The chat will start when you send the first message.
1Mose akaukutanisha mkutano wote wa wana wa Isiraeli, akawaambia: Haya maneno ndiyo, Bwana aliyowaagiza kuyafanya.
2Kazi na zifanywe siku sita, lakini siku ya saba sharti iwe takatifu kwenu kuwa siku ya Bwana ya kupumzika kabisa. Kila atakayefanya siku hiyo kazi yo yote hana budi kuuawa.[#2 Mose 20:8-11; 31:12-17.]
3Msiwashe moto siku ya mapumziko po pote, mtakapokaa.
4Kisha Mose akauambia mkutano wote wa wana wa Isiraeli kwamba: Hili nalo ni neno, Bwana aliloliagiza kwamba:
5Mchangieni Bwana kwenu vipaji vya tambiko, kila mtu na avilete hivyo vipaji vya tambiko vya kumpa Bwana, kama moyo wake unavyomtuma: dhahabu na fedha na shaba,[#2 Mose 25:2.]
6na nguo za kifalme na nywele za mbuzi,
7na ngozi nyekundu za madume ya kondoo na ngozi za pomboo na migunga,
8na mafuta ya taa na manukato ya kutengeneza mafuta ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri,
9na vito vya oniki na vito vingine vya kutia katika kisibau cha mtambikaji mkuu na katika kibati cha kifuani.
10Nao wote walio wenye werevu wa kweli mioyoni kwenu na waje kuyatengeneza yote, Bwana aliyoyaagiza:
(11-19: 2 Mose 31:7-11.)11Kao lenyewe pamoja na Hema lake na chandalua chake na vifungo vyake na mbao zake na misunguo yake na nguzo zake na miguu yao;
12lile Sanduku (la ushahidi) na mipiko yake na Kiti cha Upozi na pazia la kukifungia;
13meza na mipiko yake na vyombo vyake vyote na mikate ya kuwa usoni pa Bwana;
14kinara cha kuangazia na vyombo vyake na taa zake na mafuta ya kuwasha;
15meza ya kuvukizia na mipiko yake na mafuta ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri na nguo za pazia ya hapo pa kuliingilia Kao;
16meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko pamoja na wavu wake wa shaba na mipiko yake na vyombo vyake vyote na birika na wekeo lake;
17nguo za ua na nguzo zake na miguu yake na pazia la langoni kwa ua;
18mambo za Kao na mambo za ua pamoja na kamba zao;
19na nguo nzuri za mapazia za kutumiwa Patakatifu na mavazi matakatifu ya mtambikaji Haroni na mavazi ya wanawe, wapate kuwa watambikaji.
20Ndipo, watu wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli walipotoka kwa Mose.
21Kisha watu wote wakaja kwa kuhimizwa na mioyo yao na kwa kutumwa na roho zao, wakaleta vipaji vyao vya tambiko vya kumpa Bwana vya kulitengeneza Hema la Mkutano na vya kutumiwa kwa kazi zake zote na vya nguo za Patakatifu.[#2 Mose 36:3; 1 Mambo 29:5,9; 2 Kor. 9:7.]
22Wakaja waume kwa wake, maana wote walitumwa na mioyo yao, wakaleta vipini na mapete ya masikioni na pete za vidoleni na mapambo yo yote ya dhahabu; tena kila mtu akaleta dhahabu kuwa vipaji vya tambiko vya kupitishwa motoni vya kumpa Bwana.
23Kila mtu aliyeona kwake nguo ya kifalme nyeusi au nyekundu au nguo ya bafta au nywele za mbuzi au ngozi nyekundu za madume ya kondoo au ngozi za pomboo, akazileta.
24Nao wote waliotaka kutoa fedha na shaba kuwa vipaji vyao vya tambiko wakazileta kumpa Bwana hivyo vipaji vya tambiko. Nao wote walioona kwao miti ya migunga iliyofaa kutumiwa kwa kazi yo yote wakaileta.
25Nao wanawake waliokuwa wenye ujuzi huo mioyoni mwao wakasokota nyuzi kwa mikono yao, kisha wakazileta hizo nyuzi, walizozisokota za kufuma nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na nguo za bafta.
26Nao wanawake wote waliohimizwa na mioyo yao kwa kuijua vema kazi hiyo wakasokota nywele za mbuzi.
27Nao wakuu wakaleta vito vya oniki na vito vingine vya kutiwa katika kisibau cha mtambikaji mkuu na katika kibati cha kifuani,
28na manukato na mafuta ya taa na ya kutengeneza mafuta ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri.
29Hivyo wakachanga wana wa Isiraeli wote, waume kwa wake, waliotumwa na mioyo yao kuyapeleka yafaayo ya kufanya kazi zote, Bwana alizoziagiza kinywani mwa Mose, zifanywe.
30Kisha Mose akawaambia wana wa Israeli: Tazameni, Bwana amemwita kwa jina lake Besaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa shina la Yuda;
31akamjaza roho yake ya Kimungu na kumgawia werevu wa kweli na utambuzi na ujuzi wa kutengeneza kazi yo yote,
32ajue kuvumbua kazi nzuri za ufundi wa kufua dhahabu na fedha na shaba;
33naye ni fundi wa kukatakata vito na kuvizungushia vikingo na fundi wa kuchora miti na fundi wa kufanya kazi zote za ufundi.
34Tena akampa moyoni mwake uwezo wa kufundisha wengine, yeye na mwenzake Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa shina la Dani.
35Mioyo yao aliijaza werevu wa kweli, wafanye kazi zo zote: kuchora kwa ufundi ulio werevu wa kweli, kufuma nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na nguo za bafta, kama mafundi wa kufuma nguo wanavyojua, kufanya kazi zote pia, hata kuvumbua kazi nzuri zisizofanyika bado.