The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose: Nenda, uondoke hapa, wewe na watu hawa, niliowatoa katika nchi ya Misri, uwapeleke katika nchi ile, niliyomwapia Aburahamu na Isaka na Yakobo kwamba: Nchi hii nitawapa wao wa uzao wako.[#2 Mose 32:13; 1 Mose 12:7.]
2Nami nitamtuma malaika wangu, akutangulie; tena nitawafukuza Wakanaani na Waamori na Wahiti na Waperizi, Wahiwi na Wayebusi.[#2 Mose 32:34.]
3Nchi ile ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali. Mwenyewe sitakuja kwenda katikati yenu, kwani m watu wenye kosi ngumu nisije kuwala njiani.[#2 Mose 32:9-10.]
4Watu walipolisikia hili neno baya wakasikitika, wala hakuonekana mtu aliyeyavaa mapambo yake,
5kwa kuwa Bwana alimwambia Mose: Waambie wana wa Isiraeli: Ninyi m watu wenye kosi ngumu; kama ningekuwa katikati yenu kitambo kimoja tu, ningewamaliza. Kwa hiyo sasa jipambueni mapambo yenu, nijue, nitakavyowafanyizia!
6Kwa hiyo wana wa Isiraeli wakayavua mapambo yao huko mlimani kwa Horebu.[#Yona 3:6.]
7Mose akaambiwa, lile Hema alichukue kila mara, alipige nje ya makambi, iwe mbali ya makambi, nalo aliite Hema la Mkutano, kila atakayemtafuta Bwana atoke kwenda kwenye Hema la Mkutano lililoko nje ya makambi.[#2 Mose 29:42.]
8Napo, Mose atakapotoka kwenda kwenye Hema, watu wote na wainuke kusimama pa kuyaingilia mahema yao, watazame nyuma yake, hata aingie Hemani!
9Tena itakuwa, Mose atakapoingia Hemani, lile wingu lililo kama nguzo litashuka na kusimama hapo pa kuliingilia Hema, Bwana akisema na Mose.[#2 Mose 13:21.]
10Watu wote watakapoliona hilo wingu lililo kama nguzo, likisimama hapo pa kuliingilia Hema, ndipo watu wote wainuke, wajiangushe chini kila mtu pa kuliingilia hema lake.
11Bwana atakapokwisha kusema na Mose uso kwa uso, kama mtu anavyosema na mwenzake, Mose na arudi makambini; lakini mtumishi wake Yosua, mwana wa Nuni, aliye kijana bado, asiondoke mle Hemani.[#2 Mose 33:20; 4 Mose 12:8; 5 Mose 34:10.]
12Mose akamwambia Bwana: Tazama, wewe unaniambia: Wapeleke watu hawa! Lakini hujanijulisha bado, kama ni nani, utakayemtuma kwenda na mimi; tena ulisema: Ninakujua kwa jina, maana umeona upendeleo machoni pangu.[#2 Mose 33:2-5.]
13Sasa kama nimeona kweli upendeleo machoni pako, unijulishe njia yako, nikujue, kwa kuwa niliona upendeleo machoni pako. Tena watazame watu hawa, kwani ndio taifa lako.[#Sh. 103:7.]
14Akamwambia: Uso wangu utakwenda na wewe, ukuongoze.
15Naye akamwambia: Uso wako usipokwenda na sisi, usitutoe huku kwenda huko!
16Ijulikane kwa nini, ya kuwa tumeona upendeleo machoni pako mimi nao walio ukoo wako, isipokuwa, wewe ukienda na sisi, tujulikane mimi nao walio ukoo wako, ya kuwa tumechaguliwa katika makabila yote yaliyoko juu ya nchi?[#5 Mose 4:6-8.]
17Bwana akamwambia Mose: Neno hili, ulilolisema, nitalifanya nalo, kwani umeona upendeleo machoni pangu, nami ninakujua kwa jina.[#2 Mose 33:12; 2 Tim. 2:19.]
18Mose akaomba: Nionyeshe utukufu wako!
19Akaitikia kwamba: Nitaupitisha wema wangu wote machoni pako, nalo Jina langu la Bwana nitalitamka kwa sauti kuu masikioni pako. Mimi nitakayemhurumia, nitamhurumia kweli; nitakayemwonea uchungu, nitamwonea uchungu wa kweli.[#Rom. 9:15.]
20Akamwambia tena: Lakini uso wangu huwezi kuuona, kwani hakuna mtu atakayekuwa yu hai akiisha kuniona.[#1 Mose 32:30; Yes. 6:5; 1 Tim. 6:16.]
21Bwana akamwambia tena: Nitakuonyesha mahali, ndipo upate kusimama juu ya mwamba.[#1 Fal. 19:8-13.]
22Hapo, utukufu wangu utakapopita, nitakuweka katika pango la huo mwamba na kukukingia kwa mkono wangu, mpaka nitakapokwisha kupita.[#2 Mose 34:5-6; 24:11.]
23Nitakapouondoa mkono wangu, utaweza kutazama nyuma yangu, lakini uso wangu mtu hawezi kuuona.