2 Wafalme 17

2 Wafalme 17

Ufalme wa Waisiraeli: Hosea, mfalme wa mwisho. Uhamisho wa Asuri.

1Katika mwaka wa 12 wa Ahazi, mfalme wa Wayuda, Hosea, mwana wa Ela, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 9.[#2 Fal. 15:30.]

2Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, lakini hakuzidi kama wafalme waliokuwa mbele yake.

3Yeye ndiye, Salmaneseri, mfalme wa Asuri, aliyemjia, naye Hosea, hakuwa na budi kumtumikia na kumtolea mahongo.[#2 Fal. 18:9-12.]

4Kisha mfalme wa Asuri akamwona Hosea kuwa mwenye njama mbaya, kwa kuwa alituma wajumbe kwa So, mfalme wa Misri, akaacha kumpelekea mfalme wa Asuri mahongo, aliyoyapeleka mwaka kwa mwaka; ndipo, mfalme wa Asuri alipomfunga na kumtia kifungoni.[#Hos. 12:2.]

5Kisha mfalme wa Asuri akaipandia hiyo nchi yote akiupandia mji wa Samaria, akausonga kwa kuuzinga miaka mitatu.

6Katika mwaka wa tisa wa Hosea mfalme wa Asuri akauteka mji wa Samaria, akawahamisha Waisiraeli kwenda Asuri, akawakalisha katika miji ya Hala, tena Habori penye mto wa Gozani na katika miji ya Wamedi.

Makosa ya Waisiraeli yaliyowatenga na Mungu.

7Ikawa hivyo, kwa kuwa wana wa Isiraeli walimkosea Bwana Mungu wao aliyewatoa utumwani katika nchi ya Misri mkononi mwa Farao, mfalme wa Misri, lakini wao wakacha miungu mingine.

8Wakaendelea na kuyafuata maongozi ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Isiraeli, nayo maongozi, wafalme wa Waisiraeli waliyoyatoa.[#2 Fal. 16:3.]

9Hivyo wana wa Isiraeli walimkosea Bwana Mungu wao na kufanya mafichoni mambo yasiyopasa kuyafanya, wakijijengea pa kutambikia vilimani katika miji yao yote iliyokuwa yenye minara tu ya kungojea, namo mijini mlimo na maboma.

10Wakajisimamishia nguzo za kutambikia na miti ya Ashera katika vilima virefu vyote na chini ya kila mti wenye majani mengi,[#1 Fal. 14:23; 2 Fal. 16:4.]

11wakavukiza vilimani po pote pa kutambikia kama wamizimu, Bwana aliowaondoa mbele yao. Kweli walifanya mambo mabaya ya kumkasirisha Bwana,[#2 Fal. 17:8.]

12wakiitumikia migogo ya kutambikia, naye Bwana alikuwa amewakataza kwamba: Msilifanye jambo hilo![#2 Mose 20:2-3; 23:13.]

13Tena Bwana aliwashuhudia Waisiraeli na Wayuda vinywani mwa wafumbuaji wote na wachunguzaji wote kwamba: Rudini na kuziacha njia zenu mbaya, myaangalie maagizo yangu na maongozi yangu na kuyafuata Maonyo yote, niliyowaagiza baba zenu, niliyoyatuma kwenu vinywani mwa watumishi wangu waliokuwa wafumbuaji.

14Lakini hawakusikia, ila walizishupaza kosi zao kuwa kama kosi za baba zao wasiomtegemea Bwana Mungu wao.

15Wakayakataa maongozi yake na Agano lake, aliloliagana na baba zao, nao ushuhuda wake, aliowashuhudia, wakafuata mambo yasiyo na maana wakifanya yaliyo ya bure kabisa, wakawafuata wamizimu waliokaa na kuwazunguka pande zote, naye Bwana alikuwa amewaagiza, wasifanye kama wao.[#2 Mose 23:24.]

16Wakayaacha maagizo yote ya Bwana Mungu wao, wakajitengenezea vinyago viwili vya ndama kwa shaba zilizoyeyushwa, tena wakajitengenezea vinyago vya Ashera, wakaviangukia navyo vikosi vyote vya mbinguni, wakamtumikia hata Baali.[#1 Fal. 12:28; 16:33.]

17Hata wana wao wa kiume na wa kike wakawatumia kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa motoni, wakaagua maaguaji kwa kutabana, wakajiuza katika utumwa wa kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, wamkasirishe.[#2 Fal. 16:3.]

18Ndipo, Bwana alipowachafukia sana Waisiraeli, akawaondoa usoni pake, hakusalia mtu, ila shina la Wayuda peke yake.

19Lakini Wayuda nao hawakuyaangalia maagizo ya Bwana, nao wakaendelea kuyafuata maongozi, Waisiraeli waliyoyatoa.

20Ndipo, Bwana alipokikataa kizazi chote cha Isiraeli, akawatesa na kuwatia mikononi mwa wanyang'anyi, mpaka akiwatupa, waondoke kabisa usoni pake.

21Kwani Waisiraeli walipojitenga nao wa mlango wa Dawidi na kumfanya Yeroboamu, mwana wa Nebati, kuwa mfalme wao, Yeroboamu akawahimiza Waisiraeli, wasimfuate Bwana, akawakosesha kosa kubwa mno.[#1 Fal. 12:20.]

22Wana wa Isiraeli wakaendelea kuyafanya makosa yote, Yeroboamu aliyoyafanya, hawakuyaepuka,

23mpaka Bwana akiwaondoa Waisiraeli usoni pake, kama alivyosema vinywani mwa watumishi wake wafumbuaji, akawatoa Waisiraeli katika nchi yao na kuwahamisha kwenda Asuri mpaka siku hii ya leo.[#5 Mose 28:63-64.]

Kabila la Wasamaria linatokea.

24Kisha mfalme wa Asuri akatoa watu mle Babeli na Kuta na Awa na Hamati na Sefarwaimu, akawakalisha katika miji ya Samaria mahali pao wana wa Isiraeli, wakaitwaa nchi ya Samaria, iwe yao, wakakaa katika miji yao.

25Ikawa, walipoanza kukaa huko, hawakumcha Bwana, naye Bwana akatuma simba kwao, wakaua watu wengine wengine.

26Ndipo, walipotuma kumwambia mfalme wa Asuri kwamba: Wamizimu, uliowahamisha na kuwakalisha katika miji ya Samaria, hawayajui yampasayo Mungu wa nchi hii, kwa sababu hii ametuma simba kwao, nao wakawaua, kwa kuwa hawajui yampasayo Mungu wa nchi hii.

27Mfalme wa Asuri akaagiza kwamba: Pelekeni huko mmoja wao watambikaji, mliowatoa huko na kuwahamisha! Na aende, akae huko na kuwafundisha yampasayo Mungu wa nchi hiyo.

28Ndipo, mmoja wao watambikaji, waliowatoa Samaria na kuwahamisha, alipokuja, akakaa Beteli, akawa akiwafundisha njia za kumcha Bwana.

29Lakini kila kabila moja wakajitengenezea miungu ya kwao, wakaiweka katika zile nyumba, Waisiraeli walizozijenga vilimani za kutambikia mle; kila kabila moja wakafanya hivyo katika miji yao, walimokaa.

30Watu wa Babeli wakatengeneza vinyago vya Sukoti-Benoti, watu wa Kuta wakatengeneza vinyago vya Nergali, watu wa Hamati wakatengeneza vinyago vya Asima,

31watu wa Awa wakatengeneza vinyago vya Nibuhazi na vya Tarkati, nao wa Sefarwaimu wakawateketeza wana wao motoni, wawe ng'ombe za tambiko za Adarameleki na za Anameleki, ndiyo miungu yao wa Sefarwaimu.[#2 Fal. 17:17.]

32Basi, hivyo walikuwa wakimcha Bwana, lakini wakajipatia miongoni mwao watambikaji wa vilimani, ndio waliowafanyia kazi za kutambika katika nyumba za vilimani.

33Hivyo walikuwa wenye kumcha Bwana pamoja na kuitumikia miungu ya kwao, kama ilivyowapasa wamizimu wa kwao, walikotolewa na kuhamishwa kuja huku.

34Hata siku hii ya leo hufanya, kama hizo desturi zao za kwanza zilivyokuwa: hawamchi Bwana kwa kweli, wala hawafanyi kwa kweli, maongozi yao na desturi zao zilivyo, wala hawaishiki njia ya Maonyo na ya maagizo, Bwana aliyowaagiza wana wa Yakobo, aliyempa jina la Isiraeli.

35Naye Bwana alikuwa amefanya agano nao na kuwaagiza kwamba: Msiche miungu mingine, wala msiiangukie, wala msiitumikie, wala msiitambikie![#2 Mose 23:24.]

36Ila Bwana aliyewatoa katika nchi ya Misri kwa nguvu kuu za mkono wake, alioukunjua, yeye sharti mmche, mmwangukie na kumtambikia!

37Nayo maongozi na maamuzi na Maonyo na maagizo, aliyowaandikia ninyi, sharti myaangalie, myafanye siku zote! Msiche kabisa miungu mingine!

38Wala msilisahau Agano, nililolifanya nanyi, wala msiche miungu mingine![#5 Mose 6:12-19.]

39Ila Bwana Mungu wenu sharti mmche! Naye atawaponya mikononi mwa adui zenu wote.

40Lakini hawakusikia, ila wao wakafanya, kama hizo desturi zao za kwanza zilivyokuwa.

41Hivyo ndivyo, hao wamizimu walivyomcha Bwana pamoja na kuvitumikia vinyago vyao. Hata wana wao na wana wa wana wao wakayafanya mpaka siku hii ya leo, kama baba zao walivyoyafanya.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania