The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, Sauli alipokwisha kufa, Dawidi akarudi kwa kuwapiga Waamaleki; kisha Dawidi akakaa Siklagi siku mbili.
2Ilipokuwa siku ya tatu, mara akaja mtu aliyetoka makambini kwa Sauli, nguo zake zilikuwa zimeraruliwa, napo kichwani pake palikuwa na vumbi; naye alipofika kwake Dawidi akajitupa chini na kumwangukia.
3Dawidi alipomwuliza: Unatoka wapi? akamwambia: Nimekimbia makambini kwa Waisiraeli.
4Ndipo, Dawidi alipomwambia: Nisimulie yaliyofanyika huko! Akamwambia, ya kuwa watu walikimbia penye mapigano, kwa maana wengi wa kwao waliangushwa, wakafa, naye Sauli na mwanawe Yonatani wamekufa.
5Dawidi akamwuliza huyo kijana aliyempasha habari hizi: Umejuaje, ya kuwa Sauli amekufa na mwanawe Yonatani?
6Yule kijana aliyempasha hizi habari akamwambia: Ikanitukia, nifike mlimani kwa Gilboa, mara nikamwona Sauli, akiuegemea mkuki wake, nayo magari pamoja na wapanda farasi wakamsonga.[#1 Sam. 31:1-3.]
7Alipogeuka nyuma, akaniona, akaniita; nami nikamwitikia kwamba: Nipo hapa!
8Akaniuliza: Wewe nani? Nikamjibu: Mimi Mwamaleki.
9Akaniambia: Njoo hapa, nilipo, uniue! Kwani kizunguzungu kimenipata, nayo roho yangu ingali nzima.
10Ndipo, nilipokuja hapo, alipokuwa, nikamwua, kwani nilijua, ya kuwa hawezi kupona kwa hivyo, alivyoanguka;. kisha nikakichukua kilemba chake kichwani pake na kikuku chake mkononi pake, nimevileta hapa kwa bwana wangu, ni hivi!
11Ndipo, Dawidi alipoyakamata mavazi yake, akayararua, nao watu wote waliokuwa naye wakafanya hivyo.[#1 Mose 37:29.]
12Wakaomboleza na kulia machozi, wakafunga mfungo mpaka jioni kwa ajili ya Sauli na kwa ajili ya mwanawe Yonatani na kwa ajili ya watu wa Bwana na kwa ajili yao wa mlango wa Isiraeli, kwa kuwa wameangushwa na panga.[#1 Sam. 31:13.]
13Kisha Dawidi akamwuliza huyo kijana aliympasha habari hizi: Wewe u mtu wa wapi? Akasema: Mimi ni mwana wa mtu mgeni wa Amaleki.
14Dawidi akamwambia: Kumbe hukuogopa kuuinua mkono wako, umwangamize aliyepakwa mafuta na Bwana?[#1 Sam. 24:7.]
15Ndipo, Dawidi alipomwita mmoja wao vijana, akamwambia: Njoo, umpige! Naye alipompiga, akafa;[#2 Sam. 4:10,12.]
16kisha Dawidi akamwambia: Damu yako na ikujie kichwani pako! Kwani kinywa chako kimekuponza na kusema kwamba: Mimi nimemwua aliyepakwa mafuta na Bwana.[#1 Fal. 2:23,33.]
17Kisha Dawidi akatunga ombolezo hili la kumwombolezea Sauli na mwanawe Yonatani.
18Akaagiza kuwafundisha wana wa Yuda wimbo huu wa upindi, nao utaukuta, umeandikwa katika kitabu cha Mnyofu:[#2 Sam. 1:22; Yos. 10:13.]
19Isiraeli, waliokuwa pambo lake wameuawa vilimani kwako!
Imekuwaje, wakiangushwa hao mafundi wa vita?
20Msiyasimulie Gati, wala msiyatangaze njiani kwa[#Mika 1:10; 1 Sam. 18:6.]
Askaloni, wasipate kufurahi wanawake wa Wafilisti, wasipige
vigelegele wao wanawake wa kimizimu!
21Msione tena umande wala mvua, ninyi milima ya Gilboa,[#4 Mose 15:18-21.]
yasiwe tena kwenu mashamba yenye malimbuko! Kwani ndiko,
zilikoachwa ngao zao hao mafundi wa vita, ngao yake Sauli
naye, kama hakupakwa mafuta.
22Upindi wake Yonatani ulikuwa hauponyi, ijapo wawe
mafundi wa vita wenye unono, uliotaka kuwaua; upanga wake Sauli haukurudi alani, usipokuwa umeua.
23Sauli na Yonatani walipatana kwa kupendana mioyoni,
hawakutengeka walipoishi, wala walipokufa. Walikuwa wepesi
kuliko kozi, walikuwa wenye nguvu kuliko simba.
24Ninyi wanawake wa Kiisiraeli, mwombolezeeni Sauli!
Kwani aliwavika mavazi ya kifalme yenye urembo mwingi, kisha
hizo nguo zenu akazipamba kwa mapambo ya dhahabu.
25Imekuwaje, wakiangushwa vitani hao mafundi wa vita?
Yonatani akiuawa vilimani kwako?
26Moyo wangu umesongeka kwa ajili yako, maana wewe
ulinipendeza sana, ndugu yangu Yonatani, upendo wako
ulinifurahisha kuliko upendo wa wanawake.
27Imekuwaje, wakiangushwa hao mafundi wa vita? hayo mata
makali ya kupigia vita yakiangamia hivyo?