Esteri 4

Esteri 4

Masikitiko na mifungo ya Wayuda.

1Mordekai alipoyajua hayo yote yaliyofanyika, Mordekai akazirarua nguo zake, akavaa gunia na majivu, akatokea mjini katikati, akaomboleza maombolezo makuu yenye uchungu.

2Hivyo akaja mpaka hapo penye lango la mfalme, kwani mtu aliyevaa gunia hakuwa na ruhusa ya kuingia langoni kwa mfalme.

3Katika kila jimbo moja mahali po pote lile neno la mfalme lilipotangazwa, masikitiko makubwa yakawapata Wayuda, wakafunga mifungo pamoja na kulia machozi na kuomboleza; wengi wakakjitandikia magunia na majivu ya kuyalalia.

4Vijana wa kike wa Esteri na watumishi wake wa nyumbani walipokuja kumsimulia mambo hayo, mke wa mfalme akaumia sana moyoni, akatuma nguo kwake Mordekai, azivae na kuliondoa gunia lake, lakini hakukubali.

5Ndipo, Esteri alipomwita Hataki, ni mmoja wao watumishi wa nyumbani, mfalme aliowatoa wa kuwa naye, akamwagiza kumwuliza Mordekai, amjulishe sababu na maana ya mambo hayo.

6Hataki akatoka, akamkuta Mordekai uwanjani mjini langoni kwa mfalme.

7Mordekai akamsimulia yote yaliyompata, hata hesabu ya fedha, Hamani alizozisema kwamba atazipima, azitie katika malimbiko ya mfalme, atakapowaangamiza Wayuda.[#Est. 3:9.]

8Kisha akampa karatasi iliyoandikwa ile mbiu iliyotangazwa Susani ya kuwatowesha, amwonyeshe Esteri na kumsimulia yote, kisha amwagize kwenda kwa mfalme kumlalamikia na kuuombea ukoo wake kwake.

9Hataki akaja, akamsimulia Esteri maneno ya Mordekai.

10Esteri naye akamwambia Hataki na kumwagiza, amwambie Mordekai:

11Watumishi wote wa mfalme na watu wote wa majimbo ya mfalme wanayajua haya: kila mtu, kama ni mwanamume au mwanamke aingiaye kwa mfalme katika ua wa ndani, asipokuwa ameitwa, hana budi kuuawa kwa ile amri moja ya mfalme; atakayepona ni yule tu, mfalme ampungiaye kwa bakora yake ya dhahabu. Nami sikuitwa kuingia kwa mfalme, sasa ni siku thelathini.[#Est. 5:2; 8:4.]

12Walipomsimulia Mordekai haya maneno ya Esteri.

13Mordekai akaagiza kumrudishia Esteri jibu la kwamba: Usijiwazie, ya kuwa kwa kukaa jumbani mwa mfalme utapona peke yako katika Wayuda wote.

14Lakini ukitaka kunyamaza kimya katika siku kama hizi, wokovu wa kuwaponya Wayuda utatoka mahali pengine, lakini wewe na mlango wa baba yako utaangamia; labda ni kwa ajili ya siku kama hizi, ukiwa mkewe mfalme.[#1 Mose 45:7.]

15Esteri akaagiza kumrudishia Mordekai jibu la kwamba:

16Nenda, uwakusanye Wayuda wote wanaopatikana humu Susani! Kisha mfunge mfungo kwa ajili yangu mimi na kuniombea, msile, wala msinywe siku tatu usiku na mchana! Mimi nami nitafunga hivyo pamoja na vijana wangu wa kike, kisha nitaingia kwake mfalme, ingawa ni mwiko. Kama ni kuangamia, basi, na niangamie![#2 Fal. 7:4.]

17Ndipo, Mordekai alipokwenda zake, akafanya yote, kama Esteri alivyomwagiza.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania