The chat will start when you send the first message.
1Festo alipokwisha kuupata utawala nchi, siku zilipopita tatu, akaondoka Kesaria, akapanda kwenda Yerusalemu.
2Ndipo, watambikaji wakuu na Wayuda wenye cheo walipomtokea kumsuta Paulo, wakambembeleza[#Tume. 24:1.]
3na kumwomba, awapendeze akiagiza, aletwe Yerusalemu, kwani walikwisha kula njama ya kumwua njiani.[#Tume. 23:15.]
4Festo akajibu: Paulo analindwa huko Kesaria, nami mwenyewe nitaondoka upesi kwenda huko.
5Kisha akasema: Wenzenu wanaoweza wafuatane nami, wamsute huko mtu huyo, akiwa ametenda neno lisilopasa!
6Alipokwisha kukaa kwao siku zisizopita nane au kumi, akatelemka kwenda Kesaria. Kesho yake akaketi katika kiti cha uamuzi, akaagiza, Paulo aletwe.
7Alipofika, Wayuda waliotelemka toka Yerusalemu wakamsimamia pande zote, wakamsingizia mambo mengi yaliyokuwa magumu, wasiweze kuyaonyesha kuwa ya kweli.
8Lakini Paulo akajikania akisema: Sikukosa wala Maonyo ya Wayuda, wala Patakatifu, wala Kaisari.
9Kwa kutaka kuwapendeza Wayuda Festo akamwuliza Paulo akisema: Unataka kupanda kwenda Yerusalemu, uhukumiwe huko mbele yangu kwa ajili ya mambo hayo?
10Paulo akasema: Ninasimama hapa penye kiti cha uamuzi cha Kaisari; ndipo panaponipasa kuhukumiwa. Wayuda hakuna, nilichowapotolea, kama nawe mwenyewe unavyojua.
11Basi, nikiwa mpotovu, nikatenda linalopasa kuuawa, sikatai kufa. Lakini masingizio yao hawa yakiwa hayana maana, hakuna tena anayeweza kunitia mikononi mwao, kwamba awapendeze. Nataka, nihukumiwe na Kaisari.
12Hapo Festo akasemezana nao wakuu, akajibu: Umetaka kuhukumiwa na Kaisari, utakwenda kwake Kaisari.
13Siku zilipopita, mfalme Agripa na Berenike wakafika Kesaria, wamwamkie Festo.
14Walipokaa huko siku nyingi, Festo akamwelezea mfalme mambo ya Paulo akisema: Yuko mtu aliyeachwa na Feliki kifungoni.[#Tume. 24:27.]
15Nilipokuwa Yerusalemu, watambikaji wakuu na wazee wa Wayuda walinitokea kwa ajili yake, wakataka mapatilizo yake yeye.
16Nikawajibu: Si desturi ya Kiroma kutoa mtu ye yote kwa mapenzi ya wengine; sharti kwanza mwenye kusutwa aonane uso kwa uso nao wasutaji wake, naye apate pa kujikania alilosutwa.
17Basi, walipokusanyika huku, sikuwakawilisha, ila kesho yake nikaketi katika kiti cha uamuzi, nikaagiza, yule mtu aletwe.
18Wasutaji walipomwinukia, vibaya nilivyoviwaza moyoni, hakuna, walichomsingizia hata kimoja;
19wakabishana naye tu kwa ajili ya tambiko lao wenyewe na kwa ajili ya mfu anayeitwa Yesu, kwani Paulo alisema: Yupo, anaishi.[#Tume. 18:15.]
20Nami kwa hivyo, nisivyojua mabishano kama hayo, nikamwuliza: Unataka kwenda Yerusalemu, uhukumiwe huko mambo hayo?
21Lakini Paulo akasema waziwazi, ya kuwa anataka kuwekwa, mpaka ahukumiwe na mfalme aliye mkuu peke yake; kwa hiyo nikaagiza, awekwe, mpaka nitakapomtuma kwake Kaisari.
22Agripa alipomwambia Festo: Nami mwenyewe nataka kumsikia mtu huyu akasema: Kesho utamsikia.[#Luk. 23:8.]
23Basi, kesho yake wakaja Agripa na Berenike, walikuwa wamejipamba kifalme vizuri, wakaingia penye hukumu pamoja na mabwana wakubwa na watu wenye cheo wa mjini. Festo alipoagiza, Paulo akaletwa.
24Ndipo, Festo aliposema: Mfalme Agripa, nanyi waume nyote mliopo hapa pamoja nasi, mtazameni mtu huyu! Kwa ajili yake yeye kundi lote zima la Wayuda limenitokea huko Yerusalemu na hapa vilevile; wakanipigia makelele ya kwamba: Haifai kabisa, huyu akiwapo vivyo hivyo![#Tume. 22:22; 25:2,7.]
25Lakini mimi nikaona, ya kuwa hakufanya neno lo lote linalopasa, auawe, naye mwenyewe akasema waziwazi: Nataka, nihukumiwe na mfalme aliye mkuu peke yake; kwa hiyo nikataka kumtuma huko.
26Lakini sinalo neno la kweli la kumwandikia bwana wangu la kwamba: Amekosa hivi na hivi. Kwa hiyo nimemleta mbele yenu, kwanza mbele yako wewe, mfalme Agripa, nipate la kuandika, mkiisha kuulizana naye.
27Kwani naona, ni upambavu kutuma mfungwa, pasipo kuyaeleza makosa yake.