The chat will start when you send the first message.
1Haya ndiyo maono, Bwana Mungu aliyonionyesha: Nimemwona, alivyotengeneza nzige hapo, mimea ya vuli ilipoanza kuchipuka; nayo ilikuwa ya majani ya vuli iliyochipuka, watu walipokwisha kumkatia mfalme majani ya ng'ombe.
2Ikawa, nzige walipokwisha kula majani ya nchi, nikasema: Bwana Mungu, waachilie! Yakobo atawezaje kusimama? Kwani yeye ni mdogo.
3Ndipo, Bwana Mungu alipoigeuza roho kwa ajili ya hayo naye Bwana akasema: Hayatakuwa.
4Hili ndilo ono, Bwana Mungu alilonionyesha: Nimeona, Bwana Mungu alivyouita moto kuja kumgombea. Nao ukala vilindi vikubwa vya maji, ukataka kula napo pa kulimia.
5Ndipo, niliposema: Bwana Mungu, acha hapo! Yakobo atawezaje kusimama? Kwani yeye ni mdogo.
6Ndipo, Bwana alipoigeuza roho kwa ajili ya hayo, naye Bwana Mungu akasema: Haya nayo hayatakuwa.
7Hili ndilo ono, alilonionyesha: Nimemwona Bwana Mungu, alivyosimama juu ya ukuta uliosimama sawasawa kwa kujengwa kwa kipimo cha timazi, naye alishika kipimo cha timazi mkononi mwake.
8Bwana akaniuliza: Unaona nini, Amosi? Nilipojibu: Kipimo cha timazi, Bwana akaniambia: Utaniona, nitakavyowapima walio ukoo wangu wa Isiraeli, sitaendelea tena kuwapita tu.[#Amo. 8:2; Yes. 34:11.]
9Vilima vya Isaka vitaangamizwa, napo patakatifu pote pa Isiraeli patabomolewa, nami nitawainukia walio mlango wa Yoroboamu kwa upanga.
10Ndipo, Amasia, mtambikaji wa Beteli, alipotuma kwa Yoroboamu, mfalme wa Isiraeli, kumwambia: Amosi anakuvurugia watu humu katika mlango wa Isiraeli, nchi haiwezi tena kuyavumilia maneno yake yote.[#Yer. 38:4.]
11Kwani haya ndiyo, Amosi anayoyasema: Yoroboamu atakufa kwa upanga, nao Waisiraeli watatekwa na kuhamishwa, watoke katika nchi yao.
12Kisha Amasia akamwambia Amosi: Wewe mchunguzaji, nenda zako kukimbia katika nchi ya Yuda, ukajilie mkate huko na kuwafumbulia maneno![#1 Sam. 9:9.]
13Lakini huku Beteli usitufumbulie tena maneno, kwani hapa ndipo patakatifu pa mfalme, nayo nyumba hii ni ya ufalme wote.
14Amosi akamjibu Amasia na kumwambia: Mimi si mfumbuaji wala mwana wa mfumbuaji, kwani nalikuwa mchunga ng'ombe, nikajitunzia mikuyu.[#Amo. 1:1.]
15Ndipo, Bwana aliponichukua, akanitoa penye ng'ombe, Bwana akaniambia: Nenda, uwafumbulie walio ukoo wangu wa Isiraeli!
16Sasa lisikie neno la Bwana! Wewe unasema: Usiwafumbulie Waisiraeli! Wala usiwahubiri walio mlango wa Isaka yatakayokuwa![#Amo. 2:12; 7:13.]
17Ni kwa sababu hii, Bwana akisema hivyo: Mkeo atakuwa mgoni humu mjini, nao wanao wa kiume na wa kike watauawa kwa upanga, nalo fungu lako la nchi litagawanywa kwa kupimwa na kamba. Nawe wewe utakufa katika nchi iliyo na mwiko wa kuikaa, nao Waisiraeli watatekwa na kuhamishwa, watoke katika nchi yao.