The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, Apolo alipokuwako Korinto, Paulo akazunguka hapo penye milima, kisha akafika Efeso, akaona wanafunzi wengine,
2akawauliza: Mmepewa Roho takatifu mlipoanza kumtegemea Bwana? Nao wakamjibu: Hapana, hatujasikia, kama iko Roho takatifu.[#Tume. 2:38.]
3Alipowauliza: Mmebatizwa ubatizo gani? wakasema: Tumebatizwa ubatizo wa Yohana.
4Ndipo, Paulo aliposema: Yohana alibatiza ubatizo wa kujutisha akiwaambia watu, wamtegemee atakayekuja nyuma yake, naye ndiye Yesu.[#Mat. 3:11.]
5Walipoyasikia wakabatiziwa Jina la Bwana Yesu.[#Tume. 8:17; 10:44,46.]
6Paulo alipowabandikia mikono, Roho Mtakatifu akawajia, akasema misemo migeni na kufumbua.
7Nao wote walikuwa waume kama kumi na wawili.
8Alipoingia nyumbani mwa kuombea, akapiga mbiu waziwazi yapata miezi mitatu, akaongeana nao mambo ya ufalme wa Mungu na kuwashinda.
9Lakini palipopatikana wenye mioyo migumu waliokataa kutii, walipoifyoza ile njia mbele ya watu waliokusanyika hapo, akawaacha, akawatenga nao wanafunzi, akaongea na watu kila siku katika shule ya Tirano.[#Tume. 9:2; 2 Tim. 1:15.]
10Vikawa hivyo kama miaka miwili; nao wote waliokaa Asia, Wayuda na Wagriki, wakapata kulisikia Neno la Bwana.
11Mungu akaifanyisha mikono ya Paulo matendo ya nguvu yasiyokuwapo hata kale.[#Tume. 14:3.]
12Kwa hiyo watu waliitwa hata miharuma na mishipi ya mwilini pake, wakawapelekea wagonjwa; ndipo, magonjwa yao yalipowaacha nao pepo wabaya wakawatoka.[#Tume. 5:15.]
13Kulikuwa na wapunga pepo wa Kiyuda waliozunguka hapo, wakajaribu kuwatajia waliopagawa na pepo wabaya Jina la Bwana Yesu, wakisema: Nawaapiza kwa nguvu ya Yesu, Paulo anayemtangaza.[#Luk. 9:49.]
14Nao waliovifanya hivyo walikuwa wana saba wa Sikewa aliyekuwa mtambikaji mkuu wa Kiyuda.
15Lakini pepo mbaya akawajibu: Yesu ninamtambua, naye Paulo ninamjua. Lakini ninyi, m wa nani?
16Kisha yule mtu mwenye pepo mbaya akawarukia, akawakamata wawili, akawafanyizia vibaya kwa nguvu zake, mpaka wakakimbia mle nyumbani wenye uchi na wenye madonda.
17Haya yakatambulikana kwa Wayuda na kwa Wagriki wote waliokaa Efeso, nao wote wakashikwa na woga, lakini Jina la Bwana Yesu likatukuzwa.[#Tume. 5:5,11.]
18Ndipo, wengi wao walioanza kumtegemea walipokuja kuyaungama matendo yao wakiyajutia.
19Nao wengi wao waliofanya kazi za uganga wakavikusanya vyuo vyao, wakaviteketeza mbele yao wote. Wakazihesabu fedha zilizotumiwa, walipovinunua, wakaona, zilikuwa fedha 50000.
20Hivyo Neno likakua, likapata nguvu kwa uwezo wa Bwana.[#Tume. 6:7; 12:24.]
21Hayo yalipomalizika, Paulo aliwaza moyoni kuzunguka katika Makedonia na Akea, apate kwenda Yerusalemu, akasema: Nikiisha kwenda huko, sharti niuone hata Roma![#Tume. 23:11.]
22Akatuma wawili waliomtumikia, Timoteo na Erasto, watangulie kwenda Makedonia, mwenyewe akakawia kidogo Asia.[#Tume. 17:14; Rom. 16:23.]
23Lakini siku zile ikawako kondo isiyokuwa ndogo kwa ajili ya hiyo njia.[#Tume. 19:9; 2 Kor. 1:8-9.]
24Kwani kulikuwa na mfua fedha, jina lake Demetirio, aliyekuwa akitengeneza vijumba vya fedha kwa mfano wa nyumba ya kumwombea Artemi; ndivyo, alivyowapatia mafundi wengi mali nyingi.[#Tume. 16:16.]
25Hao akawakusanya na wengine waliowafanyia kazi, akasema: Waume, mmejua: kazi hii ni chumo letu.
26Tena mnaona, pengine mnasikia, ya kuwa si kwenu Efeso tu, ila hata katika nchi zote za Asia ndiko, huyu Paulo anakohimiza watu na kugeuza mioyo ya makundi mazima ya watu akisema: Miungu iliyofanyika kwa mikono siyo.
27Lakini linalotuogopesha si hilo tu la kwamba: Uchumi wetu utatoweka, ila hata patakatifu pa Artemi aliye mungu wetu wa kike mkuu patabezwa kuwa si kitu. Tena pataangamia ujumbe wake mkuu unaotambikiwa na watu wote wa Asia na wa ulimwengu.
28Walipoyasikia, makali yakawajaa, wakapiga kelele wakisema; Mkuu ni Artemi wa Waefeso!
29Mji ukajaa machafuko, wakapiga mbio wote pamoja kwenda penye machezo, wakawakamata hapo na kuwaburura akina Gayo na Aristarko waliokuwa Wamakedonia, kwani waliandamana na Paulo.[#Tume. 20:4.]
30Paulo alipotaka kuwatokea watu, wanafunzi wakamzuia;
31nao wakubwa wa nchi za Asia wengine waliokuwa rafiki zake wakatuma mtu kwake, wakamtisha, asijitoe kwenda penye machezo.
32Hapo walikuwa wanapiga kelele, wengine hivi, wengine hivi. Watu waliokusanyika hapo walikuwa wamevurugika, wengi hawakujua kilichowakusanya.
33Watu wengine wakamshika Alekisandro, Wayuda waliyemsogeza, aje mbele. Naye Alekisandro akawapungia mkono, akataka kujikania mbele ya makutano;
34lakini walipomtambua, ya kuwa ni Myuda, wakapiga kelele wote pamoja kwa sauti moja kama saa mbili kwamba: Mkuu ni Artemi wa Waefeso!
35Mwandishi wa mji alipowanyamazisha wao wa makundi, akasema: Waume wa Efeso, yuko mtu asiyetambua kwamba: Mji wa Efeso ndio unaoilinda nyumba ya kumwombea Artemi aliye mkuu nao mfano wake uliotoka mbinguni?
36Basi, kwa kuwa haya hayabishiki, imewapasa ninyi kutulia, msifanye neno kwa kikaka.
37Kwani mmewaleta watu hawa wasionyang'anya vilivyomo nyumbani mwa kuombea, wala hawakumbeza mungu wetu.
38Kama Demetirio na mafundi wenziwe wako na neno la kusuta mtu, siku za uamuzi ziko, hata waamuzi wako, basi, na wasutane!
39Lakini mkiwa na neno jingine-jingine, litatimizwa mbele ya wale waliochaguliwa wa kazi hiyo.
40Kwani tunajiponza kusutiwa ugomvi kwa ajili ya matata haya ya leo; tena hatutakuwa na neno la kujikania sisi kwa ajili ya kondo hii.
41Alipokwisha kusema hivyo akauvunja mkutano.