The chat will start when you send the first message.
1Siku tano zilipopita, mtambikaji mkuu Anania akatelemka pamoja nao wazee wengine na msemaji aliyitwa Tertulo, wakamsuta Paulo mbele ya mtawala nchi.
2Yule alipoitwa, Tertulo akaanza kumsuta akisema: Kwa nguvu yako, bwana Feliki, tunapata kutengemana sana; na kwa utunzaji wako wewe hili taifa letu limetengenezewa mambo mazuri mengi.
3Hayo yote twayapokea na kukushukuru sana kila siku na kila mahali.
4Lakini nisikuchokeshe kwa maneno mengi; nakuomba utusikilize kidogo kwa utu wako.
5Kwani tumemwona mtu huyu kuwa mwangamizi, akiwaletea kondo Wayuda wote waliopo ulimwenguni po pote, tena ni mkubwa wa chama cha Wanasareti.[#Tume. 17:6.]
6Alipojaribu kupachafua napo Patakatifu, ndipo, tulipomkamata tukitaka kumhukumu kwa Maonyo yetu.[#Tume. 21:28.]
7Lakini mkuu wa kikosi Lisia akamwondoa na nguvu nyingi mikononi mwetu, akaagiza, wenye kumsuta waende kwako wewe.
8Hayo yote, tunayomsuta, utaweza kuyatambua mwenyewe ukimwulizauliza.[#Tume. 23:30.]
9Wayuda nao wakamwitikia wakisema: Hivyo ndivyo, yalivyo.
10Mtawala nchi alipomkonyeza Paulo, aseme, akajibu: Ninakujua, ya kuwa wewe ndiwe mwamuzi wa hili taifa letu tangu miaka mingi; kwa hiyo nitajikania haya mambo yangu na kuchangamka.
11Kwani wewe unaweza kutambua, ya kuwa siku, nilizopanda kwenda Yerusalemu kuombea hapo, hazijapita kumi na mbili.[#Tume. 21:17.]
12Tena hawakuniona hapo Patakatifu, nikiongea na mtu au nikiwachokoza watu, wainukiane, kama ni nyumbani mwa kuombea au mjini pengine.
13Tena wanayonisuta sasa, hawawezi kuyatokeza kuwa ya kweli mbele yako.
14Lakini mbele yako naungama waziwazi: Njia ile, wanayoiita ya chama, ndiyo yangu ya kumtumikia Mungu wa baba zetu, nikayategemea yote yaliyoandikwa penye Maonyo na katika vyuo vya Wafumbuaji.[#Tume. 24:5.]
15Tena liko jambo, ninalolingojea kwa Mungu, nalo ndilo, wanaloliitikia nao hawa wenyewe, la kwamba: Utakuwapo ufufuko wa waongofu na wa wapotovu.[#Dan. 12:2; Yoh. 5:28-29.]
16Kwa hiyo nami mwenyewe nakaza kuulinda moyo wangu, uwe umeng'aa mbele ya Mungu, hata mbele ya watu katika mambo yote.[#Tume. 23:1.]
17Mika ilipopita mingi, nikafika kwao wa taifa langu niwapelekee sadaka ya vipaji.[#Rom. 15:25-26; Gal. 2:10.]
18Hapo ndipo, waliponiona, nikieuliwa Patakatifu; hawakuniona, nikikusanya watu au nikipiga kelele.[#Tume. 21:26-27.]
19Lakini walioniona ndio Wayuda wengine waliotoka Asia; hao ingewapasa kuwapo hapa, wanisute mbele yako, waliyonionea.
20Nao hawa na waseme wenyewe, kama wameona upotovu kwangu, niliposimama mbele yao wakuu,
21lisipokuwa neno lile moja, nililolipazia sauti kabisa nikiinuka katikati yao na kusema: Ufufuko wa wafu ndio, ninaohukumiwa leo mbele yenu![#Tume. 23:6.]
22Feliki alipoyasikia haya akawakawilisha, kwani alipata kuelewa na mambo ya njia hiyo. Kwa hiyo akasema: Mkuu wa kikosi Lisia atakapotelemka, nitayatambulisha naye mambo yenu.[#Tume. 23:26.]
23Akamwagiza bwana askari, Paulo alindwe, lakini asifungwe, wala asiwazuie wenziwe kumtumikia au kumjia.[#Tume. 27:3.]
24Siku zilipopita, Feliki akaja pamoja na mkewe Dirusila aliyekuwa Myuda, akatuma kumwita Paulo, akamsikiliza, akimwonyesha, kumtegemea Kristo Yesu kulivyo.
25Lakini alipoeleza mambo ya kupata wongofu na ya kuziepuka tamaa na ya hukumu itakayokuwapo, Feliki akaingiwa na woga, akajibu: Sasa hivi jiendee tu!
26Hapo, nitakapopata mapumziko, nitakuita tena. Vile vile alingojea kupenyezewa fedha na Paulo, amfungue. Kwa hiyo akamwita mara kwa mara, aongee naye.
27Lakini miaka miwili ilipopita, Porkio Festo akampokea Feliki kazi yake. Feliki akataka kuwapendelea Wayuda, kwa hiyo akamwacha Paulo kifungoni.