The chat will start when you send the first message.
1Nilipotazama penye ukingo uliokuwa juu ya vichwa vyao Makerubi nikaona kilichokuwa kama kito cha Safiro, kikafanana sura yake kuwa kama kiti cha kifalme, kikaonekana kuwa juu yao.[#Ez. 1:22,26.]
2Akamwambia yule mtu aliyevaa vazi la ukonge, akasema: Ingia katikati ya magurudumu yaliyo chini ya Makerubi, uvijaze viganja vyako makaa ya moto yaliyoko katikati ya Makerubi, kisha yamwagie mji huu! Ndipo, alipopaingia machoni pangu.[#Ez. 9:2; Ufu. 8:5.]
3Makerubi yalikuwa yamesimama kuumeni penye hiyo Nyumba, yule mtu alipoingia, nalo lile wingu lilikuwa limeujaza ua wa ndani.
4Utukufu wa Bwana ukaondoka kwa Makerubi kwenda penye kizingiti cha kuiingilia hiyo Nyumba, hiyo Nyumba ikajazwa na lile wingu, ua nao ukajaa ung'avu wa utukufu wa Bwana.[#Ez. 1:4-28; Yes. 6:4.]
5Uvumi wa mabawa ya Makerubi ukasikilika mpaka kwenye ua wa nje, ukawa kama sauti ya Mwenyezi Mungu, akisema.
6Ikawa, alipomwagiza yule mtu aliyevaa vazi la ukonge kwamba: Chukua moto penye magurudumu katikati ya Makerubi, naye alipoingia na kusimama kando ya gurudumu,
7ndipo, Kerubi alipokunjua mkono wake kwenye Makerubi na kuupeleka penye moto uliokuwa katikati ya Makerubi, akautwaa, akampa mwenye vazi la ukonge na kuutia katika viganja vyake, naye akauchukua, akatoka.
8Kisha kukaoneka kwa Makerubi chini ya mabawa yao mfano wa mkono wa mtu.
9Nilipotazama mara nikaona magurudumu manne kando ya Makerubi, gurudumu moja kando ya Kerubi mmoja, vivyo hivyo gurudumu moja kando ya kila Kerubi mmoja; nilipoyatazama hayo nagurudumu, jinsi yalivyokuwa, yalikuwa kama kito cha Tarsisi.[#Ez. 1:15-16.]
10Yote manne mfano wao ulionekana kuwa mmoja, ulikuwa kama gurudumu moja lililomo ndani ya gurudumu lenziwe.
11Yalipokwenda yalikwenda pande zote nne pasipo kugeuka katika mwendo wao, kwani mahali hapo, kichwa kilipoelekea, ndipo, walipopafuata pasipo kugeuka katika mwendo wao.
12Nayo miili yao na migongo yao na mikono yao na mabawa yao, nayo magurudumu yalikuwa yamejaa macho po pote, penye magurudumu yote manne vilikuwa hivyo.
13Hayo magurudumu yakaitwa masikioni pangu Kimbunga.
14Kila Kerubi mmoja alikuwa na nyuso nne: Uso mmoja ulikuwa wa Kerubi, uso wa pili ulikuwa wa mtu, wa tatu ulikuwa wa simba, wa nne ulikuwa wa tai.
15Kisha Makerubi wakaenda juu. Hawa ndio nyama, niliyemwona kwenye mto wa Kebari.
16Makerubi walipokwenda, magurudumu yakaenda kando yao; tena Makerubi walipoyakunjua mabawa yao, waondoke katika nchi kwenda juu, magurudumu nayo hayakugeuka kuondoka kando yao.
17Waliposimama, nayo yakasimama; walipoinuka kwenda juu, nayo yakajiinua kwenda juu pamoja nao, kwani roho ya huyo nyama ilikuwa namo katika hayo magurudumu.
18Kisha utukufu wa Bwana ukatoka kwenye kizingiti cha kuiingilia hiyo Nyumba, ukasimama juu ya Makerubi.
19Makerubi wakayakunjua mabawa yao, wakaondoka katika nchi kwenda juu machoni pangu; ndivyo, walivyotoka hapo, hayo magurudumu hayo yakawa kandokando yao; wakasimama tena kwenye lango la Nyumba ya Bwana lielekealo maawioni kwa jua, nao utukufu wa Mungu wa Isiraeli ulikuwa juu yao.[#Ez. 10:1.]
20Huyo ndiye nyama, niliyemwona chini yake Mungu wa Isiraeli kwenye mto wa Kebari, nikajua, ya kuwa hao ndio Makerubi.
21Kila mmoja wao alikuwa na nyuso nne, tena kila mmoja alikuwa na mabawa manne, tena iliyofanana na mikono ya watu ilikuwa chini ya mabawa yao.
22Nazo nyuso zao hao zilikuwa zimefanana na zile nyuso, nilizoziona kwenye mto wa Kebari; ndivyo, zilivyoonekana kuwa, nao wenyewe walikuwa hivyo. Kila mmoja wakaenda na kufuata hapo, uso wake ulipoelekea.