The chat will start when you send the first message.
1Zile nguo za kifalme nyeusi na nyekundu walizitumia za kutengeneza mavazi mazuri ya kutumikia Patakatifu, wakayatengeneza hayo mavazi matakatifu ya Haroni, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
2Kisha walikitengeneza kisibau kwa dhahabu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu.
3Hizo dhahabu wakazisanasana kuwa mabati membamba, kisha wakayapasuapasua kuwa nyuzi, ziwezekane kufumwa pamoja na nyuzi za nguo za kifalme nyeusi na nyekundu, tena na nyuzi za bafta, kazi hii ilikuwa kazi ya ufundi wa kweli.
4Hicho kisibau kilikuwa chenye vipande viwili vilivyounganika mabegani, penye ncha zake mbili ndipo, kilipofungika.
5Nayo masombo yake ya kukifunga kifuani pake yalikuwa ya kazi iyo hiyo: yalitengenezwa kwa dhahabu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
6Kisha wakatengeneza vito viwili vya oniki, wakavizungushia vikingo vya dhahabu vya kuvishika, nayo majina ya wana wa Isiraeli yakachorwa humo, kama machoro ya muhuri yanavyochorwa.
7Kisha akavibandika hivyo vito penye vile vipande viwili vya mabegani vya kisibau kuwa vito vya kumbukumbushia wana wa Isiraeli, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
8Kisha wakakitengeneza kibati cha kifuani, nacho kilikuwa kazi ya ufundi wa kweli kama ile kazi ya kisibau, nacho kilitengenezwa kwa dhahabu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu.
9Pande zake zote zilikuwa sawasawa, tena hicho kibati kilikuwa kimekunjwa kuwa kuwili; urefu wake ulikuwa shibiri, nao upana wake ulikuwa shibiri, tena kilikuwa kimekunjwa kuwa kuwili.
10Wakakijaza vito na kuviweka kuwa mistari minne ya vito. Mstari wa kwanza: sardio, topazio na sumarato; ndio mstari wa kwanza.
11Mstari wa pili: almasi nyekundu, safiro na yaspi;
12mstari wa tatu: hiakinto, akate na ametisto;
13mstari wa nne: krisolito, oniki na berilo. Navyo vilipotiwa vyote vilikuwa vimezungushiwa vikingo vya dhahabu vya kuvishika.
14Hivyo vito vilikuwa kumi na viwili kwa hesabu ya majina ya wanawe Isiraeli vikiyafuata hayo majina yao, kila kimoja chao kilipata jina lake moja katika hayo mashina kumi na mawili, lilikuwa limechorwa humo, kama kazi ya muhuri ilivyo.
15Tena wakatengeneza kwa dhahabu tupu vikufu vilivyofanana na kamba zilizosokotwa, wakavitia penye kibati cha kifuani.
16Kisha wakatengeneza vipini viwili vya dhahabu na pete mbili za dhahabu, wakazitia hizo pete mbili penye zile ncha mbili za juu za kibati cha kifuani.
17Kisha hivyo vikufu viwili vya dhahabu vilivyofanana na kamba wakavifunga katika zile pete mbili penye zile ncha za juu za kibati cha kifuani.
18Kisha hiyo miisho mingine miwili ya hivyo vikufu viwili vilivyofanana na kamba wakaifunga katika vile vikingo viwili vya dhahabu, kisha wakavifunga penye vipande vya mabegani vya kisibau upande wake wa mbele.
19Kisha wakatengeneza tena pete mbili za dhahabu, wakazitia penye zile ncha mbili za chini za kibati cha kifuani katika upindo wake ulioko upande wa ndani uliokielekea kisibau.
20Kisha wakatengeneza tena pete mbili, wakazitia katika vipande vile viwili vya mabegani vya kisibau chini yake upande wake wa mbele papo hapo, vile vipande vilipounganika, juu ya masombo ya kisibau.
21Kisha wakakifunga kibati cha kifuani kwa kamba ya nguo nyeusi ya kifalme wakitia katika pete zake, tena katika pete za kisibau, kibati cha kifuani kipate kukaa juu ya masombo ya kisibau, kisiweze kusogeasogea hapo pake penye kisibau, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
(22-26: 2 Mose 28:31-35.)22Kisha wakatengeneza kanzu iliyokipasa hicho kisibau, nayo ilikuwa kazi ya fundi aliyejua kweli kufuma kwa nyuzi za rangi, yote nzima ilikuwa ya nguo nyeusi ya kifalme.
23Upande wa juu wa kanzu katikati yake ulikuwa na tundu lililofanana na tundu la shati ya chuma ya mpiga vita, kando lilizungukwa na taraza, lisipasuke.
24Penye upindo wa chini wa kanzu wakatengeneza komamanga kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu zilizo ngumu.
25Kisha wakatengeneza vikengele vidogo vya dhahabu tupu, wakavitia hivyo vikengele katikati ya komamanga kuuzunguka upindo wa chini wa kanzu po pote katikati ya komamanga,
26vikawa hivyo: kikengele kidogo na komamamnga, kikengele kidogo na komamanga, vivyo hivyo po pote kuuzunguka upindo wote wa chini wa kanzu, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
(27-29: 2 Mose 28:39-42.)27Wakamtengenezea Haroni na wanawe shati za bafta, nayo ilikuwa kazi ya fundi aliyejua kufuma kweli.
28Wakatengeneza nacho kilemba na kofia ndefu za nguo za bafta na suruali nyeupe za ukonge na za nguo za bafta na za nguo za kifalme nyeusi na nyekundu,
29nayo ilikuwa kazi ya fundi aliyejua kufuma kwa nyuzi za rangi, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
(30-31: 2 Mose 28:36-38.)30Kisha wakatengeneza kwa dhahabu tupu bamba kuwa taji takatifu ya pajini, wakachora humo machoro yaliyokuwa kama machoro ya muhuri kwamba: Mtakatifu wa Bwana.
31Wakalifunga kwa kamba ya nguo nyeusi ya kifalme, wapate kulifunga vema katika kilemba upande wake wa mbele, kama Bwana alivyomwagiza Mose.[#2 Mose 29:6; 3 Mose 8:9.]
32Hivyo ndivyo, kazi zote za kulitengeneza Kao la Hema la Mkutano zilivyokwisha, nao wana wa Isiraeli waliyafanya yote; kama Bwana alivyomwagiza Mose, waliyafanya yote kuwa sawasawa.
33Wakampelekea Mose hilo Kao: Hema na vyombo vyake vyote, vifungo, mbao, misunguo na nguzo zake pamoja na miguu,
34na chandalua cha ngozi nyekundu za madume ya kondoo na chandalua cha ngozi za pomboo na pazia kubwa la Hemani,
35Sanduku la Ushahidi pamoja na mipiko yake na Kiti cha Upozi,
36meza na vyombo vyake vyote na mikate ya kuwa usoni pa Bwana,
37kinara cha dhahabu tupu pamoja na taa zake zilizokuwa zimekwisha kupangwa mstari mmoja, na vyombo vyake vyote na mafuta ya taa,
38na meza ya dhahabu ya kuvukizia pamoja na mafuta ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri na pazia la hapo pa kuliingilia Hema,
39na meza ya shaba ya kutambikia pamoja na wavu wake wa shaba na mipiko yake na vyombo vyake vyote na birika pamoja na wekeo lake,
40na nguo za mapazia ya uani pamoja na nguzo zake na miguu yake, tena guo kubwa la pazia la langoni kwa ua pamoja na kamba zake na mambo zake na vyombo vyake vyote vya kutumikia katika hili Kao la Hema la Mkutano,
41tena mavazi mazuri ya kutumikia Patakatifu, ndiyo mavazi ya mtambikaji Haroni na mavazi ya wanawe ya kufanyia kazi za utambikaji.
42Wana wa Isiraeli waliyatengeneza yote na kuzifanya kazi hizi zote, ziwe sawasawa, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
43Mose alipoyatazama hayo yote, waliyoyafanya, akaona, ya kama wameyafanya kweli kuwa sawasawa, kama Bwana alivyoagiza; kwa hiyo Mose akawabariki.