Wakolose 2

Wakolose 2

Paulo anawaonya, wasidanganyike.

1Kwani nataka, mlijue shindano langu kubwa, nililo nalo kwa ajili yenu na ya Walaodikia na kwa ajili yao wote wasioniona uso kwa uso kimwili; nalo ni hili:

2mioyo yao ipate kutulizwa, ikaunganishwa na kupendana, wapate kuzitwaa nazo mali zote, mtu azipatazo akiwa mwenye ujuzi mwingi, ni kwamba: Nao walitambue fumbo la Mungu na la Kristo.

3Mwake yeye ndimo, malimbiko yote ya werevu wa kweli na ya utambuzi yalimofichwa.[#Fano. 2:3-4; 1 Kor. 1:24,30.]

4Navisema hivi, mtu asiwadanganye akiwaambia maneno mazuri ya kuwashinda.[#Rom. 16:18.]

5Kwani mwili ukiwa hauko kwenu, moyo uko pamoja nanyi, ukaning'aa ukiona, mwonyekavyo, tena mjishupazavyo kumtegemea Kristo.[#1 Kor. 5:3; 14:40; Fil. 1:27.]

Kutahiriwa Kikristo.

6Basi, kama mlivyompokea Bwana Kristo Yesu, hivyo mwendelee kuwa wake,

7mkishusha mizizi mumo humo mwake, mkajengwa mlemle na kuongezwa nguvu za kumtegemea, kama mlivyofundishwa; hivyo mtayavumisha yale mema, mliyogawiwa.[#Ef. 2:22; 3:17.]

8Mjiangalie, mtu asije, akawateka akiwafundisha maneno ya ujuzi yaliyo ya udanganyi wa bure tu, hufanana na masimulio ya watu kama ya mambo yaliyo ya kwanza humu ulimwenguni, lakini siyo ya Kikristo.[#Kol. 2:16,20.]

9Kwani mwake Kristo ndimo mkaamo kimwili wingi wao yote yaliyo ya Kimungu.[#Yoh. 1:14,16.]

10Nanyi mkiwa naye huyapata hayo yote, maana yeye ni kichwa cha kila ukuu na cha kila nguvu.[#Ef. 1:21.]

11Tena mkiwa naye yeye hutahiriwa pasipo kutumia mikono ya mtu, maana huuvua mwili wa kimtu ulio wenye makosa, ndiko kutahiriwa Kikristo.[#Rom. 2:29; 1 Petr. 3:21.]

12Hapo, mlipobatizwa mmezikwa pamoja naye, tena papo hapo mmefufuliwa pamoja naye kwa nguvu ya kumtegemea, mwipatayo kwake, Mungu aliyemfufua katika wafu.[#Kol. 3:1; Rom. 6:4.]

13Nanyi mlikuwa wenye kufa kwa ajili ya makosa, nayo miili yenu ilikuwa haikutahiriwa hivyo, lakini aliwapa kuishi pamoja naye, akawaondolea makosa yote.[#Ef. 2:1-5.]

14Kisha akakifuta cheti kilichoandikwa maagizo, tusiyoyashika, ndicho kilichotusuta; akakiondoa hapo kati, akakipigilia msalabani.[#Ef. 2:15.]

15Nao wakuu wa wangavu akawavua ukuu wao na nguvu zao, akaonyesha waziwazi, walivyo, akawatembeza kama mateka.[#Kol. 1:13; 2:10.]

Kivuli cha mambo yanayokuja.

16Kwa hiyo mtu asiwaumbue kwa ajili ya kula au kunywa, wala kwa ajili ya kuacha kuzipa cheo sikukuu zo zote, ikiwa za miandamo ya mwezi au za mapumziko.[#Mat. 15:7-9; Rom. 14:1-12.]

17Mambo hayo ni kivuli tu cha mambo yaliyotaka kutokea, lakini yametimia kimwili, Kristo alipokuja.[#Ebr. 8:5; 10:1.]

18Mtu asiwanyang'anye tunzo lenu akiwataka, mfuatane naye kujinyenyekeza na kuwatambikia malaika! Hujiwazia kwamba: Yako, aliyoyaona, kisha hujikazia yayo hayo akijitutumua bure kwa mawazo ya mwili wake,[#Kol. 2:23.]

19asishikamane naye aliye kichwa, aliye mwenye kuuunganisha mwili wote, ukitiwa nguvu kwa fundo na viungo, upate kumkulia Mungu.[#Ef. 4:15-16.]

Miiko ni ya bure.

20Kama mmekufa pamoja naye Kristo mkiyaacha yale mambo yaliyo ya kwanza humu ulimwenguni, kwa nini mwataka tena kupewa miiko kama wenye kuukalia ulimwengu huu?[#Gal. 4:3,9.]

21Mwaambiwa: Usivishike! wala: Usivionje! wala: Usiviguse hivi na hivi!

22Navyo vyote vimewekwa, vitumike, kisha vioze. Kwa hiyo yale maagizo na mafundisho ni ya kimtu tu;[#Yes. 29:13; Mat. 15:9.]

23kweli watu husema: Ni ya werevu wa kweli, wakiyachagua matumizi yao ya Mungu na unyenyekevu wao, tena wakiinyima miili yao yaipasayo, lakini yote ni kazi za bure tu, maana zikiisha, huzitimiza tamaa zote za miili.[#Rom. 13:14; 1 Tim. 4:3.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania