The chat will start when you send the first message.
1Neno la Bwana likanijia la kwamba:[#Yes. 23.]
2Wewe mwana wa mtu, utungie mji wa Tiro ombolezo![#Hos. 9:13.]
3Uambie Tiro: Wewe ulikaa paingiapo bahari, ukachuuza katika nchi nyingi za baharini; hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wewe Tiro ulisema: Mimi nimetimiza uzuri wote.
4Kweli mipaka yako imo baharini ndani, nao waliokujenga walikutengeneza kuwa chombo chenye uzuri wote.
5Walikujenga pande zote mbili kwa mbao za mivinje ya Seniri, wakachukua mwangati huko Libanoni wa kukutengenezea mlingoti.[#5 Mose 3:8-9.]
6Mivule ya Basani waliitumia ya kukufanyizia makasia, vyumba vyako walivifanya kwa mbao za misagawi zilizopangiliwa kwa meno ya tembo, zilizotoka visiwani kwa Wakiti.
7Nguo za rangi zilizotoka Misri zilikuwa tanga lako zikawa hata bendera yako. Nguo za kifalme nyeusi na nyekundu zilizotokavisiwa vya Elisa zilikuwa chandalua chako cha kujifunika juu.[#1 Mose 10:4.]
8Waliokaa Sidoni na Arwadi walikuwa mabaharia wako, nao werevu wa kweli wa kwako, Tiro, ndio waliokuwa waelekeza chombo.
9Wazee wa Gebali na mafundi wake walikuwa kwako wa kuziziba nyufa zako. Merikebu zote za baharini zikafika kwako na mabaharia wao, wakauziana na wewe.[#1 Fal. 5:18.]
10Wapersia na Waludi na Waputi walikuwamo katika vikosi vyako vya askari wa kukupigia vita vyako; walipotundika ngao na kofia kwako waliuongea utukufu wako.
11Wana wa Arwadi na askari wako walizunguka penye kuta zako za boma, tena Wagamadi walikuwa katika minara yako; walipozitundika ngao zao po pote katika kuta zako, waliutimiza uzuri wako.
12Watarsisi wakaja kuchuuza kwako kwa ajili ya wingi wa vitu vya kwako, wakazinunua bidhaa zako kwa fedha na kwa vyuma na kwa bati na kwa risasi.
13Wagriki na Watubali na Wameseki walikuwa wachuuzi wako, wakatoa watumwa na vyombo vya shaba, wapate vitu vya kwako.[#Ez. 38:2.]
14Walio wa mlango wa Togarma walitoa farasi na farasi wa vita na nyumbu, wapate bidhaa zako.
15Wana wa Dedani walikuwa wachuuzi wako, watu wa nchi nyingi za baharini wakaja kuchuuza mikononi mwako: walikuletea meno ya tembo na mipingo kuwa malipo yao.
16Washami nao wakaja kuchuuza kwako kwa ajili ya wingi wa kazi zako, wakazinunua bidhaa zako kwa vito vyekundu na kwa nguo za kifalme na kwa nguo za rangi na kwa bafta nzuri na kwa marijani na kwa vijiwe vya yaspi.
17Wayuda nao wa nchi ya Isiraeli walikuwa wachuuzi wako, wakanunua vitu vya kwako kwa ngano za Miniti na kwa vikate vitamu na kwa asali na kwa mafuta na kwa uvumba.
18Wadamasko wakaja kuchuuza kwako kwa ajili ya wingi wa kazi zako na kwa ajili ya wingi wa mali, wakaleta mvinyo za Helboni na manyoya meupe sana ya kondoo.
19Wawedani na Wayawani walijipatia bidhaa zako na kuleta toka Uzali vyuma vilivyofuliwa vema, hata dalasini na vichiri vilikuwa malipo yao ya kukulipa.
20Wadedani walikuwa wachuuzi wako, wakanunua vyako kwa nguo nzuri za kuweka chini ya matandiko.
21Waarabu na wakuu wote wa Kedari nao wakaja kuchuuza mikononi mwako, wakanunua kwako kwa wana kondoo na kwa madume ya kondoo na kwa mbuzi.[#1 Mose 25:13.]
22Wachuuzi wa Saba na wa Raama nao walikuwa wachuuzi wako, wakazinunua bidhaa zako kwa manukato mazuri mno kupita yote mengine na kwa vito vya namna zote vyenye kiasi kikubwa na kwa dhahabu.
23Waharani na Wakane na Waedeni, nao wachuuzi wa Saba na Waasuri na Wakilmadi walikuwa wachuuzi wako.
24Hao walifanya biashara na wewe wakiuza nguo za urembo kama mablanketi makubwa ya kifalme yenye rangi nzuri na mazulia yenye machorochoro yaliyofungwa vema kwa kamba katika sanduku za miangati, wakanunua vitu vilivyouzwa kwako.
25Merikebu za Tarsisi zilikuwa kama wapangazi wako wa kupeleka vitu vya kwako, ukafurikiwa, ukatukuka sana huko ndani baharini.
26Wavutao makasia wakikupeleka kwenye vilindi vya maji, lakini upepo utokao maawioni kwa jua utakuvunja baharini kati.
27Ndipo, mali zako na bidhaa zako na vitu vya kwako na mabaharia wako na waelekeza chombo nao wazibao nyufa zako nao wachuuzi waliovichuuzia vya kwako nao wote, ulio nao wa kukupigia vita vyako, pamoja na mkutano wote wa watu wako waliomo mwako watakapoanguka kule baharini kati; itakuwa siku ile, utakapoangamizwa.
28Kwa sauti za makelele ya waelekeza vyombo vyako vitatetemeka viunga vyako.
29Ndipo, wote wavutao makasia watakaposhuka na kutoka merikebuni mwao mabaharia nao wote waelekezao vyombo baharini wasimame pwani,
30wakupalizie sauti zao na kukulilia kwa uchungu; watajitupia mavumbi vichwani pao na kujigaagaza majivuni.
31Watajikata nywele kwa ajili yako, vichwa viwe vyenye vipara, kisha watajifunga magunia, wakulilie kwa uchungu wa roho zao na kukuombolezea kwa kuliwa na uchungu.
32Watakapokulilia watakutungia ombolezo, wakuombolezee kwamba: Pako mahali gani panaponyamaza kimya kama Tiro ulioko baharini kati?
33Bidhaa zako zilipotoka baharini ulishibisha makabila mengi ya watu, kwa wingi wa mali zako na wa vitu vya kwako uliwapatia wafalme wa nchi mali nyingi.
34Lakini sasa umevunjwa, utoweke baharini kwa kutoswa vilindini penye maji mengi, navyo vitu vya kwako vya kuuza nao mkutano wa watu wako waliokuwamo mwako wamezama.
35Kwa hiyo wote wakaao kwenye bahari wanakustukia wafalme wao wakapigwa na bumbuazi, nazo nyuso zao zikatetemeka.
36Wachuuzi walioko kwenye makabila ya watu hukuzomea, kwa kuwa umegunduliwa na maangamizo, wala hutakuwapo tena kale na kale.[#Ez. 28:19.]