Matendo ya Mitume 23

Matendo ya Mitume 23

1Paulo alipokwisha kuwakazia macho hao wakuu wa barazani, akasema: Waume ndugu, mimi mpaka siku hii ya leo nimekuwapo machoni pa Mungu, kwa hiyo moyo umening'aa wote.[#Tume. 22:1; 24:16.]

2Mtambikaji mkuu Anania alipowaagiza waliosimama hapo, alipokuwa, wampige kinywani,

3ndipo, Paulo alipomwambia: Mungu atakupiga wewe, ukuta wenye uzuri wa kupakwa tu! Wewe unakaa kunihukumu, kama yanavyolingana na Maonyo, tena unayabeza Maonyo kwa kuagiza, nipigwe?[#Mat. 23:27.]

4Nao waliosimama hapo waliposema: Unamtukana mtambikaji mkuu wa Mungu?

5Paulo akasema: Ndugu zangu, sikumjua, ya kuwa ndiye mtambikaji mkuu, kwani imeandikwa: Mtawala ukoo wako usimwambia maovu![#2 Mose 22:28.]

6Paulo alipowatambua, ya kuwa fungu ni Masadukeo, fungu ni Mafariseo, akapaza sauti mbele yao wakuu: Waume ndugu, mimi ni Fariseo, mwana wa Fariseo: ninasutwa hivyo, tunavyoungojea ufufuko wa wafu.[#Tume. 22:3; 26:5.]

7Aliposema hivi, Mafariseo na Msadukeo wakainukiana, nao wengi wakajitenga.

8Kwani Masadukeo hukana ya kwamba: Hakuna ufufuko, hakuna malaika, hakuna roho. Lakini Mafariseo huungama kwamba: Yote yapo.[#Mat. 22:23.]

9Yakawa makelele makubwa; palikuwa na waandishi waliokuwa wa upande wa Mafariseo, wakainuka, wakabishana wakisema: Mtu huyu hatumwoni kiovu cho chote. Kama yuko roho au malaika aliyesema naye, hatutaki kumgombeza Mungu.[#Tume. 5:39; 25:25.]

10Lakini matata yalipokaza, mkuu wa kikosi akaogopa, Paulo asiraruliwe nao akaagiza, askari washuke, wampokonye katikati yao, wampeleke bomani.

11Usiku uliofuata Bwana akamjia na kusimama hapo, alipokuwa, akasema: Tulia! kwani kama ulivyoyashuhudia mambo yangu hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kuyashuhudia hata Roma.[#Tume. 18:9; 19:21; 28:16,23.]

Werevu wa Wayuda.

12Kulipokucha, Wayuda wakakusanyika, wakaapizana, kwamba wasile, wala wasinywe, mpaka wamwue Paulo;

13nao walioapizana hivyo walikuwa wengi kupita 40.

14Kisha wakaendea watambikaji wakuu na wazee, wakasema: Tumeapizana kwa kiapo ya kwamba: Tusionje kitu, mpaka tumwue Paulo!

15Sasa ninyi wakuu nyote, mmweleze mkuu wa kikosi, amshushe kesho kwenu, kwamba mnataka kutambua kwa welekevu, mambo yake yalivyo. Lakini sisi tuko tayari kumwua, akiwa hajawafikia ninyi.

16Mwana wa umbu lake Paulo alipoisikia njama hiyo, akaja, akaingia bomani, akamjulisha Paulo.

17Ndipo, Paulo alipoita bwana askari mmoja, akasema: Umpeleke kijana huyu kwa mkuu wa kikosi! Kwani yuko na habari ya kumpasha.

18Yule akamchukua akampeleka kwa mkuu wa kikosi, akasema: Mfungwa Paulo umeniita, akataka, nimpeleke kijana huyu kwako, yuko na neno la kukuambia.

19Mkuu wa kikosi akamshika mkono, akaondoka naye kwenda penye njama, akamwuliza: Una habari gani ya kunipasha?

20Akasema: Wayuda wamepatana kukuomba wewe, umshushe Paulo kesho kwenye wakuu, kwamba wanataka kumwuliza kwa welekevu, mambo yake yalivyo.

21Basi, wewe usiwaitikie! Kwani watu wao wengi kupita 40 wanamwotea; hao wameapizana kwa kiapo, ya kwamba wasile, wala wasinywe, mpaka wamwue yeye. Sasa wako tayari na kuongoja, uwaitikie wewe.

22Mkuu wa kikosi akamwaga yule kijana, akamkataza kwamba: Usimwambie mtu, ya kuwa umenieleza haya!

Paulo anapelekwa Kesaria.

23Akaita wabwana askari wawili, akasema: Tengenezeni askari 200, waende mpaka Kesaria, na askari wapanda frasi 70 na wenye mikuki 200, wawe tayari saa tatu ya usiku!

24Tandikeni na nyumbu za kumpandisha Paulo, wampeleke vema mpaka kwa Feliki aliye mtawala nchi!

25Akamwandikia barua yenye maneno haya:

26Mimi Klaudio Lisia nakuamkia wewe, mtawala nchi Feliki uliye na nguvu nyingi, salamu!

27Mtu huyu alikamatwa na Wayuda; nao walipotaka kumwua, nikaenda na kikosi cha askari, nikamwokoa, kwani nalisikia, ya kuwa ni Mroma.[#Tume. 21:33; 22:25.]

28Nami kwa hivyo, nilivyotaka kutambua, waliyomsuta, nikamshusha na kumweka barazani kwao wakuu wao.[#Tume. 22:30.]

29Nikaona, ya kuwa anasutiwa mashindano ya Maonyo yao, lakini hakuna neno linalompasa kuuawa na kufungwa tu.[#Tume. 18:14-15; 23:6,9.]

30Tena nilipoambiwa, ya kuwa mtu huyu anatunduiliwa, mara nikampeleka kwako, nikawaagiza hata wenye kumsuta, waseme mbele yako, wanayomsuta.[#Tume. 24:8.]

31Wale askari wakamchukua Paulo, kama walivyoagizwa, wakampeleka usiku mpaka mji wa Antipatiri.

32Kesho yake wakawaacha wale wapanda frasi, waondoke pamoja naye, nao wenyewe wakarudi bomani.

33Wale walipofika Kesaria wakampa mtawala nchi ile barua, wakamsimamisha Paulo mbele yake.

34Alipokwisha kuisoma hiyo barua, akamwuliza upande wa nchi, aliotoka. Aliposikia, ya kuwa ni mtu wa Kilikia,[#Tume. 22:3.]

35akasema: Nitakuuliza na kukusikiliza, wewe kukusuta watakapofika; kisha akaagiza, alindwe katika boma la Herode.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania