The chat will start when you send the first message.
1Mashina yote ya Waisiraeli wakaja Heburoni kwake Dawidi, wakamwambia kwamba: Tazama, sisi na wewe tu mifupa ya mmoja, nazo nyama za miili yetu ni za mmoja.[#2 Sam. 19:12.]
2Napo hapo kale, Sauli alipokuwa mfalme wetu bado, aliyewaongoza Waisiraeli kwenda na kurudi vitani ni wewe, naye Bwana alikuambia: Wewe utawachunga walio ukoo wangu wa Waisiraeli, nawe wewe utawatawala Waisiraeli.[#1 Sam. 13:14; 25:30.]
3Wazee wote wa Waisiraeli wakamjia mfalme huko Heburoni, mfalme Dawidi akafanya agano nao huko Heburoni mbele ya Bwana, wakampaka Dawidi mafuta, awe mfalme wao Waisiraeli.[#1 Sam. 16:13; 2 Sam. 2:4.]
4Dawidi alikuwa mwenye miaka 30 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 40.[#1 Fal. 2:11; 1 Mambo 29:27.]
5Huko Heburoni alikuwa mfalme wa Wayuda miaka 7 na miezi 6, namo Yerusalemu alikuwa mfalme wa Waisiraeli na wa Wayuda wote miaka 33.
6Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kwa Wayebusi waliokuwa bado wenyeji wa nchi hiyo, nao wakamwambia Dawidi kwamba: Humu hutaiangia kabisa usipowaondoa vipofu na viwete, ni kwamba: Dawidi hataingia humu.
7Lakini Dawidi akaliteka boma la Sioni, ndio mji wa Dawidi.
8Siku hiyo Dawidi alisema: Kila anayetaka kuwapiga Wayebusi na ashike njia ya kukwea katika mfereji, awafikie wale viwete na vipofu wanaochukizwa na roho yake Dawidi. Kwa hiyo husema fumbo la kwamba: Kipofu au kiwete alipo, mtu haingii nyumbani.
9Dawidi akakaa mle bomani, akaliita mji wa Dawidi, Dawidi akaujenga pande zote kuanzia Milo mpaka hapo penye nyumba za mji.
10Dawidi akaendelea kuwa mkuu, kwa sababu Bwana Mungu mwenye vikosi alikuwa naye.[#2 Sam. 3:1.]
11Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Dawidi na miti ya miangati na maseremala na waashi wa kujenga na mawe, wakamjengea Dawidi nyumba.
12Ndipo, Dawidi alipojua, ya kuwa Bwana amemweka kweli kuwa mfalme wao Waisiraeli, kwani ufalme wake ukaja kutukuka zaidi kwa ajili ya ukoo wake wa Waisiraeli.
13Kisha Dawidi akachukua tena masuria na wake mle Yerusalemu alipokwisha kuingia humo na kutoka Heburoni, Dawidi akazaa tena wana wa kiume na wa kike.
14Haya ndiyo majina ya wana, waliozaliwa mle Yerusalemu: Samua na Sobabu na Natani na Salomo,[#Luk. 3:31; Mat. 1:6.]
15na Ibuhari na Elisua na Nefegi na Yafia,
16na Elisama na Eliada na Elifeleti.
17Wafilisti waliposikia, ya kuwa wamempaka Dawidi mafuta, awe mfalme wa Waisiraeli, ndipo, Wafilisti wote walipopanda kumtafuta Dawidi. Dawidi alipovisikia, akashuka kuja ngomeni.
18Wafilisti wakaja, wakajieneza Bondeni kwa Majitu.
19Dawidi akamwuliza Bwana kwamba: Nikipanda kupigana na Wafilisti, utawatia mkononi mwangu? Bwana akamwambia Dawidi: Panda! Kwani nitawatia Wafilisti mkononi mwako.[#1 Sam. 30:8.]
20Ndipo, Dawidi alipokuja Baali-Perasimu; Dawidi alipowapiga huko akasema: Bwana amewaatua adui zangu mbele yangu, kama maji yanavyoatua ukingo. Kwa sababu hii akapaita mahali pale jina lake Baali-Perasimu (Maatuko).
21Wakaacha kule vinyago vyao, lakini Dawidi na watu wake wakavichukua.
22Lakini Wafilisti wakapanda tena, wakajieneza kulekule Bondeni kwa Majitu.
23Naye Dawidi alipomwuliza Bwana, akamwambia: Usipande, ila uzunguke migongoni kwao, upate kuwajia ukitoka juu, misandarusi iliko.
24Hapo, utakaposikia vileleni kwa misandarusi shindo kama ya watu wapitao, basi, hapo piga mbio! Kwani ndipo, Bwana atakapotokea, akutangulie kuyapiga majeshi ya Wafilisti.
25Dawidi akafanya, kama Bwana alivyomwagiza, akawapiga Wafilisti toka Geba, hata mtu afike Gezeri.