Amosi 6

Amosi 6

Wakuu wa Yuda na wa Samaria watapatilizwa.

1Yatawapata watuliao Sioni nao wajivuniao mlima wa

Samaria,

ndio wakuu wa taifa lililo la kwanza,

nao walio mlango wa Isiraeli huwaendea!

2Haya! Nendeni Kalne, mkatazame!

Tena tokeni huko kwenda Hamati ulio mji mkuu!

Kisha shukeni Gati kwa Wafilisti, mwone!

Je? Ninyi m wema kuliko watu wa nchi hizo za kifalme?

Je? Mipaka yao siyo mikubwa kuliko mipaka yenu?

3Siku mbaya mnaiwazia kuwa mbali bado,

lakini kao la makorofi mnalileta kuwa karibu.

4Ninyi hulalia vitanda vya pembe za tembo

na kujinyosha katika magodoro yenu mororo!

Hula wana kondoo mkiwatoa makundini,

nao ndama mkiwatoa mazizini!

5Hujipigia mapango, tena hujitungia vinanda vinginevyo

kama Dawidi.

6Hunywa mvinyo katika mabakuli, tena hujipaka marashi

yapitayo yote;

lakini hivyo, Yosefu alivyovunjwa, haviwaumizi.

7Kwa hiyo watatekwa sasa na kuhamishwa, waende mbele ya

mateka;

ndipo, yatakapokomea makelele ya michezo yao

waliojinyosha hivyo.

8Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu Mwenye vikosi:

Bwana Mungu ameapa rohoni mwake kwamba:

Majivuno ya Yakobo hunitapisha, nikachukizwa na majumba

yake,

kwa sababu hii nitautoa huo mji pamoja nayo yote yaliyomo

mwake.

9Itakuwa, waume kumi watakaposazwa katika nyumba moja,

watakufa.

10Ndugu ya mtu apaswaye na kumteketeza mwenziwe

akimchukua, aitoe mifupa yake nyumbani,

kama anamwuliza aliomo nyumbani ndani: Yumo, uliye naye

humu?

atamjibu: Wamekwisha kufa!

Ndipo, atakapomwambia: Nyamaza kimya!

Kwani haifai kulikumbusha Jina la Bwana.

11Kwani mtaona: Bwana akiagiza,

ndipo, watakapozipiga nyumba kubwa, hata zibomoke,

nazo nyumba ndogo, hata ziatuke nyufa.

12Je? Farasi hupiga mbio mwambani? Au mtu atapalima na

ng'ombe?

Kwani mashauri yaliyo sawa mmeyapotoa, yawe maji ya

nyongo,

nayo yaliyotengenezwa, yaongoke, mmeyapotoa, yawe

uchungu.

13Mwafurahia kisicho kitu na kusema:

Hatukujipatia pembe kwa uwezo wetu sisi?

14Kwa hiyo ndivyo, asemavyo Bwana Mungu Mwenye vikosi:

Mtaniona, nikiwainulia taifa ninyi mlio mlango wa Isiraeli;

ndio, watakaowasonga ninyi kuanzia penye njia ya kwenda Hamati,

kufikisha penye mto wa nyikani.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania