2 Wafalme 25

2 Wafalme 25

Yerusalemu unatekwa, watu wanahamishwa kwenda Babeli.

(1-21: Yer. 52:4-27; 39:1-10; 2 Mambo 36:17-20.)

1Ikawa katika mwaka wa 9 wa ufalme wake katika mwezi wa kumi siku ya kumi ya mwezi, ndipo, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alipoujia Yerusalemu yeye na vikosi vyake vyote, wakapiga makambi huko, wakaujengea boma la kuuzungusha.

2Mji ukaja kusongwa hivyo na kuzingwa mpaka mwaka wa 11 wa mfalme Sedekia.

3Siku ya tisa ya mwezi wa nne njaa ikazidi mle mjini, watu wa nchi hii hawakuwa na vyakula.

4Ndipo, mji ulipobomolewa, nao wapiga vita wote wakatoroka usiku huo kwa njia ya lango lililokuwa kati ya kuta mbili penye bustani ya mfalme, nao Wakasidi walikuwa wamelala na kuuzunguka mji, wale wakishika njia ya nyikani.

5Kisha vikosi vya Wakasidi vikamfuata mfalme na kupiga mbio, vikampata katika nyika ya Yeriko, navyo vikosi vyake vyote vilikuwa vimetawanyika na kumwacha.

6Wakamkamata mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribula, wakasema naye na kumhukumu.

7Wanawe Sedekia wakawaua machoni pake, kisha wakayapofua macho yake Sedekia, wakamfunga kwa minyororo, wakampeleka Babeli.

8Katika mwezi wa tano siku ya saba ya mwezi-ulikuwa mwaka wa 19 wa mfalme Nebukadinesari, mfalme wa Babeli-ndipo, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, mtumishi wa mfalme wa Babeli, alipoingia Yerusalemu.

9Akaiteketeza Nyumba ya Bwana na nyumba ya mfalme, nazo nyumba zote za Yerusalemu, nazo nyumba kubwa zote akaziteketeza kwa moto.

10Kisha vikosi vyote vya Wakasidi waliokuwa na mkuu wao waliomlinda mfalme vikazibomoa kuta za boma lililouzunguka Yerusalemu.

11Masao ya watu waliosalia mjini nao waliokuwa wamemwangukia mfalme wa Babeli na kurudi upande wake, hayo masao yote ya mtutumo wa watu Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawateka na kuwahamisha.

12Lakini wanyonge wa nchi hii mkuu wao waliomlinda mfalme akawasaza, wengine waiangalie mizabibu, wengine walime tu.

13Lakini zile nguzo mbili za shaba zilizokuwa penye Nyumba ya Bwana na vile vilingo vya kuwekea mitungi ya maji na bahari ya shaba iliyokuwa penye Nyumba ya Bwana Wakasidi wakazivunja, nazo zile shaba zao wakazipeleka Babeli.[#Yer. 27:19-22.]

14Hata masufuria na majembe na makato ya kusafishia mishumaa na kata navyo vyombo vyote pia vya shaba vilivyotumiwa Nyumbani mwa Bwana wakavichukua.

15Nazo sinia na vyano vilivyokuwa vya dhahabu tupu navyo vilivyokuwa vya fedha tupu, mkuu wao waliomlinda mfalme akavichukua.

16Zile nguzo mbili na ile bahari moja na vile vilingo vya kuwekea mitungi ya maji, ambavyo mfalme Salomo alivitengenezea Nyumba ya Bwana, shaba zao hivi vyombo vyote hazikuwezekana kupimwa kwa mizani.[#1 Fal. 7:15,23,27.]

17Nguzo moja urefu wake ulikuwa mikono kumi na nane, juu yake palikuwa na kilemba cha shaba, urefu wa kwenda juu wa hicho kilemba ulikuwa mikono mitatu; hicho kilemba kilikuwa kimezungukwa na misuko kama ya mkeka iliyokuwa yenye komamanga, yote pia ni ya shaba; nayo nguzo ya pili ilikuwa vivyo hivyo, nayo ilikuwa yenye misuko kama ya mkeka.

18Mkuu wao waliomlinda mfalme akamchukua mtambikaji mkuu Seraya na mtambikaji wa pili Sefania nao walinda kizingiti watatu.

19Namo mjini akachukua mtumishi mmoja wa nyumbani mwa mfalme aliyewekwa kuwa mkuu wa kuwasimamia wapiga vita na watu watano waliokuwa na kazi machoni pa mfalme waliopatikana mjini na mwandishi wa mkuu wa vikosi aliyewaandika watu wa nchi waliotakiwa uaskari na watu sitini wa shambani waliopatikana mle mjini.

20Hao akawachukua Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawapeleka Ribula kwa mfalme wa Babeli.

21Naye mfalme wa Babeli akawapiga na kuwaua huko Ribula katika nchi ya Hamati. Kisha akwahamisha Wayuda, waitoke nchi yao.[#2 Fal. 23:33.]

Mtawala nchi Gedalia anauawa wa Isimaeli.

(22-26: Yer. 40:5,7-9; 41:1-7; 43:5-7.)

22Wale watu waliosalia katika nchi ya Yuda, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, aliowasaza, akawawekea Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Safani, kuwasimamia.

23Wakuu wote wa vikosi, wao na watu wao, waliposikia, ya kuwa mfalme wa Babeli amemweka Gedalia kuwasimamia, wakaja Misipa kwa Gedalia; ndio Isimaeli, mwana wa Netania, na Yohana, mwana wa Karea, na Seraya, mwana wa Tanumeti, wa Netofa, na Yazania, mwana wa mtu wa Maka, hao wenyewe na watu wao.

24Waume hawa na watu wao Gedalia akawaapia na kuwaambia: Msiwaogope watumishi wa Wakasidi! Kaeni katika nchi hii na kumtumikia mfalme wa Babeli! Ndipo, mtakapoona mema.

25Ikawa katika mwezi wa saba, ndipo, Isimaeli, mwana wa Netania, mwana wa Elisama wa kizazi cha kifalme, alipokuja pamoja na watu kumi, wakampiga Gedalia, naye kafa; wakawaua hata Wayuda na Wakasidi waliokuwa naye huko Misipa.

26Kisha watu wote, wadogo kwa wakubwa, na wakuu wa vikosi wakaondoka, wakaja Misri, kwani waliwaogopa Wakasidi.

Mfalme Yoyakini anafunguliwa.

(27-30: Yer. 52:31-34.)

27Ikawa katika mwaka wa 37 wa kuhamishwa kwake Yoyakini, mfalme wa Wayuda, katika mwezi wa kumi na mbili siku ya ishirini na saba, ndipo, Ewili-Merodaki, mfalme wa Babeli, alipomwonea uchungu Yoyakini, mfalme wa Wayuda; ikawa katika mwaka huohuo, alipoupata ufalme, akamtoa kifungoni,[#2 Fal. 24:15.]

28akasema naye maneno mema, akampa kiti chake cha kifalme juu ya viti vya wafalme wengine waliokuwa naye huko Babeli.

29Ndipo, alipoyavua mavazi ya kifungoni, akala chakula usoni pa mfalme pasipo kukoma siku zote, alizokuwapo.

30Nazo mali za kujitunza kila siku akapewa na mfalme wa Babeli, siku kwa siku akapata yaliyompasa siku zote, alizokuwapo.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania