2 Wafalme 2

2 Wafalme 2

Elia anapazwa mbinguni.

1Bwana alipotaka kumpaza Elia mbinguni kwa nguvu za upepo wenye ngurumo, Elia na Elisa walikuwa wakienda njiani kutoka Gilgali.

2Elia akamwambia Elisa: Kaa hapa! Kwani Bwana amenituma kwenda Beteli. Elisa akajibu: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena hivyo, wewe mwenyewe ulivyo mzima, sitakuacha kabisa. Wakatelemka kwenda Beteli.

3Ndipo, wanafunzi wa wafumbuaji waliomo Beteli walipomtokea Elisa, wakamwambia: Unajua, ya kuwa leo Bwana atamwondoa bwana wako kichwani pako? Akasema: Nami nayajua, nyamazeni tu!

4Elia akamwambia: Elisa, kaa hapa! Kwani Bwana amenituma kwenda Yeriko. Akajibu: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena hivyo, wewe mwenyewe ulivyo mzima, sitakuacha kabisa. Wakaja Yeriko.

5Ndipo, wanafunzi wa wafumbuaji waliomo Yeriko walipomjia Elisa, wakamwambia: Unajua, ya kuwa leo Bwana atamwondoa bwana wako kichwani pako? Akasema: Nami nayajua, nyamazeni tu!

6Elia akamwambia: Kaa hapa! Kwani Bwana amenituma kwenda Yordani. Akajibu: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena hivyo, wewe mwenyewe ulivyo mzima, sitakuacha kabisa. Wakaenda wote wawili.

7Watu hamsini waliokuwa wanafunzi wa wafumbuaji wakaja, wakasimama mbali ng'ambo ya huku, wao wawili waliposimama Yordani.

8Ndipo, Elia alipolishika joho lake, akalizinga, akalipigisha maji; ndipo, yalipogawanyika huku na huko, nao wote wawili wakapita pakavu.[#2 Mose 14:21-22; Yos. 3:16.]

9Walipokwisha pita, Elia akamwambia Elisa: Omba unayoyataka, nikufanyizie, nikiwa sijaondolewa kwako! Elisa akasema: Ninataka, mafungu mawili ya roho yako yaje kunikalia.[#5 Mose 21:17.]

10Elia akajibu: Umeomba neno gumu. Utakaponiona, nikiondolewa kwako, na ulipate! Usipoviona, hutalipata.

11Ikawa, wangaliko njiani na kusema, mara gari la moto likatokea pamoja na farasi wa moto, likawatenga wale wawili. Ndivyo, Elia alivyopaa mbinguni kwa nguvu za upepo wenye ngurumo.[#1 Mose 5:24.]

12Elisa alipoviona akalia kwamba: Baba yangu! Baba yangu! Wewe gari la Waisiraeli na wapanda farasi wake! Lakini hakumwona tena; kisha akazishika nguo zake, akazirarua, zitoke vipande viwili.[#2 Fal. 13:14.]

Roho na nguvu za Elia zinamkalia Elisa.

13Kisha akaliokota joho lake Elia lililokuwa limeanguka, akarudi, akasimama kando ya mto wa Yordani.[#2 Fal. 2:8.]

14Akalishika hilo joho la Elia lililokuwa limeanguka, akalipigisha maji akisema: Bwana Mungu wa Elia yuko wapi? Basi; hapo, yeye naye alipoyapiga maji, mara maji yakagawanyika huku na huko, naye Elisa akapita.

15Wanafunzi wa wafumbuaji waliokuwako Yeriko ng'ambo ya huku walipomwona wakasema: Roho yake Elia inamkalia Elisa. Wakamwendea, wakamwangukia chini.[#2 Fal. 2:5,7; Luk. 1:17.]

16Wakamwambia: Tazama, huku wako watu hamsini wenye nguvu; acha, tuwatume, waende kumtafuta bwana wako! Labda roho ya Bwana imemchukua, ikamweka juu ya mlima mmoja au katika bonde moja. Akawaambia: Msiwatume!

17Walipomhimiza sana, mpaka akilegea, akasema: watumeni! Ndipo, walipowatuma wale watu hamsini, wakamtafuta siku tatu, lakini hawakumwona.

18Waliporudi kwake, yeye alikuwa angaliko Yeriko, akawaambia: Sikuwaambia, msiende?

19Kisha watu wa huo mji wakamwambia Elisa: Tazama, hapa, mji huu unapokaa, ni pema, kama wewe bwana unavyoona, lakini maji ni mabaya, kwa hiyo nchi hii hupoozesha mimba, ziharibike.

20Akasema: Nileteeni bakuli jipya, kisha tieni chumvi humo! Walipomletea,

21akaenda nje kufika hapo, maji yalipotokea, akaitupa ile chumvi papo hapo akisema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nimeyapatia maji haya uzima, hayataua tena, wala hayatapoozesha tena mimba.

22Ndipo, yale maji yalipopona hata siku hii ya leo, kama Elisa alivyosema.

23Toka huko akapanda kwenda Beteli; alipokuwa akipanda njiani, watoto wakatoka mjini, wakamfyoza wakimwambia: Panda, Chakipara! Panda, Chakipara!

24Alipogeuka nyuma akawaona, akawaapiza katika Jina la Bwana. Ndipo, chui wawili walipotoka mwituni, wakararua kwao watoto 42.

25Kisha akatoka huko kwenda mlimani kwa Karmeli, toka huko akarudi Samaria.[#2 Fal. 4:25.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania