The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamtuma Natani kwenda kwake Dawidi. Alipofika kwake akamwambia: Kulikuwa na watu wawili, wamekaa katika mji mmoja, mmoja ni mkwasi, mmoja ni maskini.
2Yule mkwasi alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi mno.
3Lakini yule maskini alikuwa hanacho cho chote, kisipokuwa kikondoo kimoja tu, alichokinunua. Akakifuga, kikakua nyumbani mwake pamoja na watoto wake, kikala chakula chake, kikanywa katika kikombe chake mwenyewe, kikalala kifuani pake, maana kilikuwa kama mtoto wake wa kike.
4Siku moja yule mkwasi akafikiwa na mgeni, akaona uchungu wa kuchukua kondoo wake au ng'ombe wake mmoja wa kumpa yule mpitaji aliyefikia kwake, basi, akakichukua kikondoo cha yule maskini, akamtengenezea yule mtu aliyefikia kwake.
5Ndipo, makali ya Dawidi yalipowaka moto sana kwa ajili ya mtu huyo, akamwambia Natani: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, mtu aliyeyafaya hayo ni mtu wa kufa!
6Kile kikondoo nacho sharti akilipe mara nne, kwa kuwa amefanya jambo kama hilo pasipo kuona huruma.[#2 Mose 22:1.]
7Natani akamwambia Dawidi: Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Mimi nilikupaka mafuta, uwe mfalme wa Waisiraeli. Mimi nami nikakuponya mkononi mwa Sauli,[#1 Fal. 20:40.]
8nikakupa nyumba ya bwana wako nao wanawake wa bwana wako, ulale nao, nikakupa nayo milango ya Isiraeli na ya Yuda; kama haya ni machache, nitayaongeza na kukupa haya na haya.
9Kwa sababu gani umelibeza neno la Bwana ukilifanya lililo baya machoni pake? Yule Mhiti Uria umemwua kwa upanga, ukamchukua mkewe, awe mke wako, ulipokwisha kumwua kwa panga za wana wa Amoni.[#2 Sam. 11; 1 Fal. 15:5.]
10Sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako kale na kale, kwa kuwa umenibeza na kumchukua mkewe yule Mhiti Uria, awe mke wako.[#2 Sam. 13:28-29; 18:14; 2 Fal. 25:7.]
11Hivi ndivyo, anavyosema Bwana: Utaniona nikikupatia jambo baya litakalotoka nyumbani mwako, nitawachukua wake zako machoni pako, nimpe mwenzako, alale nao wake zako katika mwanga wa jua hili.[#2 Sam. 16:22; Iy. 31:9-10.]
12Kweli umelifanya jambo lako na kufichaficha, lakini mimi nitalifanya jambo hilo mbele ya Waisiraeli wote na mbele ya jua.
13Ndipo, Dawidi alipomwambia Natani: Nimemkosea Bwana! Natani akamwambia Dawidi: Kwa hiyo Bwana ameliondoa hili kosa lako, hutakufa.[#2 Sam. 24:10; Sh. 51:3.]
14Lakini kwa kuwa umewapatia wachukivu wa Bwana katika jambo hilo sababu ya kuyaongeza mabezo yao, yule mwana aliyezaliwa hana budi kufa.[#2 Sam. 11:27.]
15Natani alipokwisha akwenda nyumbani kwake, Bwana akampiga yule mtoto, mkewe Uria aliyemzalia Dawidi, akawa mgonjwa sana.
16Dawidi akamtafuta Mungu na kumwombea mtoto, kisha Dawidi akafunga, tena alipoingia mwake akalala chini usiku kucha.
17Wazee wa nyumbani mwake wakamtokea, wamwinue chini, lakini akakataa, nacho chakula hakula nao.
18Ilipokuwa siku ya saba, mtoto akafa; nao watumishi wa Dawidi wakaogopa kumpasha habari hii, ya kuwa mtoto amekufa, kwani waliwaza kwamba: Mtoto alipokuwa angali akiishi, hakuzisikia sauti zetu, tulipomwambia neno; sasa tutawezaje kumwambia: Mtoto amekufa? Angejifanyia kibaya.
19Lakini Dawidi alipowaona watumishi wake, wakinong'onezana, Dawidi akatambua, ya kuwa mtoto amekufa; kwa hiyo Dawidi akawauliza watumishi wake: Mtoto amekufa? wakamwambia: Amekufa.
20Ndipo, Dawidi alipoondoka chini, akaoga na kujipaka mafuta, akavaa nguo nyingine, akaingia nyumbani mwa Bwana, akamwangukia. Kisha akaingia nyumbani mwake na kutaka vyakula; walipokwisha kumwandalia, akala.
21Ndipo, watumishi wake walipomwuliza: Jambo hili, unalolifanya, linakuwaje? Kwani mtoto alipokuwa angali akiishi, umefunga na kulia machozi; lakini mtoto alipokwisha kufa, umeinuka, ukala chakula.
22Akasema: Kweli mtoto alipokuwa angali akiishi, nimefunga na kulia machozi, kwani nilisema: Labda Bwana atanihurumia, mtoto apate kupona.
23Lakini sasa amekwisha kufa, nifungeje tena? Nitaweza kumrudisha uzimani tena? Mimi nitakwenda kwake, lakini yeye harudi kwangu.
24Dawidi akamtuliza moyo mkewe Bati-Seba, akaingia kwake, akalala naye, kisha akazaa mtoto mume, akamwita jina lake Salomo (Mtulivu), naye Bwana akampenda.
25Baadaye Dawidi akampeleka, akamtia mkononi mwa mfumbuaji Natani, huyo akamwita jina lake Yedidia (Mpendwa wa Bwana) kwa ajili ya Bwana.
26Yoabu akapiga vita kule Raba kwa wana wa Amoni, akauteka huo mji wa kifalme.[#Yer. 49:2.]
27Ndipo, Yoabu alipotuma wajumbe kwake Dawidi kwamba: Nimepiga vita huku Raba, nikauteka mji huu ulio wenye maji.
28Sasa wakusanye watu waliosalia, uuzinge mji huu, uuteke, nisiuteke mimi mji huu, jina langu likitangazwa humu.
29Ndipo, Dawidi alipowakusanya watu wote, akaenda nao Raba, akapiga vita huko, akauteka.
30Akaliondoa taji la mfalme kichwani pake, nao uzito wake ulikuwa frasila tatu za dhahabu, nalo lilikuwa na vito vyenye kima; hilo Dawidi akavikwa kichwani. Namo mjini akatoa mateka mengi sana.
31Nao watu waliokuwamo akawatoa, akawaweka chini ya misumeno na chini ya magari ya chuma ya kupuria na chini ya mashoka ya chuma, wengine akawashurutisha kupita katika moto wa tanuru. Hivyo Dawidi akaifanyizia miji yote ya wana wa Amoni. Kisha Dawidi akarudi Yerusalemu pamoja na watu wake wote.