2 Wafalme 9

2 Wafalme 9

Ufalme wa Waisiraeli: Yehu anamwua Yoramu na Ahazia.

1Mfumbuaji Elisa akamwita mmoja wao wanafunzi wa wafumbuaji, akamwambia: Jifunge viuno vyako, kisha kichukue kichupa hiki cha mafuta mkononi mwako, uende Ramoti wa Gileadi!

2Utakapofika huko, umtazame huko Yehu, mwana wa Yosafati, mwana wa Nimusi, kisha ingia mwake, umwondoe kwenye ndugu zake na kumwingiza katika chumba cha ndani!

3Kisha kichukue hicho kichupa cha mafuta, uyamimine kichwani pake na kumwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nimekupaka mafuta, uwe mfalme wa Waisiraeli. Kisha fungua mlango, ukimbie pasipo kukawia![#1 Fal. 19:16.]

4Ndipo, yule kijana aliyekuwa mfumbuaji kijana alipokwenda Ramoti wa Gileadi.

5Alipofika akawakuta wakuu wa vikosi, wakikaa pamoja, akasema: Niko na neno la kukuambia wewe mkuu. Yehu alipomwuliza: Mkuu gani kwetu sisi sote? akajibu: Wewe mkuu.

6Ndipo, alipoondoka, akaingia nyumbani; humo akayamimina yale mafuta kichwani pake na kumwambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Nimekupaka mafuta, uwe mfalme wao Waisiraeli walio ukoo wake Bwana.

7Utawaua walio wa mlango wa bwana wako Ahabu, nipate kuzilipiza damu za wafumbuaji waliokuwa watumishi wangu, nazo damu za watumishi wote wa Bwana nikizitaka mkononi mwa Izebeli.[#1 Fal. 21:22.]

8Mlango wote wa Ahabu utaangamia, nitakapowatowesha kwao wa Ahabu wote walio wa kiume, kama watakuwa wamefungwa au kama watakuwa wamefunguliwa kwao Waisiraeli.[#1 Fal. 14:10.]

9Nitautoa mlango wa Ahabu, uwe kama mlango wa Yeroboamu, mwana wa Nebati, na kama mlango wa Basa, mwana wa Ahia.[#1 Fal. 15:29; 16:3,11.]

10Naye Izebeli mbwa watamla shambani kwa Izireeli, pasiwepo atakayemzika. Kisha akafungua mlango, akakimbia.[#1 Fal. 21:23.]

11Yehu alipotokea kwao watumishi wa bwana wake, wakamwuliza: Ni habari njema? Mbona huyo mwenye wazimu ameingia mwako? Akawajibu: Mnamjua yule mtu na maneno yake.

12Wakamwambia: Uwongo huu! Tupashe habari zake! Ndipo, aliposema: Amesema hivi na hivi, akaniambia kwamba: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana: Nimekupaka mafuta, uwe mfalme wa Waisiraeli.

13Ndipo, wote walipozivua nguo zao upesi, wakaziweka miguuni pake juu ya vipago, zivifunike, wakapiga baragumu kwamba: Yehu ni mfalme![#Mat. 21:7.]

14Kisha Yehu, mwana wa Yosafati, mwana wa Nimusi, akamlia Yoramu njama. Ni hapo, Yoramu alipokuwa akiulinda mji wa Ramoti wa Gileadi, yeye na Waisiraeli wote, usichukuliwe na Hazaeli, mfalme wa Ushami.

15Lakini mfalme Yoramu alikuwa amerudi Izireeli, apate watakaomponya vidonda, Washami walivyompiga, alipopigana na Hazaeli, mfalme wa Ushami. Basi, Yehu akawaambia: Kama ndivyo, roho zenu nazo zinavyotaka, asiponyoke mtu wa kutoka humu mjini kwenda Izireeli na kuzipeleka habari hizi.[#2 Fal. 8:28-29.]

16Kisha Yehu akalipanda gari lake kwenda Izireeli, kwani ndiko, Yoramu alikougulia, naye Ahazia, mfalme wa Wayuda, alikuwa ameshuka kumtazama Yoramu.[#2 Fal. 8:29.]

17Mlinzi aliyesimama mnarani juu kule Izireeli alipoliona kundi zima la Yehu, likija, akasema: Mimi naona kundi zima la watu! Ndipo, Yoramu alipomwambia: Chukua mpanda farasi, mtume kuwaendea njiani, awaulize: Mwaleta habari njema?

18Kwa hiyo mpanda farasi akamwendea njiani, akamwambia: Hivi ndivyo, mfalme anavyouliza: Waleta habari njema? Yehu akajibu: Unatuulizaje habari? Zunguka, unifuate! Ndipo, mlinzi alipoleta habari kwamba: Yule mjumbe amefika kwao, lakini hakurudi.

19Basi, akatuma mpanda farasi wa pili; naye alipofika kwao akasema: Hivi ndivyo, mfalme anavyouliza: Waleta habari njema? Yehu akajibu: Unatuulizaje habari? Zunguka, unifuate!

20Mlinzi akapasha habari tena kwamba: Amefika kwao, lakini hakurudi. Lakini ile namna ya kuendesha gari ni kama ya Yehu, mwana wa Nimusi, kwani analiendesha gari lake kama mwenye wazimu.

21Ndipo, Yoramu alipoagiza, wafunge farasi penye magari; walipokwisha kulifungia gari lake farasi, Yoramu, mfalme wa Waisiraeli, akatoka pamoja na Ahazia, mfalme wa Wayuda, kila mmoja katika gari lake, kumwendea Yehu njiani; wakamkuta penye shamba la Naboti wa Izireeli.[#1 Fal. 21:1.]

22Yoramu alipomwona Yehu akamwuliza: Waleta habari njema, Yehu? Akajibu: Ni habari gani njema? Ugoni wa mama yako Izebeli na uchawi wake si mwingi?

23Ndipo, Yoramu alipoligeuza gari kwa mikono yake, akakimbia na kumwambia Ahazia: Tumedanganyika, Ahazia.

24Yehu akaushika upindi kwa mkono wake, akauvuta kwa nguvu, akampiga Yoramu katikati ya mabega yake, mshale ukatokea moyoni mwake, akaangukia magotini garini mwake.

25Kisha akamwagiza Bidekari aliyekuwa mkuu wa askari thelathini: Mchukue, umtupe penye shamba la Naboti wa Izireeli! Kumbuka, mimi na wewe tulipomfuata baba yake Ahabu na kupanda farasi sisi wawili, hapo Bwana alilitoa tamko lile la kumtisha kwamba:[#1 Fal. 21:19.]

26Ndivyo, asemavyo Bwana: Damu ya Naboti nazo damu za wanawe, nilizoziona jana, nitakulipisha huku kwenye shamba hili; ndivyo, asemavyo Bwana. Sasa mchukue, umtupe katika shamba hilo, kama Bwana alivyosema.

27Ahazia, mfalme wa Wayuda, alipoviona akakimbia na kuishika njia ya Beti-Hagani (Nyumba ya Bustani), Yehu akamfuata mbiombio, akaagiza: Naye mpigeni katika gari lake! Wakampiga hapo pa kupandia Guri karibu ya Ibileamu; akakimbia hata Megido, ndiko alikokufa.[#2 Mambo 22:7-9.]

28Watumishi wake wakampeleka Yerusalemu katika gari lake, wakamzika katika kaburi lake kwa baba zake mjini mwa Dawidi.[#2 Fal. 14:20; 23:30.]

29Huyu Ahazia alikuwa ameupata ufalme wa Wayuda katika mwaka wa 11 wa Yoramu, mwana wa Ahabu.

Izebeli anauawa vibaya.

30Kisha Yehu akaja Izireeli. Izebeli alipoyasikia, akatia wanja machoni pake, akakipamba nacho kichwa chake vizuri, kisha akachungulia dirishani.

31Yehu alipoingia langoni mwa mji, akamwuliza: Zimuri aliyemwua bwana wake hajambo?[#1 Fal. 16:10,18.]

32Ndipo, alipouelekeza uso wake kwenye lile dirisha na kuuliza: Yuko nani aliye upande wangu? Alipowaona watumishi wa nyumbani wawili au watatu, wakimchungulia,

33akaagiza: Msukumeni! Wakamsukuma na kumbwaga chini, ukuta ukaenea damu yake, nao farasi vilevile, nao wakamkanyaga.

34Yehu alipokwisha kuingia, akala, akanywa, kisha akaagiza: Haya! Mtazameni yule mwanamke aliyeapizwa, mmzike, kwani ni binti mfalme.

35Walipokwenda kumzika hawakumwona, ni kichwa tu na miguu na viganja vya mikono.

36Wakarudi kumpasha hizi habari; ndipo, aliposema: Hivi ndivyo, Bwana alivyosema kinywani mwa Elia wa Tisibe kwamba: Shambani kwa Izireeli mbwa watazila nyama za mwili wake Izebeli.[#1 Fal. 21:23; 2 Fal. 9:10.]

37Nao mzoga wake Izebeli utakuwa kama kinyesi cha shambani katika viwanja vya Izireeli, watu wasiweze kusema: Huyu hapa ni Izebeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania