2 Mose 26

2 Mose 26

Mapazia ya Kao Takatifu.

(1-14: 2 Mose 36:8-19.)

1Kao lenyewe utalitengeneza kwa mapazia kumi yaliyoshonwa kwa nguo za bafta ngumu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu, nayo yawe yenye mifano ya Makerubi, kama mafundi wa kufuma wanavyojua kuitengeneza, nawe uwafanyishe!

2Urefu wa pazia moja uwe mikono ishirini na minane, nao upana wake uwe mikono minne; kila pazia moja liwe lenye kipimo hiki kimoja, kiwe cha mapazia yote.

3Mapazia matano yaungwe kila moja na mwenzake kuwa moja, nayo matano ya pili yaungwe vivyo hivyo kila moja na mwenzake kuwa moja.

4Kisha ushone vitanzi vya nguo nyeusi za kifalme penye upindo wa nje wa kila pazia moja hapo, litakapoungwa na jingine; vivyo hivyo uvitie napo penye upindo wa nje wwa kila pazia la pili hapo, litakapoungwa nalo la kwanza.

5sharti ushone vitanzi hamsini katika kila pazia moja upande mmoja, na tena vitanzi hamsini katika upindo wa kila pazia la pili upande huo utakaoungwa na pazia la kwanza, hivyo vitanzi vielekeane kila moja na mwenzake.

6Kisha ufanye vifungo vya dhahabu hamsini, upate kuyafunga mapazia kila moja na mwenzake kwa hiyo vifungo, kao hilo liwe moja.

7Kisha ufanye mapazia ya nywele za mbuzi kuwa hema juu ya kao lenyewe. Utengeneze mapazia kumi na moja.

8Urefu wa kila pazia uwe mikono thelathini, nao upana wa kila pazia moja moja uwe mikono minne; hiki kipimo kimoja kiwe chao mapazia yote kumi na moja.

9Kisha uyaunge mapazia matano kuwa moja, nayo yale sita uyaunge kuwa moja, ukilikunja hilo pazia la sita kuwili hapo mbele ya hema.

10Kisha ushone vitanzi hamsini katika upande wa nje wa kila pazia moja hapo, litakapoungwa na jingine; vivyo hivyo uvitie napo penye upindo wa nje wa kila pazia la pili hapo, litakapoungwa nalo la kwanza.

11Kisha ufanye vifungo vya shaba hamsini, hivyo vifungo uvitie katika vitanzi, upate kuliunga hilo hema, liwe moja.

12Nacho kipande kitakachozidi cha mapazia ya hema cha kuangukia pembeni, hiyo nusu ya pazia itakayoangukia pembeni na iangukie upande wa nyuma wa kao.

13Nao urefu wa mapazia ya hema utakaozidi ndio mkono mmoja huku na huko, basi, huo mkono na uangukie kila upande wa kao wa kulikingia pembeni.

14Kisha sharti utengeneze chandalua cha hema kwa ngozi nyekundu za madume ya kondoo, tena utengeneze chandalua cha pili kwa ngozi za pomboo kuwa juu yake.

Mbao za kao lenyewe.

(15-25: 2 Mose 36:20-30.)

15Tena utengeneze mbao za kao lenyewe za migunga, nazo zisimame.

16Urefu wa kila ubao uwe mikono kumi, nao upana wake kila ubao mmoja uwe mkono mmoja na nusu.

17Kila ubao mmoja uwe na vigerezi viwili, navyo vitazamane kila kimoja na mwenzake. Vivyo hivyo uvitengenezee kila ubao mmoja wa kao lenyewe.

18Hizo mbao za kao lenyewe uzitengeneze kuwa ishirini upande wa kusini, ndio upande wa juani.

19Tena chini ya hizi mbao ishirini utengeneze viguu vya fedha arobaini, viwe viguu viwili chini ya kila ubao mmoja viguu viwili vya kivitilia vigerezi vyake viwili.

20Hata upande wa pili wa kao, ndio upande wa kaskazini vilevile mbao ishirini

21na viguu arobaini vya fedha, viguu viwili chini ya kila ubao mmoja, vivyo hivyo viwili chini ya kila ubao mmoja.

22Lakini upande wa nyuma wa kao unaoelekea baharini uutengenezee mbao sita.

23Tena utengeneze mbao mbili za pembeni mle kaoni upande wa nyuma.

24Nazo ziwe kama pacha, toka chini viendelee pamoja zote nzima mpaka juu penye pete la kwanza. Hivi ndivyo, zitakavyokuwa mbao zote mbili za hizo pembe mbili za nyuma.

25Hivyo zote pamoja zitakuwa mbao nane, navyo viguu vya fedha vitakuwa kumi na sita, viguu viwili chini ya kila ubao mmoja, viwe viguu viwili chini ya kila ubao mmoja.

Misunguo.

(26-30: 2 Mose 36:31-34.)

26Kisha utengeneze misunguo ya migunga, mitano ya mbao za upande mmoja wa kao,

27tena misunguo mitano ya mbao za upande wa pili wa kao, tena misunguo mitano ya upande wa nyuma wa kao unaoelekea baharini.

28Nao msunguo wa katikati ulio katikati ya mbao uupitishe toka mwisho wa huku hata mwisho wa huko.

29Nazo mbao uzifunikize dhahabu, nayo mapete yao uyatengeneze kwa dhahabu, yawe ya kutilia misunguo, nayo misunguo uifunikize dhahabu.

30Kisha ulisimamishe hilo kao, liwe kama mfano ule ulioonyeshwa mlimani.[#2 Mose 25:9.]

Mapazia mawili.

(31-37: 2 Mose 36:35-38.)

31Tena utengeneze pazia lililoshonwa kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu. Fundi wa kufuma na alitengeneze kuwa lenye mifano ya Makerubi.[#Mat. 27:51.]

32Kisha ulitungike juu penye nguzo nne za migunga zilizofunikizwa dhahabu, tena ziwe zenye vifungo vya dhahabu, chini ziwe zimesimikwa katika miguu minne ya fedha.

33Hili pazia ulitungike chini ya hivyo vifungo, kisha uliingize Sanduku la Ushahidi mbele yake pazia, hilo pazia liwatengee Patakatifu na Patakatifu Penyewe.[#2 Mose 26:6-11; Ebr. 9:3-12.]

34Kisha ukiweke kile kifuniko (Kiti cha Upozi) juu ya Sanduku la Ushahidi pale Patakatifu Penyewe.[#2 Mose 25:21.]

35Nayo ile meza iweke upande wa huku wa pazia, na kinara kile kiweke kuilekea meza upande wa kusini wa kao, lakini meza uiweke upande wa kaskazini.[#2 Mose 40:22.]

36Kisha hapo pa kuingia hemani uweke guo kubwa lililotengenezwa kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu, lifumwe nao wanaojua kweli kufuma kwa nyuzi za rangi.

37Guo hilo ulitengenezee nguzo tano za migunga, nazo uzifunikize dhahabu, uzitie vifungo vya dhahabu, kisha uzitengenezee miguu ya shaba mitano kwa kuyeyusha shaba.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania