The chat will start when you send the first message.
1Tengeneza nayo meza ya kuvukizia mavukizo, uitengeneze nayo kwa migunga.
2Urefu wake uwe mkono mmoja, nao upana wake uwe mkono mmoja, pande zote nne ziwe sawa, nao urefu wake wa kwenda juu uwe mikono miwili.
3Uifunikize dhahabu tupu juu yake na kando yake pande zote na pembe zake, kisha uzungushe juu yake taji la dhahabu pande zote.
4Kisha uitengenezee mapete mawili ya dhahabu, uyatie chini ya taji pande zake mbili penye mbavu zake mbili, yawe ya kutilia mipiko ya kuichukulia.
5Nayo mipiko uitengeneze kwa migunga, kisha nayo uifunikize dhahabu.
6Kisha uiweke upande wa huku wa pazia linaloning'inia na kulielekea Sanduku la ushahidi, mbele ya kiti cha upozi kilichoko juu yake Sanduku la Ushahidi nitakapokutana na wewe.[#2 Mose 25:22.]
7Naye Haroni na avukize juu yake mavukizo yanukayo vizuri; kila kunapokucha akizitengeneza taa za kinara na ayavukize.[#Sh. 141:2; Ufu. 5:8.]
8Hata Haroni atakapoziwasha hizo taa saa za jioni na ayavukize tena, mavukizo yavukizwe mbele ya Bwana siku zote nao walio wa vizazi vyenu.
9Msivukize juu yake manukato mageni, wala msitoe juu yake ng'ombe za tambiko za kuteketezwa wala kipaji cha tambiko.[#3 Mose 10:1.]
10Kila mwaka mara moja Haroni na azipatie upozi pembe zake kwa damu ya ng'ombe ya tambiko ya weuo; mara moja tu kila mwaka na aipatie upozi kwao walio wa vizazi vyenu, maana ni takatifu yenyewe kwa kuwa yake Bwana.[#3 Mose 16:18; 2 Mose 29:37.]
11Bwana akamwambia Mose kwamba:
12Ukivihesabu vichwa vyao wana wa Isiraeli, watakapokaguliwa, na wamtolee Bwana makombozi ya kuzikomboa roho zao, kila mtu yake kwa kukaguliwa, wasipatwe na pigo lo lote kwa kukaguliwa.
13Kwa hiyo kila atakayefika kukaguliwa sharti atoe nusu ya sekeli, ndio fedha zitumikazo Patakatifu, ambazo sekeli moja ni gera ishirini, ndio fedha moja ya thumuni nane. Nusu ya fedha hiyo iwe kipaji cha tambiko cha kumnyanyulia Bwana.
14Kila atakayefika kukaguliwa mwenye miaka ishirini na zaidi sharti mnyanyulie Bwana hicho kipaji cha tambiko.
15Mwenye mali asilipe zaidi, wala mnyonge asiipunguze hiyo nusu ya fedha kuwa kipaji cha tambiko cha kumnyanyulia Bwana, wajipatie upozi.
16Kisha uzichukue hizo fedha za mapoza, utakazowatoza wana wa Isiraeli, uzitumie za utumishi wa hema la Mkutano; ndivyo, zitakavyokuwa za kumkumbusha Bwana, awakumbuke wana wa Isiraeli, azipatie roho zenu upozi.
17Bwana akamwambia Mose kwamba:
18Tengeneza birika la shaba lenye wekeo lake la shaba, liwe la kuogea, uliweke katikati ya Hema la Mkutano na meza ya kutambikia, kisha ulitie maji.[#2 Mose 38:8.]
19Haroni na wanawe waoshe humo mikono na miguu yao.
20Watakapoingia katika Hema la Mkutano wajiogeshe majini, wasife! Au watakapoikaribia meza ya Bwana, watumikie hapo na kumchomea Bwana ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa,
21na waioshe mikono na miguu yao, wasife! Maongozi haya na yawe ya kale na kale kwake na kwa wazao wake na kwa vizazi vyao.
22Bwana akamwambia Mose kwamba:
23Jichukulie manukato yaliyo mazuri mno: manemane mabichi sekeli 500, ndio ratli 20, tena nusu yao dalasini zinukazo vizuri sekeli 250, ndio ratli 10, tena vichiri vinukavyo vizuri sekeli 250, ndio ratli 10,
24na karafuu sekeli 500, ndio ratli 20 zilizopimwa kwa mizani ya Patakatifu, tena pishi moja ya mafuta ya chekele.
25Kisha uyatengeneze kuwa mafuta matakatifu ya kupaka kwa kuchanganya mafuta na manukato, kama mtengeneza manukato aliye fundi anavyojua kuyatengeneza, yapate kuwa kweli mafuta matakatifu ya kupaka.[#2 Mose 37:29.]
26Kisha kwa hayo mafuta ulipake Hema la Mkutano na Sanduku la Ushahidi,
27na meza na vyombo vyake vyote na kinara na vyombo vyake na meza ya kuvukizia,
28na meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko na vyombo vyake vyote na birika na wekeo lake,
29uvitakase hivyo, vipate kuwa vitakatifu vyenyewe. Kisha kila atakayevigusa sharti awe ametolewa kuwa mtakatifu.[#2 Mose 30:10.]
30Naye Haroni na wanawe uwapake mafuta, uwatakase, wapate kuwa watambikaji wangu.[#2 Mose 29:7.]
31Nao wana wa Isiraeli uwaambie kwamba: Hayo mafuta ya kupaka sharti yawe matakatifu kwa vizazi vyenu, kwa kuwa ni yangu.
32Msiyamiminie mwilini mwa mtu, wala msitengeneze yaliyo sawa kama hayo, kwani ndiyo matakatifu, nayo sharti yawe matakatifu kwenu.
33Mtu atakayechanganya mafuta kuwa kama hayo au atakayeyapaka mtu mgeni sharti ang'olewe kwao walio ukoo wake.
34Bwana akamwambia Mose: Chukua viungo vinukavyo vizuri: liwa na udi na sandarusi, ndio viungo vinukavyo vizuri, tena uvumba ulio safi, vyote viwe kipimo kimoja tu.
35Uvitengeneze kuwa mavukizo, kama mtengeneza manukato aliye fundi anavyojua kuyatengeneza na kutia chumvi humo, yapate kutakata na kuwa matakatifu.
36Kisha uchukue humo kidogo, uyaponde sana, yawe kama uvumbi, kisha uchukue humo kidogo kuyaweka mbele ya Sanduku la Ushahidi katika Hema la Mkutano, nitakamokutana na wewe. Hayo mavukizo sharti yawe kwenu matakatifu yenyewe.
37Mavukizo mengine mtakayoyatengeneza, msiyatengeneze kuwa kama hayo, ila hayo sharti yawe matakatifu kwenu kwa kuwa yake Bwana.
38Mtu atakayetengeneza mavukizo kama hayo ya kuyavukiza sharti ang'olewe kwao walio wa ukoo wake.