The chat will start when you send the first message.
1Neno la Bwana likanijia la kwamba:[#Yer. 31:29.]
2Ninyi hulitumiaje katika nchi ya Isiraeli fumbo kama hilo la kwamba: Baba walipokula zabibu bichi, ndipo, wana alipokufa ganzi la meno.
3Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, hatakuwako tena kwenu atakayelitumia fumbo hili kwao Waisiraeli.
4Tazameni: Roho zote za watu ni zangu, kama ni roho za baba, au kama ni roho za wana, zote ni zangu; roho ya mtu atakayekosa ndiyo itakayokufa.
5Mtu akiwa mwongofu, afanye yaliyo sawa yaongokayo,
6asile vilimani juu, wala asiyatazamie kwa macho yake magogo ya kutambikia ya mlango wa Isiraeli, wala asimchafue mke wa mwenziwe, wala asimkaribie mwanamke mwenye siku zake,[#3 Mose 18:19-20.]
7wala asimtese mtu, ila aliyemkopa amrudishie aliyompa yeye ya kumwekea, asinyang'anye isiyo mali yake, wenye njaa awagawie vyakula vyake, wenye uchi awavike nguo,[#5 Mose 24:10-13; Sh. 15:3.]
8asikopeshee kupata faida, wala asichukue nyongeza za kupunja, mkono wake auzuie, usipotoe, aamue kwa kweli, mtu akigombana na mwenziwe,[#2 Mose 22:25.]
9ayafuate maongozi yangu na kuyashika mashauri yangu na kufanya yaliyo kweli, basi, mtu aliye hivyo ni mwongofu, naye atapata uzima wa kweli; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.
10Mtu kama huyo akizaa mwana aliye mkorofi, amwage damu, afanye moja tu la mabaya yale,
11yeye baba yake asiyoyafanya yote, kama anakula vilimani juu, au kama anamchafua mke wa mwenziwe,
12au kama anawatesa wanyonge na wakiwa, au kama ananyang'anya mali yake, au kama harudishi aliyopewa ya kumwekea mtu, au kama anayatazamia kwa macho yake magogo ya kutambikia, ayafanye yachukizayo,
13au kama anakopeshea kupata faida, au kama anachukua nyongeza za kupunja, basi, yeye atapata kabisa uzima wa kweli, ila atakufa kweli kwa kuyafanya hayo machukizo yote akitwikwa manza zake za damu, alizozikora.
14Huyu akizaa mwana, naye akiyaona makosa yote, baba yake aliyoyatenda, lakini akiyaona tu, asiyafanye yaliyo kama hayo,
15asile vilimani juu, wala asiyatazamie kwa macho yake magogo ya kutambikia ya mlango wa Isiraeli, wala asimchafue mke wa mwenziwe,
16wala asimtese mtu, wala asimtoze mtu mali za kumwekea, wala asinyang'anye isiyo mali yake, ila wenye njaa awagawie vyakula vyake, wenye uchi awavike nguo,
17auzuie mkono wake, usipotoe mnyonge, wala usichukue faida wala nyongeza za kupunja, ayafanye mashauri yangu na kuyafuata maongozi yangu, basi aliye hivyo hata kufa kwa ajili ya manza, baba yake alizozikora, ila atapata uzima wa kweli.
18Lakini baba yake aliyekorofisha kwa ukorofi wake, aliyemnyang'anya ndugu mali isiyo yake, aliyefanya katikati ya wenziwe wa ukoo yasiyo mema, mtamwona, yeye akifa kwa ajili ya hizo manza, alizozikora.
19Mkiuliza: Sababu gani mwana hatwikwi naye manza za baba yake? ni hivyo: mwana alifanya yaliyo sawa yaongokayo, akayashika maongozi yangu yote na kuyafanya, kwa hiyo atapata uzima wa kweli.
20Roho ya mtu atakayekosa ndiyo itakayokufa, lakini mwana hatatikwa manza za baba yake, wala baba hatatwikwa manza za mwanawe, nao wongofu wake mwongofu utamkalia, nao ubezi wake asiyemcha Mungu utamkalia.[#2 Mose 20:5; 4 Mose 26:11.]
21Lakini asiyemcha Mungu akirudi na kuyaacha makosa yake yote, aliyoyafanya, ayashike maongozi yangu yote na kufanya yaliyo sawa yaongokayo, basi, atapata uzima wa kweli, hatakufa.
22Nayo mapotovu yake yote, aliyoyafanya, hayatakumbukwa, ila atapata uzima kwa wongofu wake, alioufanya.[#Yes. 43:25; 44:22.]
23Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Mnaniwaziaje kwamba: Nitapendezwa, asiyenicha akifa? Je? Sitapendezwa, akirudi na kuziacha njia zake, apate uzima?[#Ez. 18:32; 33:11.]
24Lakini mwongofu akigeuka na kuuacha wongofu wake, afanye mapotovu, ayafanye hayo machukizo yote, wasiomcha Mungu wanayoyafanya, je? Atapata uzima? Sivyo, wongofu wote, alioufanya, hautakumbukwa, kwa kuwa amevunja maagano, naye kwa ajili ya makosa yake, aliyoyakosa, atakufa.[#Ez. 3:20.]
25Mkisema: Kumbe njia ya Bwana hainyoki! Sikieni, ninyi wa mlango wa Isiraeli: Je? Njia yangu hainyoki? Sizo njia zenu zisizonyoka?[#Ez. 33:17-20.]
26Mwongofu akirudi na kuuacha wongofu wake, afanya maovu, atakufa kwa ajili yao, kweli, kwa ajili ya hayo maovu, aliyoyafanya, atakufa.
27Tena asiyemcha Mungu akirudi na kumcha Mungu afanye yaliyo sawa yaongokayo, huyu ataipatia roho yake uzima.
28Akipata kuona, akirudi na kuyaacha mapotovu yake yote, aliyoyafanya, atapata uzima wa kweli, hatakfufa.
29Wao wa mlango wa Isiraeli wakisema: Njia ya Bwana hainyoki, inakuwaje, njia zangu zisiponyoka? Ninyi wa mlango wa Isiraeli, sizo njia zenu zisizonyoka?
30Kwa hiyo nitawapatiliza ninyi wa mlango wa Isiraeli kila mtu, kama njia zakezilivyo; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu. Rudini na kujigeuza na kuyaacha mapotovu yenu yote, yasiwawie tena makwazo ya kuwakosesha![#Ez. 33:11; Yes. 55:7.]
31Yatupeni mapotovu yenu yote mliyoyafanya ya kuwapotoa wenzenu, yawatoke ninyi! Kisha jipatieni mioyo mipya! na roho mpya! Mbona mnataka kufa, ninyi wa mlango wa Isiraeli?[#Ez. 36:26.]
32Kweli sipendezwi na kufa kwake mwenye kufa; ndivyo asemavyo Bwana Mungu. Kwa hiyo jigeuzeni, mpate uzima![#Ez. 18:23.]