Mpiga mbiu 1

Mpiga mbiu 1

Vitu vyote vya huku nchini ni vya bure.

2Mpiga mbiu asema: Yote ni ya bure kabisa, kweli yote ni ya bure kabisa, yote pia ni ya bure.

3Mtu hupata nini kwa masumbuko yake yote, anayojisumbua chini ya jua?[#Mbiu. 2:22.]

4Kizazi kimoja kikienda zake, kingine huja, lakini nchi hukaa kale na kale.[#Sh. 90:3.]

5Jua hucha, tena huchwa, kisha hupakimbilia pake pa macheo yake.

6Upepo ukienda kusini, kisha hugeuka kwenda kaskazini; ndivyo, upepo unavyojiendea na kugeukageuka. Kwa kugeukageuka kwake upepo hurudia hapo, ulipotokea.

7Mito yote huenda baharini, lakini bahari haijai; papo hapo, mito inaposhika njia zao, ndipo, inapojiendea na kuishika njia ileile.

8Mambo yote huchokesha, mtu asiweze kuyasema yote, wala macho hayashibi kwa kuyatazama, wala masikio hayajai kwa kuyasikia.[#Sh. 90:10.]

9Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako tena, nayo yaliyofanywa ndiyo yatakayofanywa tena; hakuna jipya litakalotokea chini ya jua.

10Kama litatokea, watu wanalotaka kulisema kwamba: Hili ni jipya kweli, limekwisha kuwako siku za kale kabisa zilizokuwako mbele yetu.

11Ni hivyo tu, wa kwanza hawakumbukwi, vivyo nao wa nyuma watakaokuwako hawatakumbukwa kwao watakaokuwako nyuma yao.

12Mimi Mpiga mbiu nilikuwa mfalme wa Isiraeli huko Yerusalemu.[#Mbiu. 1:1.]

13Nikajipa moyo, kuyatafuta na kuyapeleleza kwa werevu wa kweli yote pia yanayofanyika chini ya mbingu; ni sumbuko baya, Mungu alilowapa wana wa Adamu kulisumbukia.

14Nikayatazama yote yanayofanywa chini ya jua, nikayaona yote kuwa ya bure, kuwa kuukimbilia upepo.

15Yapotokayo hayanyosheki, wala yasiyokuwako hayahesabiki.

16Naliwaza moyoni mwangu kwamba: Mimi nimejipatia werevu wa kweli mwingi, nikauongeza kuwa mwingi zaidi kuupita wa watu wote waliokuwako mbele yangu Yerusalemu, kweli moyo wangu ulipata werevu wa kweli na juzi mwingi.[#Mbiu. 7:13.]

17Lakini nilipojipa moyo kujua, jinsi werevu wa kweli ulivyo, tena kujua, jinsi upumbavu na ujinga ulivyo, ndipo, nilipojua, ya kuwa hayo nayo ni kuukimbilia upepo.[#Mbiu. 2:12; 7:25.]

18Kwani werevu mwingi ulipo, yapo nayo masikitiko mengi, naye aongoezaye ujuzi huongeza nayo maumivu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania