2

Mkosaji aliyejuta aachiliwe.

1Lakini moyoni naliwaza hivi: Nisije tena kwenu mwenye sikitiko![#1 Kor. 12:21; 1 Kor. 4:21.]

2Kwani mimi nikiwasikitisha ninyi, yuko nani atakayenichangamsha, asipokuwa yule aliyesikitishwa nami?

3Kwa sababu hii naliyaandika yale ya kwamba: Nitakapokuja nisisikitishwe nanyi mliopaswa na kunifurahisha; kwa maana ninyi nyote mmenipa moyo wa kwamba: Furaha yangu ni furaha yenu nyote.[#1 Kor. 5.]

4Kwani naliwaandikia kwa maumivu mengi, moyo ukanipotelea, vikanitoa machozi mengi, siko kwamba msikitishwe, ila mpate kuutambua upendo unaonikaza kuwapenda ninyi kuliko wengine.

5Lakini kama yuko aliyesikitisha, hakunisikitisha mimi; ila fungufungu, maana nisiseme na kuyapita ya kweli, amewasikitisha ninyi nyote.[#1 Kor. 5:1.]

6Aliye hivyo inamtosha, akionywa hivyo na wenzake walio wengi.

7Kisha imewapasa ninyi kumwendea kwa upole na kumtuliza moyo, asididimizwe, masikitiko yakimshinda.

8Kwa hiyo nawabembeleza ninyi, mmwonyeshe, ya kuwa mwampenda.

9Kwani kwa hiyo naliwaandikia, nipate kuutambua welekevu wenu, kama mnatii katika mambo yote.[#2 Kor. 7:15.]

10Lakini mmwachiliaye neno, hata mimi humwachilia. Kwamba hata mimi, ikiwa nimemwachilia mtu neno, nimemwachilia kwa ajili yenu machoni pa Kristo,[#Mat. 18:18; Luk. 10:16.]

11maana tusidanganywe na Satani; kwani mizungu yake hatukosi kuijua.[#Luk. 22:31; 1 Petr. 5:8.]

Manukato yenye kufa nayo yenye uzima.

12Hapo, nilipofika Tiroa kuutangaza Utume mwema wa Kristo, nikafunguliwa mlango kwa nguvu ya Bwana;[#Tume. 14:27; 1 Kor. 16:9; Kol. 4:9.]

13lakini sikuona utulivu moyoni mwangu, kwa kuwa sikumkuta ndugu yangu Tito; kwa hiyo nikaagana nao, nikatoka kwenda Makedonia.[#Tume. 20:1.]

14Lakini Mungu atukuzwe anayetupa kushinda siku zote, tukiwa katika Kristo! Kwa hivyo, tunavyomtumikia yeye, hutokeza po pote waziwazi, ya kuwa wenye kumtambua wafanana na maua yanukayo vizuri.

15Kwani tukawa mbele yake Mungu kama manukato mazuri ya Kristo kwao wanaookoka, nako kwao wanaoangamia:[#1 Kor. 1:18.]

16hao tunawanukia kama wenye kutoka kufani wanaorudi kufani, lakini wale tunawanukia kama wenye kutoka uzimani wanaorudi uzimani. Yuko nani atakayeyaweza hayo.[#2 Kor. 3:5-6; Luk. 2:34.]

17Kwani sisi hatufanani nao wale wengi wanaolichuuzia Neno la Mungu, ila kwa ung'avu wa mioyo, tulioupata kwa Mungu, tunasema kama watu walio pamoja na Kristo mbele yake Mungu.[#2 Kor. 1:12.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania