The chat will start when you send the first message.
1Dawidi akawakagua watu waliokuwa naye, akawawekea wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia.[#2 Sam. 15:19.]
2Kisha Dawidi akawatuma hao watu kwenda vitani, akawatia fungu la tatu mkononi mwa Yoabu, fungu jingine la tatu mkononi mwa Abisai, mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, tena fungu jingine la tatu mkononi mwa Itai wa Gati. Kisha mfalme akawaambia hao watu: Hata mimi nitatoka pamoja nanyi kwenda vitani.
3Lakini watu wakasema: Usitoke pamoja nasi! Kwani kama itakuwa, tukimbie, wale hawatatuelekezea sisi mioyo; ijapo watu wa kwetu wafe kama nusu nzima, hawatuelekezea sisi mioyo, kwani wewe u kama watu elfu kumi wa kwetu. Kwa hiyo itatufaa sasa, ukae mjini, upate kuja kutusaidia.
4Mfalme akawaitikia kwamba: Yaliyo mema machoni penu, basi, nitayafanya. Kisha mfalme akaja kusimama kando penye lango la mji, nao watu wote wakatoka mia kwa mia, na elfu kwa elfu.
5Ndipo, mfalme alipomwagiza Yoabu na Abisai na Itai wa Gati kwamba: Nataka hili tu, mmwendee mvulana Abisalomu kwa upole! watu wote wakayasikia, mfalme alipowaagiza wakuu wote hayo kwa ajili ya Abisalomu.[#2 Sam. 18:12.]
6Kisha watu wakawaendea Waisiraeli maporini, nayo mapigano yakawa katika mwitu wa Efuraimu.
7Nao watu wa Waisiraeli wakapigwa kabisa na watumishi wa Dawidi, wapata hata 20000,
8nayo mapigano yalikuwa yameenea po pote katika nchi hiyo, nao watu, mwitu uliowala, walikuwa wengi kuliko wao, panga ziliowala siku hiyo.
9Ikatukia, watumishi wa Dawidi wamwone Abisalomu, naye Abisalomu alikuwa amepanda nyumbu; huyo nyumbu alipopita chini ya mkwaju mkubwa wenye matawi mengi yaliyofungamana, mara tawi moja likakikamata kichwa chake mlemle katika mkwaju, hivyo akaangikwa katikati ya mbingu na nchi, kwani nyumbu aliyekuwa chini yake alikimbia.
10Mtu mmoja aliyeviona akampasha Yoabu habari akisema: Tazama, nimemwona Abisalomu, alivyoangikwa mkwajuni.
11Ndipo, Yoabu alipomwambia yule mtu aliyempasha habari hiyo: Kama umemwona hivyo, sababu gani kukumpiga, aanguke chini, nami nikakupa fedha kumi na mkanda mmoja?
12Yule mtu akamwambia Yoabu: Ijapo ningepimiwa mimi fedha elfu mikononi mwangu, nisingemkunjulia mwana wa mfalme mkono wa kumpiga, kwani masikioni petu mfalme amekuagiza wewe na Abisai na Itai kwamba: Niangalieni mvulana Abisalomu![#2 Sam. 18:5.]
13Kwani ningaliipotoa roho yake, jambo hilo lote halingalifichikana kwa mfalme, nawe wewe ungaliniinukia.
14Yoabu akasema: Haifai, nikijikawilisha huku kwako. Akachukua mikuki mitatu mkononi mwake, akamchoma nayo Abisalomu moyoni, angaliko mzima mlemle mkwajuni.
15Kisha vijana kumi waliomchukulia Yoabu mata wakamzunguka Abisalomu, wakamaliza kumwua kwa kumpiga.
16Kisha Yoabu akapiga baragumu; ndipo, watu waliporudi wakiacha kuwakimbiza Waisiraeli, kwani ndivyo, Yoabu alivyowazuia watu wake.
17Wakamchukua Abisalomu, wakamtupa mle mwituni katika shimo kubwa, juu yake wakakusanya mawe kuwa chungu kubwa sana. Kisha Waisiraeli wote wakakimbilia kila mtu hemani kwake.
18Naye Abisalomu alipokuwa mzima bado alichukua nguzo ya mawe kule Bondeni kwa Mfalme, akaisimamisha, kwani alisema: Mimi sina mwana wa kulikumbusha jina langu; kwa hiyo aliiita ile nguzo ya mawe kwa jina lake, ikaitwa Mkono wa Abisalomu hata siku hii ya leo.
19Ahimasi, mwana wa Sadoki, akasema: Na nipige mbio kumpelekea mfalme utume mwema, kwani Bwana amemwamulia na kumwokoa mikononi mwa adui zake.[#2 Sam. 15:36; 17:17.]
20Lakini Yoabu akamwambia: Siku hii ya leo wewe hu mtu wa kupeleka utume; siku nyingine utapeleka utume, lakini siku hii ya leo hutapeleka utume wewe, kwa kuwa mwana wa mfalme amekufa.
21Kisha Yoabu akamwambia Mnubi: Nenda kumpasha mfalme habari za mambo, uliyoyaona! Yule Mnubi akamwangukia Yoabu, kisha akaenda na kupiga mbio.
22Lakini Ahimasi, mwana wa sadoki, akamwambia Yoabu tena: Nami na niende mbiombio, nimfuate yule Mnubi. Yoabu akamwambia: Wewe utakimbilia nini, mwanangu? kwani hakuna ujira, utakaopewa.
23Akajibu: Haidhuru, nitakwenda nami na kupiga mbio. Akamwambia: Haya!, Ndipo, Ahimasi alipopiga mbio na kushika njia ya nchi ya tambarare; ndivyo, alivyompita yule Mnubi.
24Naye Dawidi alikuwa amekaa katikati ya malango mawili; mlinzi alipopanda humo langoni kufika juu yake ukutani na kuyainua macho yake, achungulie, mara akaona mtu anayekimbia peke yake.
25Ndipo, mlinzi alipoita, akampasha mfalme habari hizo; naye mfalme akasema: Kama yuko peke yake, basi, kinywani mwake umo utume mwema. Huyu alipofika karibu,
26mlinzi akaona mtu mwingine anayekimbia peke yake; ndipo, mlinzi alipomwita mlinda lango, akamwambia: Tazama, yuko mtu anayekimbia peke yake! Mfalme akasema: Huyu naye analeta utume mwema.
27Kisha mlinzi akasema: Mbio zake yule wa kwanza ninaziona kuwa kama mbio za Ahimasi, mwana wa Sadoki. Mfalme akasema: Ni mtu mwema huyu, naye anakuja kuleta utume mwema.
28Ahimasi akaita na kumwambia mfalme: Pongezi! Kisha akamwangukia mfalme na kujiangusha chini kifudifudi, akasema: Bwana Mungu wako na atukuzwe! Kwani wao waliomwinulia bwana wangu mfalme mikono yao amewatoa.
29Mfalme akauliza: Mvulana Abisalomu hajambo? Ahimasi akasema: Nimeona mtutumo mkubwa, mtumishi wa mfalme Yoabu alipomtuma mtumishi wako, lakini sikujua, kama kuna nini.
30Mfalme akamwambia: Zunguka, uje kusimama hapa! Naye akazunguka, akasimama hapo.
31Mara yule Mnubi akaja, naye akasema kwamba: Bwana wangu mfalme na ausikie huu utume mwema, ya kuwa Bwana amekuamulia leo na kukuokoa mikononi mwao wote waliokuinukia.
32Mfalme akamwuliza huyu Mnubi naye: Mvulana Abisalomu hajambo? Huyu Mnubi akasema: Adui wote wa mfalme na wafanyiziwe kama huyo mvulana! Nao wote waliokuinukia kufanya mabaya na wawe hivyo!
33Ndipo, mfalme alipostuka, akapanda katika chumba cha juu hapo langoni, akalia akisema hivyo, akajiendea na kusema hivyo: Mwanangu Abisalomu! Mwanangu! Mwanangu Abisalomu! Ningalikufa mimi mahali pako! Mwanangu Abisalomu! Mwanangu!