The chat will start when you send the first message.
1Dawidi alipokwisha kupita kidogo hapo kilimani juu, mara Siba, kijana wa Mefiboseti, akamwendea njiani, anao punda wawili waliotandikwa kuchukua mikate 200 na maandazi 100 ya zabibu na maandazi 100 ya kuyu na kiriba cha mvinyo.[#2 Sam. 9:2.]
2Mfalme alipomwuliza: Haya unanileteaje? Siba akasema: Punda ni wa kuchukua walio wa mlango wa mfalme, nayo mikate na maandazi ni ya kula ya vijana, nayo mvinyo ni ya kunywa, mtu akichoka nyikani.
3Mfalme akamwuliza: Naye mwana wa bwana wako yuko wapi? Ndipo, Siba alipomwambia mfalme: Tazama, anakaa Yerusalemu, kwani amesema: Leo wao wa mlango wa Isiraeli watanirudishia ufalme wa baba yangu.[#2 Sam. 19:26.]
4Ndipo, mfalme alipomwambia Siba: Tazama, mali zote za Mefiboseti ni zako! Siba naye akasema: Ninakuangukia, nione tena upendeleo machoni pako, bwana wangu mfalme!
5Mfalme Dawidi alipofika Bahurimu, mara mle akatoka mtu wa ukoo wao walio mlango wa Sauli, jina lake Simei, mwana wa Gera; alipotoka alikwenda akitukana.[#2 Mose 22:28; 1 Fal. 2:8.]
6Tena akamtupia Dawidi mawe nao watumishi wote wa mfalme Dawidi, nao watu wote na mafundi wa vita wote walikuwa kuumeni na kushotoni kwake.
7Hivi ndivyo, Simei alivyosema akitukana: Toka! Toka, wewe mtu wa damu, wewe mtu usiyefaa!
8Bwana anakulipisha damu zao wote walio wa mlango wa Sauli, ambaye umejifanya kuwa mfalme mahali pake. Yeye Bwana ameutia ufalme mkononi mwa mwanao Abisalomu, wewe nawe umepatwa na mabaya, kwa kuwa wewe u mtu wa damu.
9Ndipo, Abisai, mwana wa Seruya, alipomwambia mfalme: Mbona mbwa mfu huyu anamtukana bwana wangu mfalme? Acha, nimwendee, nimkate kichwa mara moja![#1 Sam. 26:8.]
10Lakini mfalme akasema: Tuna bia gani mimi nanyi, wana wa Seruya? Na atukane hivyo; kama Bwana amemwagiza: Mtukane Dawidi! yuko nani awezaye kusema: Mbona unafanya hivyo?[#2 Sam. 19:22.]
11Kisha Dawidi akamwambia Abisai na watumishi wake wote: Tazameni, mwanangu aliyetoka kiunoni mwangu anaitaka roho yangu! Sasa huyu mtu wa Benyamini anafanya nini? Mwacheni, atukane, kwani Bwana amemwagiza hivyo.
12Labda Bwana atautazama ukiwa wangu, yeye Bwana anirudishie mema kwa hivyo, huyu anavyonitukana leo hivi.
13Kisha Dawidi akaenda zake na watu wake, Simei naye akaenda kandokando ya mlima karibu yake akiendelea kutukana na kumtupia mawe na kumpiga kokotokokoto.
14Mfalme na watu wote waliokuwa naye walipofika mahali fulani walikuwa wamechoka, wakapumzika hapo.
15Abisalomu na Waisiraeli wote walipoingia Yerusalemu, Ahitofeli alikuwa naye.
16Ikawa, Mwarki Husai, yule rafiki yake Dawidi, alipofika kwa Abisalomu, Husai akamwambia Abisalomu: Pongezi, mfalme! Pongezi, mfalme![#1 Sam. 10:24; 2 Sam. 15:37.]
17Abisalomu akamwuliza Husai: Huu ndio welekevu, unaomfanyizia rafiki yako? Mbona hukuenda pamoja na rafiki yako?
18Husai akamwambia Abisalomu: Sivyo! Ila yule, Bwana aliyemchagua na watu hawa wote na waume wote wa Waisiraeli, basi, nami ni mtu wake, nikae naye!
19Tena nimtumikie nani? Siye mwanawe? Kama nilivyomtumikia baba yako, ndivyo, nitavyokutumikia.
20Abisalomu akamwambia Ahitofeli: Haya! Nipeni shauri, jinsi tutakavyofanya!
21Ahitofeli akamwambia Abisalomu: Ingia kwao masuria wa baba yako, aliowaacha kuiangalia nyumba! Hapo, Waisiraeli wote watakaposikia, ya kuwa umechukizwa kabisa na baba yako, ndipo, mikono yao wote waliorudi upande wako itakapopata nguvu.[#2 Sam. 15:16.]
22Kisha wakampigia Abisalomu hema darini, naye Abisalomu akaingia kwao masuria wa baba yake machoni pao Waisiraeli wote.[#2 Sam. 12:11; 3 Mose 18:8.]
23Siku zile shauri, alilolitoa Ahitofeli likawa sawa na neno, mtu aliloliuliza kwake Mungu. Ndivyo, mashauri yote ya Ahitofeli, yalivyowaziwa kuwa, kama siku za Dawidi, vivyo hivyo hata siku za Abisalomu.